TANZANIA NI MFANO KATIKA STRATEJIA ZA UDHIBITI WA COVID-19 BARANI AFRIKA .
Rais John Magufuli akihutubia wananchi waliohuhuria Ibada katika Kanisa la Paulo wa Msalaba jijini Dodoma, Machi 22, 2020.
Na Midladjy Maez - Dar es Salaam
Kihistoria Tanzania kati ya miaka ya 1960 hadi 1994 imejulikana sana barani Afrika na Dunia kote kuwa ni nchi iliyojitolea kwa hali na mali kusaidia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika zikiwemo Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na hatimaye Afrika ya Kusini. Japokuwa uwezo wa kiuchumi ulikuwa mdogo sana wa Tanzania UKEREKETWA wa BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS NYERERE KATIKA KUFANIKISHA JAMBO LETU HILO ulifunika mapungufu yote ya mapambano makali yaliyojiri katika hatua zote za ukombozi Kusini mwa Afrika.
Kuthibitisha hilo Kamati Maalum ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi za Afrika wakati huo OAU sasa ni AU iliweka makao makuu yake jijini Dar es Salaam chini ya uongozi wa Hayati Brigedia Jenerali Hashim Mbita.
Mchango wa Tanzania wa hali na mali ulikuwa wa kistratejia zaidi na uwezo wake wa kuwasilisha ajenda ya ukombozi kwa nchi zilizo nje ya bara la Afrika yakiwemo mataifa ya Umoja wa Usovieti (USSR) sasa ni Urusi(Russia), Jamhuri ya Watu wa China. Nchi kama Algeria na Ethiopia zilishiriki kikamilifu kutoa mafunzo kwa Wapiganaji Uhuru wa nchi mbalimbali zilizoainishwa awali.Tanzania yenyewe ilikuwa na kambi kadhaa ambapo wapiganaji kutoka vyama vya ukombozi mathalan, Frelimo, Swapo, ANC, PAC,MPLA,Molinaco(Comoro) walijifunza mbinu za medani. Kuundwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC ilikuwa kama hitimisho la kutoka awamu moja ya mapambano ya kugombea uhuru wa kisiasa na kuingia awamu ya pili ya mapambano ya ukombozi wa kiuchumi.
Hiyo ni dibaji sasa kuna mapambano yanaendelea duniani kote. Ukweli kwamba kuanzia Machi , 2020 dunia imekumbwa na taharuki ya ugonjwa wa korona unaonezwa na virusi vya Covid-19 ulioanzia nchini China mwishoni mwa mwaka 2019 na kusambaa duniani kwa kasi kubwa ya ajabu.
Vyombo vya habari vya kimataifa vinapongezwa kwa kufikisha taarifa hizi kwa nchi zote kwa wakati ili kila nchi ichukue hatua za kuwalinda raia wake kama inavyopaswa. Lakini baadae hivi vyombo kwa maoni ya wengine vimetumika kupandisha joto la hofu hasa kwa wahanga wa Covid-19 na jamaa zao. Kwani taarifa zilikuwa zikitolewa mfululizo siku nzima saa 24 zikiripoti kusambaa kwa korona bila ya dalili za kudhibitiwa.
Halikadhalika kulianza malumbano kila taarifa mpya ikichomoza kutoa matumaini kuwa sio muda mrefu ugonjwa wa homa kali ya mapafu UTADHIBITIWA! Ilikuwa ukitoa taarifa ya matumani ni kama umetenda dhambi lakini ukikuza taarifa za hofu unaungwa mkono na hiyo habari itapewa kipa umbele kwa vyombo vyote vikubwa duniani.
Rais Magufuli akiteta jambo na Mwananchi mmojawapo ndani ya Kanisa la Paulo wa Msalaba jijini Dodoma Machi 22, 2020.
Maoni mengine yanaainisha huenda vyombo vikubwa vya habari vimechangia kuongeza wahanga wa korona kwa kukuza HOFU ambayo kisayansi inatajwa kuwa kisababishi cha kushusha kinga za binadamu mwilini.
Hapa Tanzania Rais John Magufuli akihutubia kwa mara ya kwanza hadharani katika Kanisa la Paulo wa Msalaba jijini Dodoma Machi 22, 2020 kuhusu athari za ugonjwa wa korona aliwataka Watanzania wasiwe na hofu wachape kazi na kuzingatia masharti ya kujikinga yaliyoainishwa na Wataalam wa Afya.
Aidha alisisitiza kwa Watanzania kumtanguliza Mungu kwa kufanya Ibada na hatimaye hili janga litakwisha tu kama majanga mengine ya kijamii.
Waziri Ummy Mwalimu mwenye dhamana ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yuko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona nchini.
Baada ya hapo kilichotokea ni historia ikiwemo mazoezi ya kujifukiza kwa nyungu, dawa ya Nimr kufikia Juni mwaka huu Tanzania ilerejea katika maisha yake ya kawaida japo tahadhari zipo palepale. Vyuo na shule vimefunguliwa, michezo imerejea na maisha mengine pamoja na sherehe za harusi.
