Ads

UMATI MKUBWA WAJITOKEZA JIJINI DAR KATIKA MAZISHI YA MWANDISHI MWANDAMIZI WA HABARI ZA MICHEZO NCHINI ASHA MUHAJI 








Na Mwandishi Maalum- Dar es Salaam

UMATI MKUBWA wa waombolezaji wakiwemo waandishi wa habari wa kada mbalimbali na wanamichezo wamejitokeza kwa wingi katika mazishi ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari  za Michezo Mahiri Asha Muhaji(50) ambaye amezikwa katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu  jijini Dar es Salaam jana jioni.

Katika mazishi ya marehemu Asha ,viongozi wa vilabu mbalimbali na wadau wa soka wameeleza kuwa kifo chake kimeacha pengo kubwa kubwa katika tasnia ya Michezo na sekta ya habari hasa za Michezo kwani enzi za uhai wake Asha alikuwa Mwandishi Habari wa Michezo mwenye kipaji  na alikuwa mfano kwa wengine.

Kabla ya mwili wake kupelekwa kwenye makaburi hayo kwa ajili ya mazishi , ulipelekwa nyumbani kwao Kijitonyama, Mtaa wa Mabatini jijini  Dar es Salaam ambako msiba wake umewekwa.

Baadhi ya waombolezaji waliohudhuria msiba wa Asha Muhaji na kutoa Salaam zao ni pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Wallace Karia na Katibu wake, Wilfred Kidau, Msemaji wa Simba SC, Haji Manara, Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire,  wachezaji na wadau mbalimbali.

Akitoa Salaam zake msibani hapo Rais wa TFF Karia amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Asha Muhaji na kwamba enzi za uhai wake ametoa mchango mkubwa kwa TFF katika kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua katika soka huku akieleza namna ambavyo alijitoa kwa timu ya Taifa ya Tanzania ' Taifa Stars'

"Tumepoteza mtu kwenye michezo, ila rai yetu tunayo nafasi ya kuendeleza yale mema ambayo ameyafanya kwa maendeleo ya soka letu". Alisisitiza Karia.

Wakati huo huo Kocha Msaidizi wa Klabu ya Simba na Mwalimu wa Soka nchini Suleiman  Matola amesema ni pigo kubwa na kwamba yeye amebahatika kufanya naye kazi kwa nyakati tofauti hasa kwa kuzingatia kuna wakati alikuwa naye  Simba akiwa Mwalimu na Asha Muhaji akiwa msemaji wa Klabu hiyo.

 Msemaji wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema binafsi anamfahamu uwezo mkubwa aliokuwa nao Asha Muhaji za uhai wake katika eneo la uandishi wa habari za michezo na kwamba mchango wake katika kuhakikisha eneo la michezo linasonga mbele nchini Tanzania hautasahaulika huku akieleza kuwa Asha alikuwa ni Mwandishi ambaye muda wowote aliohitajika kufanya kazi yake alikuwa tayari na sio   miongoni mwa waandishi ambao wamekuwa na kasumba ya kuomba fedha kwa watoa taarifa.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau,  kwa upande wake ameeleza namna ambavyo alikuwa akipata ushirikiano wa  kutosha kutoka kwa Asha Muhaji za uhai wake na kwamba ni moja ya waandishi wa habari za Michezo ambaye amejitoa kwa sehemu kubwa  kufanikisha timu ya taifa inafanya vema katika medani ya soka.

Mdau mwingine wa michezo nchini kutoka Jeshi la Wananchi  wa Tanzania( JWTZ) Luteni Suleiman Semunyu amesema  kuwa Asha Muhaji enzi za uhai wake alihakikisha anatumia taaluma yake ya uandishi wa habari za Michezo kuandika habari za aina mbalimbali za michezo Michezo ikiwemo ile ambayo haina umaarufu mkubwa.

