Dk Shein aongoza mazishi ya Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki yaliyofanyika leo Zanzibar!
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza mazishi ya Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki yaliyofanyika kijijini kwao Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, dini na serikali pamoja na wananchi, ndugu na jamaa walihudhuria katika mazishi hayo akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa, ambaye amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
Viongozi wengine waliohudhuria ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Brigedia Jenerali wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar Fadhil Omar Nondo, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mapema Alhaj Dk. Shein aliungana na viongozi wa dini, vyama vya siasa na Serikali, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika sala ya kumsalia Marehemu Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki katika Msikiti Mushawar, Mwembeshauri, Mjini Unguja sala iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kahbi.
Post a Comment