Ads

TRENI ZA ABIRIA ZA SEPTEMBA 19 NA 21- 2017 KWENDA NA KUTOKA BARA ZAFUTWA!

KAMPUNI YA RELI TANZANIA(TRL)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI (PRESS RELEASE)

Uongozi wa  Kampuni ya Reli Tanzania {TRL) unapenda kuwatangazia wateja wake na wananchi kwa ujumla  kuwa Kampuni inatarajia kufanya marekebisho ya uboreshaji wa miundombinu  ya  reli yake   katika  eneo la kati ya stesheni ya Morogoro na Mazimbu, ambapo daraja lililopo hapo eneo la km 209/7,  liliharibika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha  hivi karibuni.

Daraja hilo lilisombwa na maji ya mvua  mnamo Mei 13, 2017 , majira ya saa 5 usiku na  likafanyiwa matengenezo ya dharura tu. Kwa sasa tathmini ya kiufundi imefanyika na kuthibitisha  kuwa ni hatari kuendelea kupitisha treni hapo bila ya kuliimarisha  zaidi.

Uongozi wa kampuni umeona ni muda muafaka sasa kulifanyia marekebisho madhubuti na ya uhakika ili kuhakikisha usalama wa wateja wetu na wananchi kuwa unapewa kipaumbele.

Kwa maana hiyo ili kuweza kuifanya kazi hiyo kwa umakini Kampuni imefanya marekebisho kidogo ya ratiba yake ili kutoa nafasi ya  kufanikisha zoezi hilo la kulifanyia matengenezo madhubuti darala hilo.

Hivyo basi ile  treni yetu ya abiria ya siku ya Jumanne  tarehe 19 Septemba 2017 kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na Kigoma  na ile treni ya siku ya Alhamisi ya tarehe  21 Septemba, 2017 ya kutoka Kigoma na Mwanza kuja Dar es salaam zimefutwa na  hazitakuwapo.

Ratiba zetu nyingine zinabakia kama kawaida hadi hapo tutakapotangaza vinginevyo. Wananchi wanaombwa kuzingatia hilo na kutuunga mkono ili tuweze kuendelea kutoa huduma zetu kwa uhakika na usalama unaostahili.

Uongozi wa Kampuni  unawaomba radhi abiria na wananchi kwa ujumla kwa usumbufu utakaojitokeza
Atakayesoma  taarifa hili  amwarifu mwenzake.

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa TRL,
Ndugu Masanja Kungu Kadogosa
Dar es Salaam,
Septemba 15, 2017

MAELEZO YA PICHA:

Pichani katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Nd Focus Sahani akizungumza na Waandishi Habari makao makuu ya TRL leo asubuhi kuelezea umuhimu wa ukarabati wa daraja kati ya stesheni za Morogoro na Mazimbu na hivyo kulazimu kusitishwa safari za treni kwa muda wa siku 2! Pamoja naye ni Mkuu wa Usalama wa safari za reli Mhandisi Adolphina Ndyetabula kushoto na Mkuu wa Masoko Nd Shaaban Kiko.

No comments