Ads

JUMLA YA MALI ZENYE THAMANI YA BILIONI 58 ZATAIFISHWA NA SERIKALI !

Na Mwandishi Maalum  Dar



Mkurugenzi wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mhe. Biswalo Mganga akizungumza  wakati wa kukabidhi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James mali  zilizotaifishwa kutokana na  kesi zinazohusiana na uhalifu sambamba na fedha zilizolipwa  kutokana na kesi za madini zilizopo katika akaunti ya AFR katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zenye thamani ya TZS Bilioni 58.6 kutoka kushoto ni Waziri wa Madini Mh. Dotto Biteko na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome .



Mhe Dotto Biteko wa Waziri wa  Madini wa pili kutoka kulia, Dk. Agustine Mahiga Waziri wa Katiba na Sheria na Dk. Philip Mpango Waziri wa Fedha na Mipango wakionesha madini yaliyorejeshwa kutoka nchini Kenya baada ya kutaifishwa na Serikali kwa amri ya Mahakama ya Tanzania. Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mhe. Biswalo Mganga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome na kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe Dotto James na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BoT Profesa Florens Luoga.

 

Mkurugenzi wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mhe. Biswalo Mganga akionesha moja ya kipande cha madini ya dhahabu yaliyokabidhiwa rasmi kwa serikali leo  baada ya kutaifishwa kwa amri ya mahakama huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango  Mhe Dotto James akishuhudia.



Baadhi ya vipande vya dhahabu vikiwa katika begi maalum.



Mhe Dotto Biteko Waziri wa  Madini akizungumza katika makabidhiano hayo yaliofanyika kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania BoT jijini Dar es salaam leo.



Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo.



Waziri wa Sheria na Katiba Dkt. Agustine Mahiga akizungumza katika makabidhiano hayo.



Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BoT Profesa Florens Luoga akitoa shukurani zake kwa hafla hiyo kufanyika katika kumbi za benki hiyo lakini pia kuaminiwa kwa ajili ya kuhifadhi mali hizo za Serikali.



Makasha mbalimbali yaliyohifadhi dhahabu na fedha yakiingizwa ukumbini kabla ya kukabidhiwa rasmi.

 

Baadhi ya viongozi wa taasisi mbalimbali mbalimbali za  Serikali, Mahakama, Sheria na Katiba na Madini wakiwa katika hafla hiyo

 

SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefanikiwa kupata amri za kutaifisha mali na fedha zinazohusiana na uhalifu sambamba na fedha zilizolipwa  kutokana na kesi za madini zilizopo katika akaunti ya AFR katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zenye thamani ya TZS Bilioni 58.6.

Akizungumza na Waandishi wa Vyombo vya Habari leo Jumatatu (Februari 10, 2020) Jijini Dar es Salaam, wakati wa makabidhiano ya utaifishaji wa mali za uhalifu mali hizo baina ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na DPP na Katibu Mkuu Hazina, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga alizitaja mali hizo ni pamoja na Nyumba, magari, viwanja, mashamba, mbao na jahazi.

Mkurugenzi huyo alisema Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, mbali na fedha hizo, imepata amri ya kutaifisha nyumba 24, magari 65, viwanja 9, mashamba 2, mbao 6894, jahazi 1 iliyotokana na uvuvi haramu kwenye ukanda wa bahari kuu ya Tanzania pamoja na boti moja ya Yohanda iliyohusika katika kuingiza nchini vipodozi vyenye sumu.

‘’Kwa ufupi ukichukua thamani ya madini na kiasi cha fedha zilizomo kwenye akaunti ya Asset Forfeiture Recovery (AFR) ya BOT unapata TZS 19,639,782,781.46 ambazo nakabidhi, hivyo ukijumuisha thamani ya madini yote, fedha iliyolipwa kutokana na kesi zinazohusiana na madini pamoja na fedha zilizomo kwenye akaunti ya AFR jumla yake inakuwa TZS 58,604,375,783.56’’ alisema Biswalo.

Mhe Biswalo alisema tangu kuzinduliwa rasmi kwa ofisi hiyo mwezi Agosti mwaka 2018, Ofisi yake imefanikiwa kutaifisha jumla ya kilo 397.937 za dhahabu zenye thamani ya TZS Bilioni 32.2 zilizokuwa zikitoroshwa nje ya nchi na kuisababishia serikali kukosa mapato, ambapo kati ya hizo, kilo 351.76 za dhahabu zenye thamani ya TZS Bilioni 29 zimeshakabidhiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambaye ndiye mtunzaji wa mali za Serikali.

‘’Leo hii nakabidhi jumla ya kilo 46.177 za dhahabu zenye thamani ya TZS Bilioni 3.2, pamoja na hayo tumeendesha kesi na kufanikiwa kupata amri za kutaifisha madini aina ya Almas, Tanzanite, Silver, Amethyst, Rhodolite, Bati, Blue Sapphire, Spinel, Ruby, Tourmaline, Acuamarine, ambapo jumla ya thamani ya madini yote yaliyotaifishwa pamoja na faini zilizolipwa na washitakiwa ni TZS Bilioni 42.2’’ alisema Biswalo.

Katika hatua nyingine, Biswalo alisema kufuatia marekebisho ya sheria mbalimbali Na. 11 ya mwaka 2019, Ofisi yake imeendesha kesi katika zoezi la washtakiwa kukiri makosa yao ambapo jumla ya TZS Bilioni 12.3 zimeshalipwa kama kodi iliyokwepwa, faini na  fidia katika akaunti maalum iliyopo Benki Kuu ya Tanzania.

Akifafanua zaidi Biswalo alisema zoezi la urejeshaji wa fedha kwa washitakiwa 341 ambao hawajamaliza kutimiza makubalino linaendelea na makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa kama yalivyosajiliwa kwa amri ya mahakama, ambapo katika madai hayo Serikali inawadai washitakiwa wote kiasi cha TZS Bilioni 32.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Augustine Mahiga alisema wakati umefika kwa Watanzania kunufaika kikamilifu na uwepo na rasilimali zao ikiwemo madini ambayo katika miaka ya nyuma hayakuwa na usimamizi madhubuti, hivyo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa yanaleta manufaa endelevukwa wananchi wake.

Kwa upande wake Waziri wa Madini, Dotto Biteko aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kuzingatia sheria kwa kuwa serikali haitokuwa na msamaha kwa mtu yoyote atakayejihusisha na vitendo vya utoroshaji wa rasimali madini nje ya nchi kwani yamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuinyima nchi mapato.

Aidha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema zoezi la utaifishaji wa mali za uhalifu, ni dalili tosha kuwa Tanzania sio nchi maskini na hivyo hakuna sababu ya Serikali kwenda kukopa nje ya nchi na badala yake itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa raslimali zake zitalindwa kwa nguvu zote.

(PICHA ZOTE NA JOHN BUKUKU-FULLSHANGWEBLOG-DSM)


No comments