WASOMI WAELEZWA FURSA ZA KIUCHUMI ZILIZOBUNIWA NA AWAMU YA TANO
Na Mwandishi Maalum-Arumeru
Mkuu wa Wilaya wa Arumeru Jerry Muro
Wasomi wapatao 142 kutoka vyuo mbalimbali mkoani Arusha wamepata fursa ya kufahamu fursa mbali mbali zilizobuniwa na Serikali ya awamu ya Tano tokea iingie madarakani Novemba 05, 2015 hadi sasa.
Akizungumza na Wasomi hao leo Septemba 17, 2020 wanaohudhuria programu maalum ya mafunzo katika Chuo cha Maendeleo cha MS TCDC kilichopo Usa River, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe Jerry Muro amewafafanulia fursa mbali mbali ambazo Serikali yao imezitengeneza kupitia kuanzisha miradi mikubwa ya kihistoria.
Baadhi ya miradi hiyo ni ule wa Ujenzi wa Bwawa la Ufuaji Umeme la Julius Nyerere katika Mto wa Rufiji(JNHPP) unaotarajiwa kuzalisha megawati 2115. Miradi mingine iliyozalisha fursa za ajira ni Ujenzi wa Reli ya Kisasa -SGR ambayo katika kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ujenzi wake unakaribia kukamilika. Reli ya SGR katika awamu zake 5 za ujenzi utafika hadi Mwanza na kumwaga ajira nyingi(Dar-Morogoro, Morogoro-Makotopora, Makotopora-Tabora, Tabora-Isaka na Isaka-Mwanza).
Mkuu wa Wilaya aidha aliainisha pia mpango wa ajira milioni nane ambao Serikali ya CCM chini ya Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli imepanga kuzitoa itakapopewa dhamana ya kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020. Wasomi hao waliopata fursa ya kuzungumza na Mhe Muro ni Wanafunzi kutoka Vyuo vya Makumira, Arusha University, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru na Chuo cha Mifugo Lita-Tengeru.
Post a Comment