TAARIFA KWA WAINGIZAJI, WAZALISHAJI, WASAMBAZAJI, NA WAUZAJI WA BIDHAA ZA KUJIKINGA NA VIRUSI VYA KORONA
TAARIFA KWA UMMA
(Imetolewa chini ya kifungu cha 62(4) na 65(2)(g)vya
Sheria ya Ushindani ya Mwaka 2003)
Tume ya Ushindani (Tume), ni Taasisi ya Serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya
Ushindani (Namba 8 ya Mwaka 2003).
Tume imepewa dhamana ya kushajiisha na kulinda
ushindani na kuwalinda walaji dhidi ya mienendo isiyo ya haki na ya kupotosha katika
uchumi.
Baada ya Serikali kutangaza kuwa virusi vya Korona vimeingia nchini na kutolewa kwa
miongozo ya namna ya kujikinga na maambukizi, wananchi wamejitokeza kwa wingi
kununua bidhaa za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo. Hata hivyo, Tume
imepokea malalamiko juu ya uhaba na kuongezeka kwa kasi kwa bei za bidhaa hizo.
Bidhaa zinazolalamikiwa ni pamoja na:
1. Dawa za kutakasa mikono na maeneo yanayoweza kuguswa kwa mikono (Hand
Sanitizers and Surface Disinfectants);
2. Barakoa (face masks); na
3. Vizuizi vya mikono (gloves);
Tume imefanya uchunguzi wa awali na kubaini uhaba wa bidhaa za kujikinga na
maambukizi ya virusi vya Korona na kwamba maduka kadhaa yamekuwa yakiuza bidhaa
hizo kwa bei za juu ilikinganishwa na bei zilizokuwepo kabla ya tangazo la virusi hivyo
kuingia nchini.
Mwenendo huu wa soko unaashiria ukiukwaji wa Sheria ya Ushindani,
hususan:
i. Kupanga bei baina ya washindani;
ii. Kuficha, kupunguza, au kukataa kusambaza sokoni bidhaa kwa lengo la
kupandisha bei na kujipatia faida kubwa isivyo halali;
iii. Vitendo hadaifu dhidi ya walaji wa bidhaa kuhusiana na uhalisia na usahihi wa aina
ya bidhaa.
Tume inatoa ONYO kwa waingizaji, wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa jumla na
rejareja wa bidhaa husika kuwa ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani kujihusisha
na vitendo vilivyolalamikiwa hapo juu na inawataka kuacha vitendo hivyo mara moja.
Aidha, Tume inawakumbusha Walaji kuwa makini katika kununua bidhaa hizo, ikiwa ni
pamoja na
(i) kukagua bidhaa na kujiridhisha kabla ya kuzinunua na
(ii) kudai na kutunza
risiti za manunuzi.
Wananchi wenye taarifa kuhusiana na uwepo wa vitendo hivyo sokoni, wawasiliane na
Tume kwa:
1. Simu ya bure Namba 0800110094
2. Barua Pepe yenye anuani ya info@competition.or.tz
Tume inaendelea kuwasisitizia wananchi wote kuzingatia miongozo inayotolewa na
Serikali kuhusiana na kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona.
Imetolewa na
Mkurugenzi Mkuu
TUME YA USHINDANI
Machi 19, 2020
Post a Comment