UNENE NI JAMBAZI LINALOIBA TAKRIBAN KILA KITU UTULIVU , KUJIAMINI NA...
MADA YA LEO : UNENE NI JAMBAZI LINALOIBA TAKRIBAN KILA KITU UTULIVU , KUJIAMINI NA...
Hii mada ya unene ni jambazi nilikuwa niandike siku nyingi kutokana na uzoefu binafsi karibu miaka 20 iliyopita!
Nilikuwa nanenepa pole pole na kugundua kila mwaka naongezeka kidogo kidogo. Mwaka 1994 sababu mojawapo ya kuondolewa kusoma habari ITV ni unene!
Hata hivyo miaka 20 baadae nikiwa Reli wakati fulani kama TRC na sasa TRL nimeongezeka wastani mara mbili zaidi.
Kusifiwa kama 'Pepe Kalle' au 'Mutu ya Nguvu'....'Mutu ya Kilo'....hizi sifa za kipuuzi ndio sababu mojawapo sikutanabahi mapema kuwa naunda mfumo wa kijambazi ambao mwilini mwangu ambao hatimaye utafanikiwa kuiba kila kitu ikiwemo 'Furaha', kujiamini, utulivu na uwezo wa kuyafanya yale ambayo miaka 20 iliyopita niliyamudu kujifanyia au kuwafanyia wale ambao ni lazima niwafanyie kwa hiyari au kwa kuwajibika..!
Sasa baada ya kujiridhisha kuwa unene ni adui mbaya ambaye anakuja kwa ghilba kuwa naongeza wajihi na kuonekana mtu mwenye uwezo mkubwa! Adui ni adui tu awe ana sura nzuri au mbaya awe, ndugu yako kipenzi au rafiki yako wa kufa na kuzikana ni kumuepuka na ikiwezekana ni kummaliza!
Lazima niseme kweli kuwa kipindi kilichonitanabaisha na kunijaalia afueni ni cha Madame Rita Show Azam Two nilifungua kama ajali nikamuona Dada mmoja anathibitisha kuwa kuna mchanganyiko wa juisi ambayo inaingizwa vikorokoro vyote vya mboga, protini nakadhalika Ukinywa hicho kitu basi ndio mlo wako baadae unaiongezea na kipande cha protini na saladi mchana na pia jioni hivyo hivyo. Nikaamua kujaribu hiyo 'regime' kweli baada ya wiki zile sehemu za mwili zilikuwa taabu sana kuzifikia kwa urahisi nikaaanza kuzifikia. Nilifurahi sana na nikaanza kujiamini tena na kutokuwa na wasiwasi. Sijapungua sana lakini kiboko cha unene uliopoitiliza ni hili mug ambalo 'my wife' ananitayarishia kila asubuhi kwa kutumia 'blender'! Ili nipungue sana inabidi kufanya mazoezi ya viungo licha ya kuwa kila siku nikiwa Dar huwa nafatiki ya kukwea ghorofa 3 kwa vile fleti yangu iko ghorofa ya 3 pale maghorofa ya Reli katikati ya Mitaa ya Ghana, Ohio , Garden na Mirambo! Kumbe juice ya karanga, mbogamboga, i na vitunguu swaumu ni kiboko cha jambazi Unene! Mchanganyiko wenyewe ni: Karot moja, karanga kidogo, kitunguu maji nusu, kitunguu swaumu chembe nne, mchicha vijiti vitatu au matembele majani manne, green cauliflower kubwa nusu kama dogo zima vyote unaweka katika blender unapata kinywaji cha mug moja! Unakunywa polepole...mchana salad na kipande cha kuku...jioni hivyo hivyo salad na kipande cha samaki au kuku! Kuna kahawa unakunywa ukisikia njaa..ambayo huongezi sukari...baada ya siku 10 utaona mabadiliko mafuta yataanza kuyeyuka mwilini na kutumika kuupa mwili nguvu..na ukifanya mazoezi kasi itaongezeka! Karibu..!
Sitaki tena kuitwa Mutu ya kilo wala Pepe Kalle! UNENE NI JAMBAZI APIGWE VITA KILA FURSA IKIPATIKANA! WAKATABAHU! Midladjy Maez wa Reli
Post a Comment