Ibada zimeshamiri zaidi kwani hata wakati taasisi nyingine za kijamii zilipofungwa nyumba za ibada hazikufungwa ziliruhusiwa kuendelea na huduma zake za kiroho kwa masharti ya kuzingatia kujikinga na maambukizi ya Covid-19 yalivyoanishwa na Wataalamu wa Afya nchini.
Baada ya Tanzania kuchukua hatua ya kufungulia shughuli zote za kijamii zikiwemo kumbi za starehe kama nchi ilijikuta katika daraja la kutokuwa MFANO MZURI kwa wakubwa hasa makampuni yanayozalisha madawa na yale yanayotarajia kuuza chanjo, hivyo basi
Shirika la Afya Duniani-WHO na wengine wanaiona TANZANIA kama mwana mpotevu.
Waziri Selemani Jafo wa TAMISEMI amepata umaarufu kwa kuhamasisha matibabu ya asili yakiwemo mafukizo ya Nyungu dhidi ya COVID-19.
Naam hayo mengine tuwaachie wakubwa lakini kulikoni majirani zetu kitu gani kinawazuia kuja kuona hali halisi wakachukua katika uzoefu wetu kile kitakacho wasaidia wanamuogopa nani au wanaogopa kuitwa WANAWAPOTEVU?
Vyombo vya habari vya kimataifa vinahusika na kuongeza taharuki na hutangaza kwa unyonge taarifa za kupungua maambukizi. Inaelekea taarifa hizo hawazipendi ni sawa na enzi za ukombozi wapigania uhuru waliitwa Magaidi na wa upande wa pili Wapenda Demokrasia.
Kinachoshangaza hiyo demokrasia mbona haiachiwi kusaidia mapambano dhidi ya Covid-19.
Je vyombo habari hasa vya kimataifa vina ajenda kuwa taharuki lazima iendelee ili chanjo ikipatikana kuwepo wateja tena wa kutosha ?
Taarifa zozote za kupungua waathirika wa korona ni habari hasi.Ndio maana wanasita kuleta Waandishi wao wa Habari maalum nchini Tanzania kufanya uchunguzi. Wana hofu kuwa watakachokiona hatimaye KITAPASUA PUTO LA HOFU LA KIMATAIFA WANALOLIJAZA HEWA KILA USIKU UCHAO!
Stratejia aliyoitumia JPM kwa maoni ya wengi zitasaidia sana nchi zinazofanana na sisi kimazingira na kijamii Barani Afrika, hata hivyo dhana ya kuogopa kuitwa ‘Mwanampotevu IMETAMALAKI’.
Ikumbukwe baadhi ya viongozi wa siasa na Waandishi Habari nchini walidiriki kumkejeli Rais Magufuli na kusema kama kweli Mungu au Imani imeisaidia Tanzania katika kuidhibiti korona basi wafaidika wa kwanza wangekuwa Wataliano kwa vile ndiko yaliko Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani. Hii ilikuwa kejeli ya daraja la kwanza. Lakini kuna sababu za msingi sisi tulitumia taaluma ya tiba za asili na kumuomba Mungu dhidi ya korona na mazingira ya hali ya hewa ya joto kwa jumla ni tofauti na Ulaya yenye mazingira tofauti ya hali ya hewa yenye baridi kali. Tunaamini kile ambacho kimewezekana Tanzania, kinawezekana kwa kila nchi kulingana na mazingira yake.
Mahudhurio makubwa kupita kiasi aka 'nyomi' ya Wapenzi wa Vilabu vikubwa vya kandanda nchini vya Simba na Yanga katika Uwanja wa Michezo wa Benjamin Mkapa wakati wa maadhimisho ya matamasha yao hivi karibuni ni ushahidi tosha kuwa Watanzania hawana tena hofu ya maambukizi ya COVID-19.
Hata hivyo tunaamini nchi za Afrika zinaweza kupata faraja ya haraka sana kama watakuja kujifunza uzoefu wetu. Sawa na Wapigania Uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Afrika walivyotiririka miaka ya 60 nchini kujifunza mbinu za vita vya ukombozi.
Wakati wapenda amani na ustawi wa jamii wa hapa nchini na duniani kote kimya kimya wakimpa Kongole Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa mafanikio aliyoyapata katika mapambano dhidi ya gonjwa la Korona nchini na kulidhibiti tahadhari lazima iendelee TUSIBWETEKE.
Watalii wana miminika kufurahia utajiri wa kipekee wa mali asili za mbuga zetu za daraja la juu duniani, lakini miongoni mwa Watalii ni wachunguzi na MA-THOMASO wanataka kuhakikisha hizo kelele za hospitali kuelemewa na waathirika wa Covid-19 nchini ni kweli?
Kuna wasiwasi wa kuhujumiwa kiaina hivyo basi Watanzania wote na hasa Wataalamu wa Afya wawe makini ili dunia ya kimataifa yenye ajenda HASI wasije kutupandikizia VILIPUZI VYA COVID-19 NCHINI KIRAHISI! Hili linatuhusu sote , taasisi, viongozi, mtu binafsi na kila mzalendo. SHIME: ‘INAWEZEKANA TIMIZA WAJIBU WAKO’.
Post a Comment