ALIYOZUNGUMZA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI DKT. HASSAN ABBASI WAKATI WA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI LEO MACHI 15, 2020 JIJINI DODOMA
Nianze na ugonjwa wa Corona, pamoja na nchi zaidi ya 100 kuathirika sisi bado tuko salama na tuendelee kuchukua tahadhari.
Kama nchi Tumejiandaa katika kanda zote, pale Dar es Salaam na katika maeneo mengine kuna maeneo tumeyatenga na iwapo akitokea mtu mwenye *Virusi vya Corona* atapelekwa huko, tunafuatilia na tunapokea maoni ya wataalamu ili kama kuna hatua zaidi zitaendelea kutangazwa. Watu wasipaniki lakini wachukue tahadhari.
Kuhusu nchi yetu na uchumi, IMF katika report yao ya Machi 5, 2020 wamesema uchumi wetu uko imara na wametathmini pia deni letu la Taifa na kuona ni himilivu.
IMF wamevutiwa pia mapambano dhidi ya rushwa na wametambua namna tulivyowekeza katika sekta ya afya, elimu na miundombinu.
Utekelezaji katika sekta mbalimbali unaendelea kwa kasi sana na leo nitaeleza maeneo maachache kama ifuatavyo;
▪Mpaka kufikia Machi mwaka huu Serikali kupitia Wizara ya Ardhi imetatua migogoro ya Ardhi zaidi ya 10,000
▪ Mapato kwenye sekta ardhi yameongezeka kutoka Tsh Bil. 54.1 mwaka 2014/15 hadi kufikia Tsh Bil. 100 kwa mwaka 2018/19.
Mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria unaogharimu Tsh Bil. 600 na kunufaisha wakazi Mil.1.8 katika vijiji zaidi ya 90 katika maeneo yote ya mradi kuanzia kanda ya ziwa hadi kufikia Tabora mjini, Igunga na Nzega.
Pia mradi umeanza kunufaisha watumiaji na kwa mara ya kwanza watu wa Tabora wanafaidika na maji ya kutoka mbali kabisa Ziwa Victoria. *Huu ni uwekezaji mkubwa wa Serikali*
Maandalizi ya ujenzi wa majengo ya ofisi awamu ya pili na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami (km 40) katika mji wa Serikali Mtumba unaendelea
Watumishi 15,361 wa Wizara na Taasisi za Serikali wamehamia Makao Makuu ya Serikali, Dodoma, ujenzi wa awali wa Ofisi za Serikali katika mji wa Serikali, Mtumba umekamilika
Mchezo wa Simba na Yanga uliochezwa Machi 8, 2020 umeweka rekodi ya mapato kwa kuingiza shillingi Milioni 545.4 kwa timu na mapato ya Serikali shillingi milioni 153.2 ambayo hayajawahi kupatikana wakati wote katika historia ya Simba na Yanga
Lakini tunaweza kupata mapato zaidi, Natoa onyo, asije mtu akaleta ujanja ujanja katika mechi zote zinazochezwa kwa kuanzia katika viwanja vya taifa vya Dar es Salaam, na nchi nzima kwa ujumla.
Tuzisaidie timu, zimekuwa masikini kwa muda mrefu, tunataka kuhakikisha vilabu na serikali vinapata mapato stahili.
Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), zimesaini mikataba mitano inayohusu utekelezaji wa miradi mitatu ya kimkakati kwa mkopo wa masharti nafuu ya Dola Mil 495.59 ambayo ni sawa na TZS Tril 1.14 zitakazowezesha kutekeleza miradi mbalimbali kama ifuatavyo;
▪Ujenzi wa miradi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato Jijini Dodoma kwa gharama ya Dola Mil. 271.63
▪Ujenzi wa barabara ya Bagamoyo-Horohoro -
Lungalunga-Malindi kwa kiwango cha lami (km 120.8) kwa gharama ya Dola Mil. 168.76
▪Na Dola Milioni 55.2 kwa ajili ya Programu ya utawala bora na kuendeleza Sekta Binafsi.
*Tunaweka bayana miradi hii ili kuonesha uwazi na utekelezaji, na kila Mtanzania ajue tunakopa na tutalipa kwa wakati*
Mmeniuliza msimamo wangu kuhusu malalamiko ya baadhi ya viongozi wa Chadema, wanasema kuwa wameonewa, niseme tu Mahakama imetimiza wajibu wake na siku zote sheria haziangalii chama, kabila wala dini ya mtu ndio maana zipo kesi Mbowe na wenzake walishashinda katika Mahakama hizo hizo, au waliposhinda hawakuwa Chadema siku wakishindwa ndio wanakuwa Chadema?
Zipo pia kesi wana CCM tena waandamizi wa ngazi ya Uwaziri waliwahi kufungwa tena bila kupewa mbadala wa kulipa faini, (Mmesahau ya Mramba na Yona?)
Mtu anayebeza uamuzi wa Mahakama hajui kanuni ya Mens Rea na Actus Reus katika masuala ya jinai na ana hoja dhaifu na yeye mwenyewe ni dhaifu katika mawazo.
Mwisho. Ninawapa pole waandishi wa habari Mkoani Morogoro waliopata majeraha kutokana na kulipukiwa na mitungi ya gesi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kuripoti ajali ya gesi jana, Serikali inaendelea na uchunguzi dhidi ya tukio hilo na tumefatilia, majeruhi wanapatiwa matibabu hospitalini na wanaendelea vizuri.
(Imeandaliwa na Idara ya Habari - MAELEZO)
Post a Comment