Ads

JESHI LA MAGEREZA KUJITEGEMEA KWA KUTUMIA RASILIMALI ZAKE



Kamishna Jenerali Suleiman Mzee akiwahutubia Maafisa Magereza Waandamizi Jijini Dodoma leo


Na ASP. Lucas Mboje, Dodoma

MKUU wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee, amesema kuwa Jeshi hilo limeanza kuyafanyia kazi maagizo mbalimbali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kuhakikisha linatekeleza mikakati ya kuanza kujitegemea ikiwemo kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Amesema hatua hiyo inaanza mara moja kwani Jeshi hilo lina uwezo mkubwa wa kutumia rasilimali zake zilizopo ndani ya Jeshi ambazo zinaweza kuliwezesha kujitegemea bila kutegemea bajeti ya Serikali.

Kamishna Jenerali Suleiman Mzee amesema hayo leo jijini Dodoma katika kikao kazi cha maafisa waandamizi wa Jeshi hilo kutoka mikoa yote Tanzania Bara ambacho kililenga kupeana mikakati ya namna ya kufanikisha mpango wa kujitegemea.

“Magereza kujitegemea inawezekana kwani tunazo rasilimali nyingi ikiwemo mashamba ya kilimo, mifugo, wataalam wakutosha na nguvu kazi ya wafungwa ambapo tukizisimamia vizuri na kuachana na ubinafsi tutaliwezesha Jeshi letu la Magereza kujitegemea”, alisema Kamishna Jenerali wa Magereza Suleiman Mzee.

Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali Suleiman Mzee ametoa maelekezo kwa wakuu wote wa Magereza Mikoa yote Tanzania Bara kuhakikisha kuwa wanaanza kujitegemea kwa asilimia mia moja kwa chakula cha wafungwa na huduma nyinginezo kwani kila mkoa unazo fursa nyingi za kuliwezesha Jeshi hilo kujitegemea.



Maofisa Magereza wakimsikiliza kwa makini Kamishna Jenerali Suleiman Mzee

“Kuanzia mwezi ujao, Machi 1, 2020 kila Mkuu wa Magereza Mkoa(RPO) lazima ahakikishe kuwa anajitegemea katika mkoa wake na lazima mkubali kufanya mabadiliko haya bila visingizio. Atakayeshindwa kujitegemea nitamwajibisha mara moja”, amesisitiza Jenerali Suleiman Mzee.

Aidha, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee ameongeza kuwa tayari ameanza maandalizi ya ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza pamoja na nyumba za watumishi wa Jeshi hilo jijini Dodoma kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizopo Jeshini.

Kikao kazi cha Maafisa Waandamizi wa Magereza ndicho kikao cha juu cha uongozi ambacho huwakutanisha Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu, Wakuu wa Magereza wa Mikoa, Wakuu wa Vyuo, Mkuu wa Kikosi maalum na Mkuu wa Sekondari Bwawani. Kikao hicho hulenga kuwekeana mikakati mbalimbali ya namna ya kuboresha utendaji kazi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao waliokabidhiwa.


No comments