Ads

Kampuni saba za simu zakumbana na rungu la TCRA, zapigwa faini Sh5.9 bilioni



 Na Mwandishi Maalum,Dar es Salaam. 



Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria wa TCRA, Dk Philip Filikunjombe 

Kwa muhtasari

Kampuni saba za simu nchini zimepigwa faini baada ya kubanikia kushindwa kutekeleza masharti ya leseni na kukidhi viwango vya ubora wa huduma kwa mujibu wa Kanuni za Ubora wa Huduma za mwaka 2018.


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imezipiga faini  kampuni saba za simu baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya leseni na kukidhi viwango vya ubora wa huduma kwa mujibu wa Kanuni za Ubora wa Huduma za mwaka 2018.

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria wa TCRA, Dk Philip Filikunjombe katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Jumapili Desemba 29, 2019 kuwa adhabu hiyo ilitolewa Desemba 24, mwaka huu.

Dk Filikunjombe amezitaja kampuni hizo kuwa ni Airtel Tanzania plc Sh1.6bilioni , Tanzania Telecommunications Corporation (TTCL) Sh1.6 bilioni, Viettel Tanzania plc (Halotel) Sh900 milioni, Zanzibar Telecom plc Sh850 milioni, MIC Tanzania plc (Tigo)- Sh500 milioni na Vodacom Tanzania plc-Sh450milioni.

Amesema kwa mujibu wa taarifa ya upimaji wa ubora wa huduma kati ya Julai, Agosti na Septemba, 2019, imebainisha kampuni za simu nchini zimeshindwa kukidhi baadhi ya vigezo vya ubora wa huduma kinyume na matakwa ya Kanuni za Ubora wa Huduma, 2018.

“TCRA imetoza faini hizo kwa mujibu wa sheria ikiwa na lengo la kushinikiza kampuni za simu nchini kuwajibika kwa kutoa huduma bora zinazokidhi vigezo vilivyowekwa, ili mtumiaji wa huduma za mawasiliano nchini, apate huduma bora na inayolingana na thamani ya malipo anayoyafanya kwa huduma hizo,” alifafanua.

Amesema baadhi ya vigezo ambavyo watoza huduma za mawasiliano ya simu wanatakiwa kuzingatia na kuhakikisha wanafikia ni pamoja na upatikanaji wa mtandao wa uhakika.

Vigezo vingine ni kiwango cha simu zinazoshindwa kuunganishwa, kiwango cha simu zinazokatika wakati mtu anazungumza, ubora wa sauti na upatikanaji na ufanisi wa huduma za ujumbe mfupi.

Dk Filikunjombe amebainisha kuwa kanuni ya 20 ya Kanuni za Ubora wa Huduma, 2018, inatamka kwamba mtoa huduma yeyote atakayeshindwa kukidhi vigezo vya ubora wa huduma, atozwe faini isiyopungua fedha za Kitanzania Shilingi milioni tano kwa kila kigezo alichoshindwa kufikia na faini ya milioni tano kwa kila siku ambayo watashindwa kukidhi viwango.

Ameeleza kuwa upimaji wa ubora wa huduma ni zoezi endelevu linalofanywa kila mwezi ambapo taarifa juu ya hali ya ubora wa huduma hutolewa kwa kila robo mwaka.

“Hatua hii ya faini kwa kampuni ya simu, imetekelezwa kutokana na taarifa ya ubora wa huduma ya robo ya kwanza ya mwaka, miezi ya Julai, Agosti na Septemba, 2019,” alisisitiza.


 


No comments