Ads

WANANCHI WALIOTAPELIWA ARUMERU WAANZA KUTABASAMU


Na Mwandishi Maalum- Arumeru


Nd Jerry Muro Mkuu wa Wilaya ya Arumeru akipokea  TZS 21,700,000/=  kutoka kwa Nd Deo Mtui ambaye ni Mkuu wa TAKUKURU Wilayani Arumeru  ambazo Taasisi  imeziokoa kutoka kwa matapeli.

Ofisi ya Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo Septemba 25  2020 imekabidhi Jumla ya TZS 21,700,000/= kwa Wananchi 7 Wilayani Arumeru.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Nd Deo Mtui ambaye ni Mkuu wa TAKUKURU Wilayani Arumeru , amesema kiasi cha TZS 21,700,000/= zimekabidhiwa kwa Wananchi 7, ambapo kiasi cha TZS 7,500,000 kimekabidhiwa kwa Waalimu 6 wa Shule ya Sekondari Mariado Mwl.Abdallah Marambo, Mwl.Ezekiel Mwaipopo, Mwl.Andrew Mike, Mwl.Samson Hamza, Mwl.Christina Lekashu na Mwl.Ellen A. Lomau ikiwa ni mishahara yao ambayo hawakulipwa na mwajiri.

Halikadhalika kiasi cha TZS 14,000,000/= kimekabidhiwa kwa Emmnuele Vumilia Kilembe(pichani) ambaye alidhulumiwa katika mauzo ya gari lake kinyume na mkataba wa mauziano. Aidha Mtui ametoa Wito kwa wananchi kuendelea kuiamini TAKUKURU na endapo wanamalalamiko ambayo wanasadiki ni malalamiko ya kweli, wasisite kufika TAKUKURU na kama ilivyo Ada, TAKUKURU itayafanyia kazi na kuhakikisha wanapata haki yao.

Baadhi ya Walimu pichani wakipokea fedha zao zilizo okolewa na Takukuru wilayani Arumeru


Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo Nd Jerry Muro amesema Serikali haitamfumbia macho yeyote anayewadhulumu Wananchi ambapo amemwagiza Mkuu wa TAKUKURU Wilaya hiyo kumkamata mtu mmoja ndani ya masaa 48 anayedaiwa kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi kwa kuuza ardhi kwa mtu zaidi ya mmoja. Nd Muro amewaonya wanaofanya biashara ya mikopo kinyume na taratibu kwani wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi kwa mikopo yenye riba kandamizi sambamba na kuchukua vitambulisho vya taifa vya wananchi hao. " Ni muhimu kusajili biashara ili iwe halali na kufanyika kwa kuzingatia taratibu". Amesisitiza Mkuu wa Wilaya .

Wananchi waliopata haki kwa kukabidhiwa fedha zao wameishukuru Serikali kutetea haki za wanyonge ambapo Mwl. Abdallah Malambo ameushukuru uongozi wa Wilaya na kukiri kunufaika na sera ya Mhe.Rais Dkt.John Pombe Magufulu kujali wanyonge . Emanuel G. Kilembe ambaye amekabidhiwa TZS 14,000,000/= kama mauzo ya Gari lake amesema amefarijika sana na utendaji wa Awamu ya Tano kwani Kauli mbiu: 'HAPA KAZI TU: inatekelezwa.





















No comments