Ads

Madaktari feki wakamatwa wakitoa huduma ya mifugo

Na Mwandishi Maalum Tanga

Madaktari bandia wakiwa chini ya ulinzi wa Maofisa wa Idara ya Mifugo na Uvuvi. Kutoka kushoto ni Watuhumiwa Raphael Francis na Evance Mushi.

 IDARA ya Mifugo na Uvuvi Jiji la Tanga, inawashikilia Madaktari wawili wa bandia waliokuwa wakitoa chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu kwa ng’ombe bila kusajiliwa na Baraza la Mifugo (VTC).

 Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Jiji la Tanga Daktari Erick Mosha alisema jana madaktari hao walikutwa juzi wakitoa huduma ya afya ya mifugo bila kusajili huku wakitoza bei kubwa kuliko bei elekezi iliyotolewa na serikali.

Aliwataja Madaktari hao bandia kuwa ni Evance Mushi (24) na Raphael Francis (25) wakazi wa Kange walikokutwa wakitoa huduma hiyo.

 “Tumewakamata huko Kange-Kasera wakitoa huduma za afya ya mifugo wakiwa hawana kibali…Huduma hiyo ni kuchanja na kutoa ugonjwa wa homa ya mapafu kwa ng’ombe,” alisema Dkt Mosha.

Dkt Mosha alisema kwa kawaida huduma hizo zinatolewa na Madaktari wa Mifugo wakiwa chini ya usimamizi wa daktari aliyesajiliwa na VCT.

 Suala jingine alilosema Dkt Mosha ni kwamba Madaktari hao bandia, wamekuwa wakitoza Sh 5,000 kwa Ng’ombe mmoja mkubwa na ndama wamekuwa wakitoza Sh 3,000.

 Alisema bei elekezi kwa kuchanja ng’ombe mmoja iliyotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi ni chini ya Sh 800 na siyo vinginevyo na dawa hizo hazitolewi kwa Madaktari wasiokuwa na sifa.

 “Wale vijana ni Madaktari kweli wa mifugo lakini hawakusajili na Baraza hivyo walikuwa wakifanya makosa kutoa huduma hiyo,” alisema.

Dkt Mosha akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani.

Dawa za mifugo walizokutwa nazo madaktari hao

No comments