Ads

Dkt. Chamuriho ataka bajeti ya michezo ipewe kipaumbele!


Na Bahati Mollel, TAA



Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi) Dkt. Leonard Chamuriho amezitaka taasisi zilizopo chini ya Sekta hiyo kuhakikisha wanaweka bajeti ya michezo mbalimbali inayoshirikisha watumishi wake.

Dkt Chamuriho ametoa kauli hiyo leo kwenye bonanza la uzinduzi wa mazoezi ya kujiandaa na michezo ya kusherehesha sherehe za Mei Mosi lililofanyika kwenye viwanja vya Klabu ya Sigara Jijini Dar es Salaam.

Amesema pia michezo iwe moja ya agenda kwenye mabaraza ya Wafanyakazi kwa kuangalia changamoto na mafanikio yake na jinsi ya kuzitatua.

"Mazoezi yanamfanya mfanyakazi kuwa na afya njema na anaondokana na magonjwa nyemelezi, kama mlivyoona wote mmeshiriki kwa wingi hivyo muendelee hivi hivi ili msiwape shida makocha katika uteuzi wa kushiriki michezo mbalimbali," amesema Dkt. Chamuriho.

Hatahivyo amesema uteuzi wa wachezaji utafanyika kwa kuzingatia weledi, uwakilishi mkubwa katika mazoezi na bidii ya mchezaji husika na sio kwa njia nyingine yeyote.

Akizungumza changamoto za klabu hiyo zilizowasilishwa wizarani, amesema tayari wameanza kufanyia kazi hususan la kila taasisi kutoa mchango wa kuchangia klabu hiyo; kuruhusu wachezaji walioteuliwa kushiriki na kuwapa posho kwa wakati ili kuwaondolea msongo wa mawazo wawapo katika mshindano.



Pia amezitaka taasisi nyingine za Uchukuzi kuanza kujipanga kwa maandalizi ya mabonanza ili kuimarisha afya za watumishi kama walivyofanya TRC na TCAA.

Naye Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mbura Tenga amesema timu hiyo inaundwa na wachezaji kutoka taasisi 13 za Sekta ya Uchukuzi, ambapo imekuwa ni moja ya klabu 100 zinazounda Shirikisho la Shimiwi.

Tenga amesema klabu hiyo pamoja na kupata mafanikio makubwa kwa miaka miwili mfululizo ya kutwaa vikombe 13 mwaka 2018 na vikombe tisa mwaka 2019 vya michezo ya Mei Mosi, lakini inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa vifaa vya wachezaji na mahitaji ya klabu kwa ujumla.

"Wakuu wa taasisi hawaipi uzito hii klabu na kuona kama ni kikundi cha watu wachache, hili ni hapana ipo kwa mujibu wa kanuni na sheria za Baraza la Michezo nchini na tupo Shimiwi," amesisitiza Tenga.

Naye Makamu Mwenyekiti Ahmed Hassan amempongeza katibu mkuu Dkt. Chamuriho kwa ushiriki wake wa mara kwa mara kwenye mabonanza.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema sasa TRC ndio inafufua timu zake za michezo na watakuwa wakishiriki mara kwa mara.




(Picha zote zinaonesha Washindi wa michezo mbalimbali wakipokea tuzo kutoka kwa mgeni rasmi Dk Chamuriho).

Naye Rais wa klabu ya mbio fupi fupi ya Wasafi, Noordin Mshamu amesema klabu yake ipo tayari kushiriki kila bonanza watakaloalikwa.

Katika michezo mbalimbali iliyochezwa leo  mchezaji
Johari Mushi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ameng'ara kwa kuibuka mshindi katika mbio za kukimbia na gunia kwa wanawake, wakati kwa wanaume  kashinda Toba Malungula wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

Katika mchezo wa kufukuza kuku jogoo kwa wanaume Kashinda Julius Chezari wa TRC wakati kwa wanawake kashinda Carre Msofe wa Wasafi Jogging Club.

Timu ya wanawake ya kuvuta  kamba ya Uchukuzi imewashinda TRC kwa mvuto 1-0; kwa wanaume Uchukuzi wamewashinda TRC kwa mivuto 2-0; nao Wasafi waliwashinda TRC mvuto 1-0 katika mchezo wa pili wa kuvuta kamba wanaume.

Kwa upande wa soka timu ya TRC iliwashinda Uchukuzi mabao 2-1 yote yamefungwa na Joseph  Paul katika dakika ya 20 na dakika 30 na bao la Uchukuzi limefungwa na Ibrahim Issack katika dakika ya 35.

Katika mchezo mwingine timu ya Wasafi jogging walicheza na Ticts na kufungwa bao 1-0 lililofungwa na Henry Philemon katika dakika ya 10.

Huku katika netiboli Uchukuzi wametawazwa mabingwa kwa kuwatoa jasho TRC kwa kuwafunga alama 9-1. Hadi mapumziko Uchukuzi walikuwa mbele kwa alama 4-0.

Ticts waliwashinda TRC kwa penati 4-1 katika mchezo wa fainali ya mchezo wa soka baada ya kumaliza dakika za awali kwa kufungana bao 1-1.

Katika mchezo wa bao Mwalimu Ambakisye Mwasunga wa NIT aliibuka bingwa huku katika mchezo wa draft ameshinda Salum Mbonde wa TRC.


No comments