Amesema kuwa Asha Muhaji enzi za uhai wake hakuwa akiandika habari za mpira wa miguu bali alihakikisha wanaandika na habari za Michezo mingine kama Gofu na tenisi." Ametangulia mbele za haki lakini ukweli mchango wake katika medani ya michezo tutaendelea kuukumbuka.Kwetu sisi kila tulipomuhitaji alikuja na pale aliposhindwa alikuwa anatuletea Mwandishi mwingine.Aliaminiwa kwenye kupika waandishi mahiri wa habari za Michezo."










Mwili wa aliyekuwa Msemaji wa Simba SC na Mwandishi mahiri wa habari za Michezo nchini,Asha Muhaji ukihifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele,Katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu, jijini Dar es Salaam jioni jana.








Jeneza lenye Mwili wa Marehemu Asha Muhaji ukisaliwa nyumbani kwao  Kijitonyama,Jijini Dar kabla ya kumuhifadhi kwenye nyumba yake Milele jana jioni katika Makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu jijini Dar es Salaam.

















Baadhi ya Waumini mbalimbali wakishiriki mazishi ya aliyekuwa Msemaji wa Simba SC na Mwandishi Habari Mahiri za Michezo nchini,Asha Muhaji














 Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa msemaji wa Simba SC na Mwandishi Mahiri wa Habari za Michezo nchini,Marehemu Asha Muhaji likipakiwa kwenye gari la ambulance tayari kuelekea kumhifadhi kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu, jijini Dar es Salaam











  Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Msemaji wa Simba SC na Mwandishi Mahiri wa Habari za Michezo nchini,Marehemu Asha Muhaji ukipelekwa kwenye gari maalum tayari kuelekea kumhifadhi katika nyumba yake ya milele katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu, jijini Dar es Salaam jana jioni.











 Mwakilishi wa Mashabiki wa timu ya Yanga SC,Ndugu Kaligo akitoa salamu za pole  nyumbani kwa familia ya Marehemu jioni jana  kabla ya Maziko kufanyika, kwa Familia,Wafiwa wote Ikiwemo timu ya Simba SC na mashabiki wake kwa kuondokewa na Mpendwa wao Asha Muhaji ambaye alifariki juzi katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam .











 Ndugu,Jamaa na Marafiki wakisikiliza salamu za pole zilizokuwa zikitolewa kutoka kwa wawakilishi mbalimbali kufuatia kufariki kwa Marehemu Asha Muhaji,aliyekuwa Msemaji wa timu ya Simba SC na Mwandishi Mahiri wa Habari za Michezo nchini











 Mmoja wa Wakilishi wa habari za Michezo, Mohamed Mharizo akitoa salamu za pole kwa niaba ya Waandishi wa Habari za Michezo na wengine kwa ujumla











 Rais wa TFF Wallace Karia (wa pili kulia) pamoja na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau (wa kwanza kulia) wakijadiliana jambo na baadhi ya Wadau wa Michezo,walipofika kutoka salamu za polenyumbani kwa familia ya Marehemu Asha Muhaji,ambaye amezikwa jana makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu, jijini Dar es Salaam











 Wadau wa Michezo wakijadiliana jambo walipofika nyumbani kwa familia ya Marehemu Asha Muhaji kushiriki shughuli za mazishi na maziko katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu jijini Dar es Salaam jana jioni.










Ndugu, jamaa na Marafiki wakiwa wamekusanyika nyumbani kwao marehemu Asha Muhaji wakiomboleza jioni jana kabla ya Maziko kufanyika.











Msemaji na Mhamasishaji kipenzi  wa Simba SC Haji Manara akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Uongozi wa Timu hiyo pamoja na Wapenzi wa Klabu hiyo nyumbani kwa Marehemu jioni jana kabla ya maziko kufanyika katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu , Jijini Dar es Salaam
jana jioni.














Wadau mbalimbali wakishiriki ibada ya mazishi nyumbani kwao Marehemu Asha Muhaji, maeneo ya Kijitonyama, Jijini Dar es Salaam jana.
Marehemu amezikwa jana jioni katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu Jijini Dar es Salaam.



Picha na Michuzi JR-Michuzi Media.


No comments