Faru mzee kuliko wote duniani amekufa Ngorongoro Tanzania
Na Mwandishi Maalum, Arusha
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema Faru Fausta ambaye alikuwa mzee kuliko wote dunia amekufa jana Ijumaa Desemba 27, 2019.
Arusha. Faru Fausta (57) ambaye ndiye alikuwa Faru mzee duniani amekufa jana usiku Ijumaa Desemba 27, 2019.
Faru huyo ambaye alikuwa amehifadhiwa kwenye Banda maalum ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa zaidi ya miaka mitatu amefariki kutokana na maradhi.
Faru Fausta alikuwa amehifadhiwa kwenye banda hilo ili kumlinda kuliwa na wanyama wengine hasa fisi kutokana jicho lake moja kutoona .
Kamishna wa uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk Fredy Manongi amethibitisha kifo cha faru huyo.
Dk Manongi amesema faru huyo ambaye alikuwa amehifadhiwa alikuwa amepoteza uoni na hivyo kushindwa kujipatia chakula tofauti na ambavyo alikuwa akilishwa.
Alisema Faru Fausta alivunja rekodi ya kuishi iliyokuwa inashikiliwa na Faru aliyepewa jina la Sana wa Afrika Kusini ambaye alifariki akiwa na miaka 55.
Faru Fausta kwa muda mrefu amekuwa akitumia majani aina la lucini kiasi cha maroba 250 kila baada ya miezi minne na kuigharimu mamlaka hiyo kiasi cha Sh5 milioni hatua ambayo ilisababisha mamlaka hiyo kupanda majani hayo.
Faru huyo pia alikuwa akipatiwa miwa ili kuimarisha afya yake.
Kwa upande wake, Daktari wa Wanyama katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Athanas Nyaki alisema, Faru Fausta ililazimika kuhifadhiwa kutokana na kuanza kushambuliwa na fisi.
Alisema kutokana na jicho moja la Faru huyo kutoona na pia kukabiliwa na uoni hafifu katika jicho jingine, aliwahi kushambuliwa na fisi na kusababishiwa majeraha kadhaa.
Hata hivyo, Dk Nyaki alisema tangu Faru huyo amehifadhiwa afya yake iliimarika na majeraha yalipona lakini hali ilibadilika juzi usiku na kufa.
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, ni moja ya hifadhi chache nchini ambazo, zimeweza kuwa na Faru wengi, ambao wanalindwa saa 24 kwa mitambo maalum ili kuwazuiwa kuuawa na majangili.
Majangili wamekuwa wakiwaua faru ili kuchukua pembe zao ambazo huuzwa katika nchi za Mashariki ya Kati kutokana na imani potofu kuwa unga wake ni dawa ya magonjwa kadhaa ikiwapo nguvu za kiume.
Post a Comment