Ads

RAIS MAGUFULI AWAAPISHA MABALOZI WA AFRIKA KUSINI, ZIMBABWE, NAMIBIA NA NIGERIA



Rais  Dkt. John Magufuli  leo Januari 14, 2020 amewaapisha Mabalozi wanne aliowateua hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Nigeria.

Walioapishwa ni Mej. Jen (Mstaafu) Gaudence Salim Milanzi anayekuwa Balozi wa Tanzania Pretoria - Afrika Kusini, Dkt. Modestus Francis Kipilimba anayekuwa Balozi wa Tanzania Windhoek – Namibia, Prof. Emmanuel David Mwaluko Mbennah anayekuwa Balozi wa Tanzania Harare – Zimbabwe na Dkt. Benson Alfred Bana anayekuwa Balozi wa Tanzania Abuja – Nigeria.

Mabalozi wakila kiapo


Baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya wiki 2 kuanzia sasa na amewasisitiza kwenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia maslahi ya Taifa hasa kiuchumi na kuwawezesha Watanzania kupata ajira katika fursa zilizopo katika nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amewataka Mabalozi hao kufuatilia maeneo yote ambayo Mhe. Rais Magufuli alikubaliana na Waheshimiwa Marais wenzake alipotembelea nchi hizo hivi karibuni, na pia kuitangaza vyema Tanzania ambayo kwa sasa inapiga hatua kubwa katika maeneo mengi.

Hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

Kabla ya kuwaapisha Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.


No comments