Ads

VIFURUSHI VYA BIMA YA AFYA KUZINDULIWA RASMI ALHAMISI NOVEMBA 28, 2019.


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)Bw. Bernard Konga akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Shirika hilo zilizopo jengo la Ushirika jijini Dar es salaam leo wakati alipotangaza uzinduzi wa vifurushi vipya vya bima ya afya vya Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya vitakavyozinduliwa kesho kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Kulia ni Baraka Maduhu Meneja Takwimu na Utafiti (NHIF) na katikati ni Bi. Angella Mziray Meneja uhusiano wa (NHIF)

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)Bw. Bernald Konga wa pili kutoka kushoto akimzikiliza Bi. Angella Mziray Meneja uhusiano wa (NHIF) wakati alipokuwa akitambulisha wakuu wa vitengo mbalimbali wa NHIF walioshiriki katika mkutano katika ya shirika hilo na waandishi wa habari leo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)Bw. Bernard Konga akiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa vitengo mbaimbali wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mara baada ya mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.


Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), unatarajia kuzindua rasmi usajili wa wanachama kupitia mpango mpya wa vifurushi vya bima ya afya vya hiari ambao utawezesha wananchi kujiunga na huduma za Mfuko kulingana na mahitaji yao na kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote. Mpango huu utazinduliwa kesho Novemba 28, 2019 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. 

Mpango huu wa Vifurushi vya bima ya afya unatoa uwanja mpana wa wananchi kujiunga na bima ya afya kwa kujipimia kulingana na mahitaji ya huduma, ukubwa wa familia na umri. Vifurushi hivi  vimegawanywa katika makundi matatu yanayojulikana kama Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya. 

Kuanza kwa mpango huu kumekuja baada ya kuona uhitaji uliopa katika umma wa kuwa na uwigo mpana wa wananchi kujiunga na Mfuko huu. Hitaji la huduma hizi limedhihirika wazi baada ya kufanya majaribio ya mpango huu(Pilot test)  mwezi Septemba mwaka huu kwa muda wa wiki tatu ambapo mwitikio ulikuwa mkubwa kutoka kwa wananchi. Tathmini ya majaribio hayo ilitoa nafasi ya kufanya maboresho mbalimbali ya mpango huu na sasa uko tayari kwa ajili ya kuletwa kwa wananchi.

Kuanza kwa mpango huu ambao viwango vyake vya uchangiaji vinaanzia 192,000 kumezingatia hali halisi ya makundi yote na kutawezesha Watanzania wengi zaidi kujiunga na Mfuko na kuwa na uhakika wa kunufaika na huduma za matibabu wakati wanapougua hivyo kuondokana na changamoto za kukosa matibabu.

Aidha, uanzishwaji wa mpango wa vifurushi unawawezesha wananchi wengi zaidi kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha. Hivyo, kutokana na maboresho haya, wananchi wana fursa ya kukabiliana na gharama za matibabu ambazo zimekua zikiongezeka siku hadi siku na wakati mwingine kushindwa kuzimudu na kuangukia katika janga la umaskini au kifo. 

MADHUMUNI YA VIFURUSHI VYA BIMA YA AFYA

Kutoa fursa kwa wananchi katika sekta isiyo rasmi wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea ili kujisajili na kunufaika na huduma za matibabu.Kutoa fursa  kwa wananchi wengi zaidi  kupata huduma za matibabu kwa kuzingatia uhitaji wa huduma, umri na ukubwa wa familia.

Vifurushi hivi ni mahsusi kwa wananchi wenye kujali afya zao kwa kujiunga na bima ya afya na kuwa na uhakika wa kupata huduma mwaka mzima. Mwanachama atapatiwa  kadi ya matibabu ya Mfuko ambayo ataitumia kupata huduma katika vituo zaidi ya 7,500 vilivyosajiliwa na Mfuko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

MANUFAA KWA WANACHAMA

Wanachama wa vifurushi hivi watanufaika na huduma za matibabu kuanzia ngazi ya zahanati hadi Hospitali ya Rufaa ya Taifa katika vituo zaidi ya 7,500 Tanzania nzima ikiwa ni vya Serikali, Binafsi na vya Madhehebu ya Dini. Aidha, mwanachama atakwenda ngazi ya Hospitali ya Kanda ya Mkoa na Hospitali ya Rufaa ya Taifa kwa utaratibu wa rufaa. 

Vifurushi vyote vya Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya vimezingatia upana wa huduma kwa mwananchi ikiwa ni kuanzia gharama za kumwona daktari, vipimo, dawa, kulanza, upasuaji mkubwa na mdogo, matibabu ya kinywa na meno na mengineyo. Ukubwa wa kitita cha mafao utazingatia aina ya kufurushi ambacho mtu atachagua. 

JINSI YA KUJISAJILI NA MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA

Mfuko utafanya usajili katika ofisi zake ambazo ziko katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mfuko utaendesha pia kampeni za usajili katika maeneo ya watu kila mkoa.

Mwanachama anatakiwa kujaza fomu ya kujiunga ambayo inapatikana katika ofisi zote za Mfuko nchi nzima, au kupitia katika tovuti ya Mfuko www.nhif.or.tz.au kupitia katika mfumo wa kieletroniki.Mwanachama atapewa namba ya malipo (control number) ambayo ataitumia kufanya malipo kupitia benki au mitandao ya simu.Mwanachama anatakiwa kuwa na kitambulisho kimojawapo kati ya kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpiga kura, leseni ya udereva au hati ya kusafiria.Mwanachama atafanya malipo yote kwa mkupuo au kwa awamu kupitia utaratibu maalum wa benki.Mwanachama atapaswa kuwa na picha moja ya rangi ya ukubwa wa passport size.Mwanachama atapatiwa kitambulisho cha matibabu na kuanza kupata huduma zilizoainishwa katika kifurushi alichokichagua kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.Mwanachama anayemwandikisha mwenza atahitaji kuambatanisha picha moja ya mwenza ya rangi, nakala ya cheti cha ndoa, pamoja na kitambulisho kimojawapo cha mwenza kati ya kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpiga kura, hati ya kusafiria au leseni ya udereva.Mwanachama anayemwandikisha mtoto kama mtegemezi atahitajika kuambatanisha picha ya mtoto na nakala ya cheti cha kuzaliwa cha mtoto. Tangazo la kuzaliwa linaweza kuwasilishwa kama mbadala wa cheti cha kuzaliwa endapo mtoto ana umri wa chini ya miezi 6. 

Mfuko unatoa wito kwa wananchi kujiunga na bima ya afya kabla ya kuugua ili kunufaika na kuepuka usumbufu wa kugharamia matibabu endapo wataugua kabla ya kujisajili.

Mfuko unawakaribisha wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mnazi Mmoja kesho ili kuzindua kwa pamoja mpango huu. Aidha Mfuko unavishukuru vyombo vya habari vyote kwa kuwa wadau muhimu katika uelimishaji na uhamasishaji wa wananchi kujiunga na huduma za NHIF.

Imetolewa na:

Bernard Konga

Mkurugenzi Mkuu

MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA

No comments