Ads

Watoto wanaoishi mazingira hatarishi wapata msaada sare za shule


    Na Mwandishi Maalum, Korogwe

Kaimu Mkurugenzi Wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Joseph Gweba akimkabidhi vifaa vya shule Issa Haji Kivule.

WATOTO 50  wanaoishi katika mazingira hatarishi wa Kijiji cha Majengo-Mswaha wilayani hapa, wamepatiwa msaada wa sare za shule pamoja na madaftari ili weweze kuendelea masomo.

Wakitoa vifaa hivyo, vikundi 12 vilivyokuwa chini ya Mpango wa Wote Tuwalee (LIMCA) ulioratibiwa na Shirika la Kusaidia Wazee, Watoto na Wanawake (TAWOREC), walisema watoto walichaguliwa kutoka watoto 250 waliokuwa na mahitaji yanayofanana.

Akisoma risala iliyoelezea vifaa walivyowapa watoto, Bw Adam Shaban alisema vifaa hivyo vimenunuliwa kutokana na michango ya Wanavikundi hivyo ili kuwasaidia watoto hao wanaokabiliwa na changamoto ya kusoma.

“Watoto 50 tutawapa sare za shule,madaftari,kalamu na vifaa vinavyotumika shuleni, lakini pia wanafunzi wanaofanya vizuri huwa tunawapa zawadi mbalimbali,” alisema  Shaban.

Shaban alisema vifaa hivyo vinathamani ya sh. 600,000 na vikundi hivyo vitaendelea kuchanga ikiwemo kukopeshana wenyewe kwa ajili ya kuinuana kiuchumi.

Akielezea changamoto, alisema kuwa wanakosa mitaji ya kuendelea kusaidiana kiuchumi ikiwemo kuwasaidia watoto wengi zaidi hivyo wameiomba serikali kuwapa mikopo ili waongeze mitaji yao.

Awali Mwalimu Mustafa Salimu akielezea historia ya vikundi hivyo alisema walivianzisha mwaka 2013 katika kijiji hicho kikiwa kikundi kimoja chenye watu 22 wakiwa wanawake watupu na sasa vimekuwa 12 kupitia Shirika la Kimarekani la World Education.

“Tulianza tukiwa 22 na kila mwishoni mwa juma tulikuwa tukichanga kila mmoja sh. 200 ambazo zimetuwezesha kuwasaidia watoto,” alisema.

Mwakilishi wa Shirika la TAWOREC la mkoani Tanga, Zamia Shabani alisema walipata wafadhili wa Kimarekani ambao waliwajengea uwezo vikundi hivyo hadi vikafikia kuweka pesa ambazo kiasi kingine kimetengwa kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Aliwaasa viongozi wa vikundi hivyo kuhakikisha fedha inayotengwa kwa ajili ya watoto haipaswi kuliwa na kwamba Jamii inawajibu wa kusaidia kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili waweze kufikia malengo yao.

Alisema Shirika la TAWOREC limekuwa likitoa elimu kuhusu migogoro ya ndoa,ukatili wa kijinsia, kiuchumi, kisaikolojia na ukatili dhidi ya watoto.

“Tunaomba Jamii isaidie kutatua matatizo ya ukatili dhidi ya makundi mbalimbali,” alisema.

Akitoa msaada huo kwa watoto Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Joseph Gweba aliwataka Wazazi na Walezi kuhakikisha watoto wanakwenda shuleni ili kusaidia mapambano ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

“Wazazi tunatakiwa tuwalee watoto katika misingi na taratibu zilizopo. Serikali kwa kushirikiana na mashirika imekuwa ikisaidia jitihada mbalimbali za kusaidia, watoto.” Alisema na kueleza moja ya mipango ya Serikali ni kutoa elimu bure.

Alisema Serikali kutoa elimu bure imeweza kupunguza gharama kwa Wazazi na Walezi ili wasikwame au kushindwa kuwapeleka Watoto Shuleni na kwamba sasa ni jukumu lao kuhakikisha watoto wanakwenda shuleni kupata elimu.

Aliyashukuru Mashirika na Vikundi vinavyojitolea kusaidia Jamii ikiwemo watoto hao kuwapa sare na vifaa vya shuleni akielezea yote hayo ni malengo na mipango ya kusaidia juhudi hizo.Halima Mussa akikabidhiwa sare za shule na Kaimu Mkurugenzi. Wanachama wa kikundi kimojawapo wakifuatilia sherehe hizo za kukabidhi vifaa vya shule.

No comments