Ads

WAKATAENI MABEBERU NA MAWAKALA WAO-DKT HASSAN ABBASI


Na Mwandishi  Maalum

Dkt Hassan Abbasi

MAMBO 10 ALIYOYASEMA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI , DKT. HASSAN ABBASI KATIKA MAHOJIANO NA TIMES FM JANA SEPTEMBA 23, 2020:

1. Wakati wanasiasa wakiendelea na kampeni za uchaguzi, Serikali bado ipo na kazi mbalimbali zinaendelea kama ilivyopangwa, sheria za nchi zipo na wasemaji wa nchi wapo; ukitugusa na uongo wako tutakujibu;

2. Miradi mbalimbali mikubwa na midogo inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania inaendelea vyema na tutaendelea kutoa takwimu za kila mara kuhusu utekelezaji;

3. Kuhusu faida za ndege hili tumeshalieleza sana kwamba ndege ni ajira hivyo zimeshaingiza zaidi ya ajira 400 za moja kwa moja; ndege ni mapato hivyo zimeshaongeza mapato ya Shirika na Serikali kutoka Bilioni 2.5 kwa mwezi hadi Bilioni 15 kwa mwezi na kodi zaidi zinalipwa zinazokwenda kuhudumia wananchi;



4.Kuhusu madai kwamba ndege zilinunuliwa bila uwazi wala bajeti yake haijulikani Dkt. Abbasi alihoji wanaotoa madai hayo kama wanaishi Tanzania au vipi! Alisema ununuzi ulikuwa kwa mujibu wa kifungu kipya cha 65A cha Sheria ya Ununuzi wa Umma (marekebisho ya 2016) ambayo inaruhusu, kwa nia ya kupata bei bora na thamani ya fedha, taasisi ya ununuzi kununua moja kwa moja kutoka kwa mtengenezaji wa bidhaa husika badala ya mawakala wanaopandisha bei;
5. "Kama kuna mtu alikuwa na wakala wake mfukoni katika ununuzi wa hizi ndege imekula kwao, Serikali imenunua moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wanaojulikana Kimataifa kama Boeing na Bombardia na sheria inaruhusu hivyo na ilipata bei ya chini kuliko hata zile zilizoainishwa kwenye tovuti zao," alisema.

6. Kwamba ndege hizi haijulikani zinanunuliwa kwa fedha kutoka wapi, Dkt. Abbasi alisema Watanzania waendelee kuwakataa wanaotoa hoja hizo dhaifu kwa kuwa ni matapeli wasiojua lolote linaloendelea nchini;
7. Akimwaga ushahidi wa bajeti za mwaka 2016/17, 2017/18 na 2019/20 kutoka Fungu 2006 na mradi namba 4294 (Acquisition of New Aircrafts-ATCL), Dkt Abbasi alisema kwa miaka takribani minne mfululizo Serikali imekuwa ikitenga wastani wa TZS Bilioni 500 kwa mwaka na zinajadiliwa na zinapitishwa na Bunge kupitia fungu hilo, akashangaa wanaodai kuwa fedha za ndege hazijulikani zinatoka wapi kama ni watu wanaoishi Tanzania au ndio wamekuja nchini juzi kushangaa maendeleo yetu!;


Rais Dkt John Magufuli akizungumza baada ya ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa SGR.

8. Aliulizwa hoja kama hiyo kuhusu usiri katika ujenzi wa reli ya SGR na Mradi wa Umeme Rufiji na fedha zinakotoka Dkt. Abbasi akaainisha vipande vyote vya ujenzi wa reli na Mradi wa Umeme kuwa vilishindanisha wataalamu wa ndani na nje. Akatoa mfano mradi wa SGR Dar kwenda Moro walijitokeza washindani zaidi ya 40, Moro kwenda Makutupora walijitokeza washindani takribani 36 na sasa akawaalika "wenye watu wao" waache kupiga kelele bali wawalete washiriki Zabuni iliyotangazwa Agosti mwaka huu ya ujenzi wa SGR kwa kipande cha Mwanza-Isaka. Kuhusu mradi wa Umeme Rufiji alisema zabuni ilitangazwa wazi na takribani makampuni manne yalishiriki kutoka mataifa ya Afrika, Ulaya na Asia;


Rais Dkt John Magufuli akikagua mradi wa SGR kwa kutumia treni maalum hivi karibuni katika kipande cha reli ambao ujenzi wake umekamilika kati ya Dar es Salaam na Morogoro.

MICHORO YA MUONEKANO WA  MRADI WA JNHPP MARA UJENZI WAKE UTAKAPOKAMILIKA MNAMO MWAKA 2022.


Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani akifafanua jambo mbele ya Waandishi Habari kuhusu mradi wa JNHPP hivi karibuni.

9. Aidha, Dokta Abbasi alizidi kusisitiza kuwa fedha zote za miradi hii zipo kwenye bajeti na zinapitishwa na Bunge kila mwaka huku akitaja mradi wa Rufiji kuwa mpaka sasa TZS Trilioni 1.432 zimeshatolewa; "Kuna wageni wengi nchini kwa sasa kwa hiyo tuwavumilie, mtu anahoji hela za SGR hazijulikani zinatoka wapi, nataka tuamini yeye ndio hajulikani ametoka wapi na anataka nini, anayehoji hii akasome fungu 2005, mradi namba 4281 kwenye Sekta ya Uchukuzi aone kila mwaka Bunge liliidhinisha sh. ngapi kwa miradi ya SGR kuanzia mwaka 2017/18," alisema na kuwataka Watanzania kuwapuuza waropokaji wanaoumizwa na maendeleo yanayotokea. 10. Akasisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekeleza mambo makubwa yenye mwangwi mkubwa katika kuwanufaisha Watanzania na kuwataka Wananchi kuendelea kutimiza wajibu wao na kuwakataa mabeberu na mawakala wao. Akaulizwa beberu ni nani? Akajibu: "Beberu hana rangi wala utaifa, beberu ni mtu, taasisi au taifa lolote ambalo tukiwa hatuna hospitali, barabara, madaraja, ndege na vingine muhimu kwa maendeleo wanatubeza; tukianza kuvijenga na kuvifanyia kazi wananuna na kujaribu kuhujumu na kuvibeza bila hoja; mtu wa namna hii awe Mtanzania au si Mtanzania ni beberu tu," alisema.


No comments