Ads

PUMA WATAKIWA KUPELEKA HUDUMA VIJIJINI


Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza akiwa mgeni rasmi katika sherehe za utoaji tuzo na zawadi kwa waendesha vituo vya mafuta vya Puma Energy Tanzania Limited, Februari Mosi, 2020 jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameitaka Kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited kupeleka huduma zake katika mikoa yote nchini na hasa maeneo ya vijijini.
 
Amesema kwamba sera ya serikali ni kupeleka nishati za umeme, gesi na mafuta katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya vijijini.
 
Dkt Kalemani aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana Februari Mosi, 2020 wakati akizungumza akiwa mgeni rasmi katika sherehe za utoaji tuzo na zawadi kwa waendesha vituo vya mafuta vya Puma Energy Tanzania Limited.
 
"Maagizo yangu ni kwamba mfike mikoa yote nchini ambayo hamjafika ili ipate huduma. Najua hamjafika Katavi, Rukwa, Kigoma, Geita, Mara, Simiyu. Nendeni mikoa hiyo," aliagiza Dkt Kalemani.
 
Aliongeza, "Sera yetu ni kufikisha nishati vijijini. Nishati hizo ni umeme, gesi na mafuta. Kwa gesi tumefanya vizuri sana na umeme unaendelea kusambazwa vijijini. Ninyi vituo vya mafuta vijijini bado tuko nyuma. Anzisheni vijijini sio mijini."



Katika picha hizi mbili Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwakabidhi washindi mbalimbali ambao ni waendesha vituo vya mafuta vya Puma Energy Tanzania Limited, tuzo na zawadi katika hafla iliyofanyika Februari Mosi, 2020 jijini Dar es Salaam. Waziri alikuwa Mgeni Rasmi katika sherehe hiyo.

Alisema si jambo jema kuona wananchi wanabeba mafuta katika madumu au chupa za maji za plastiki huku yakihifadhiwa nyumbani jambo linalohatarisha usalama wa wananchi.
 
Aidha, aliwaagiza kuongeza ushindani, huku akiwapongeza kwa kutoa ajira 149 za kudumu kwa Watanzania na za jumla takribani 800 kwa wazawa.
 
Dkt Kalemani alitoa shukrani kwa bodi na menejimenti kwa kusimamia ajira hizo na kuhakikisha Watanzania wengi wanaajiriwa katika kampuni hiyo.
 
Puma Energy Tanzania limited inamilikiwa kwa asilimia 50 na Serikali ya Tanzania kupitia Msajili wa Hazina na Kampuni ya Puma Investments Limited.
 
Kutokana na hilo, aliipongeza kwa kutoa gawio kwa Serikali ambalo limekuwa likiongezeka kutoka shilingi bilioni 9.0 mwaka 2018 na shilingi bilioni 11.0 mwaka jana. Aliwataka mwaka huu waongeze kufikia zaidi ya shilingi bilioni 13.
 
Akizungumzia sekta ya mafuta kwa ujumla, aliwapongeza wadau wote wanaoagiza mafuta kwa pamoja kwa kuiwezesha nchi kuwa na mafuta ya kutosha kila wakati.
 
Alisema kuna ziada ya mafuta ya dizeli ya siku 28 lita milioni 197, petroli ziada ya lita 97.04 kwa siku 38 na mafuta ya ndege ziada ya lita milioni 30.9 kwa siku 56, hivyo hakuna hofu katika nishati hiyo.
 
Alimpongeza Rais John Magufuli kwa usimamizi mzuri wa sekta ya nishati na kusimamia uanzishaji wa mfumo wa kuagiza mafuta kwa pamoja.
 
Pia, Waziri aliwapongeza washindi na wote waliopata zawadi katika sherehe hizo.
 
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania Limited, Dominic Dhanah alisema hizo ni tuzo za kwanza za aina yake kufanyika nchini.
 
Dhanah alisema lengo la tuzo hizo ni kutoa hamasa na kuwapa changamoto waendesha vituo hao kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wao kote nchini.
 
"Sisi ni kampuni namba moja kwa ukubwa wa soko tunalolihudumia Tanzania, tukihudumia takribani asilimia 15 ya soko lote Tanzania, lakini pia tukiwa tunatambulika kwa ubora wa huduma zetu, na zaidi ubora wa mafuta yetu na bidhaa zetu nyingine.
 
"Kwa sasa matamanio yetu makubwa ni kukua zaidi na kuwa kampuni ya kwanza katika soko katika kipengele hiki cha "retail", alisema Dhanah.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Puma Energy, Dkt Selemani Majige alisema wamepokea sifa na changamoto walizopewa na Waziri na kuahidi kuzifanyia kazi ili kuhakikisha kampuni hiyo inazidi kufanya vizuri zaidi na kuchangia zaidi katika pato la serikali kwa kodi na gawio.
 


No comments