Miaka 70 Na Miujiza Ya Wachina..
Miaka 70 Na Miujiza Ya Wachina..
Leo, Oktoba Mosi ni siku kubwa kwa Jamhuri ya Watu Wa China.
Ni China iliyoanza kama taifa masikini mno na kuja kuwa taifa la pili kwenye uchumi wa dunia. Hii ni miujiza ya Wachina.
Na kwetu Watanzania Wachina ni marafiki zetu wa kweli.
Tanzania na China zimekuwa na uhusiano wa kirafiki wa miaka mingi.
Inaweza kusemwa, kuwa China na Tanzania, zina historia ya kusimama upande mmoja wa mapambano. Si ajabu, kwa kusaidiwa na Tanzania kuingia kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa enzi zile Dr. Salim Ahmed Salim na Tanzania ilipokuwa Rais wa Baraza, China hapa juzi tu imemtunuku Dr. Salim Ahmed Salim nishani ya juu ya heshima. Ni heshima tuliyopewa Watanzania wote.
Itakumbukwa, kuwa China nayo imetusaidia katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuimarisha miundo mbinu yetu. Mradi wa ujenzi wa reli ya TAZARA ni mfano mmoja kati ya mingi.
Naam. Wakati umebadilika, nasi tubadilike. Tushirikiane na marafiki zetu waliopiga hatua zaidi. Na katika ushirikiano wetu wa sasa na China tuna lazima ya kuiangalia China kwa miwani mingine.
Ndio, China ya jana ilikuwa ni tishio la kitikadi zaidi kwa Marekani na nchi nyingine za kibepari. Lakini China ya leo ni tishio kubwa la kiuchumi.
Leo China inashindana na mataifa makubwa katika uzalishaji wa bidhaa za viwanda. Inashindana na nchi nyingine kubwa kiviwanda katika kuuza
bdhaa zake kwenye soko la dunia. China ya leo inahitaji malighafi
zaidi kwa viwanda vyake, inahitaji mafuta pia. Marekani nq nchi nyingine za viwanda hali ni hiyo hiyo. Kwa vyovyote vile, mafuta
yanayozalishwa sasa duniani hayatatosha kukidhi mahitaji ya viwandani.
China , Marekani na nchi nyingine za viwanda haziwezi kutegemea mafuta kutoka Mashariki ya Kati pekee.
China ya leo imeendelea sana kiteknolojia. Inazalisha kwa wingi na inatafuta masoko ya bidhaa zake katika pande zote za dunia. Nchikadhaa zinazoendelea katika Afrika na Marekani ya Kusini tayari zinaiangalia China kwa miwani mingine kabisa, tofauti na China ya miaka ya 70 na 80.
Huko nyuma, balozi wa nchi ya Kisoshalisti au Kikomunisti iwe kutoka Afrika, Ulaya Mashariki au
Marekani ya Kusini aliyetumwa kwenda kuiwakilsha nchi yake China alikuwa ni mtu aliyeiva kiitikadi. Baada ya Ukomunisti kuanguka miaka ya 80, waliopelekwa China kuziwakilisha nchi zao kama mabalozi, mara
nyingi ilionekana kama ni "adhabu" kwa makosa waliyofanya nyumbani. Au walipelekwa China kama watu waliochoka na waliohitaji kupumzika wakisubiri kustaafu.
Bado tuna nchi za Kiafrika ambazo hazijaondokana na mtazamo wa kizamani juu ya China. hata hivyo, kuna nchi zilizoamka toka usingizini. Nchi hizi hazipeleki tena China mabalozi kwa vigezo vya kuiva kiitkadi au kama nafasi ya kumpumzika na kusubiri kustaafu.
China wanakwenda wanadiplomasia mahiri, wajuzi wa masuala ya kiuchumi,
wenye uwezo wa kuagalia kwa karibu na kuchambua kwa makini mfumo wa kiuchumi wa China na mipango yao mingine ya kimaendeleo. Wanafanya
hivyo ili kuona ni kwa jinsi gani nchi zao wanazoziwakilisha
zitakavyoweza kunufaika na yanayofanyika China.
Katika harakati zao za kukuza uchumi wa nchi zao, China, Marekani na Ulaya zinatambua, kuwa Afrika bado ni bara lenye utajiri
mkubwa wa rasilimali ikiwemo mafuta. Kuna mafuta mengi Sudan, Chad,
Angola, Nigeria na pengine hata pwani ya Afrika ya Mashariki ikiwemo Tanzania na Kenya. Wakati huo huo Afrika inazalisha malighafi nyingi kwa bidhaa za viwandani. Kutokana na kuendelea kwa hali ya mashaka ya kivita katika Masharki ya Kati, Marekani imeigeukia Afrika katika kutafuta na kuvuna mafuta, China nayo hivyo hivyo.
Huko nyuma wakubwa walipigana vikumbo kugombea makoloni Afrika, leo wanapigina vikumbo
kugombea mafuta na malighafi nyingine za viwanda kutoka bara hili.
Baadhi ya nchi za Kiafrika na hata Marekani ya Kusini
zimeshabaini umuhimu wa kushirikiana kiuchumi na China kwa maslahi ya kiuchumi ya pande mbili. Kwa nchi hizi zinazoendelea kama vile Nigeria
na Brazil, nchina ni mshirika wa kuaminika zaidi na wa miaka mingi.
Mathalan, katika mapambano ya ukombozi barani Afrika na mapambano
dhidi ya ubeberu duniani, China siku zote imesimama upande wa Afrika na Marekani ya Kusini.
Kwa nchi masikini duniani, kuna mengi ya kunufaika kiuchumi kama zinaingia mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi na China bila
kuhatarisha sana maslahi ya kiuchumi ya mataifa hayo. Mathalan, si kawaida kwa makampuni ya China kushiriki katika vitendo vya rushwa na hujuma za kiuchumi katika harakati za kupata mikataba ya kuchumi na
pale wanapoanza shughuli za uzalishaji wa bidhaa au malighafi husika..
Kama China inakwenda Nigeria kuchimba mafuta, basi, si kampuni binafsi ya mafuta itakayofanya kazi hiyo, bali ni kampuni ya taifa ya mafuta
ya China (China State Oil Company).
Hatua ya miaka ya karibuni kwa China kuwekeza katika mahusino yake na nchi zinazoendelea hususan Afrika bila shaka imo katika
mipango ya muda mrefu ya China.Itakumbukwa, kuwa mwaka 2000 China ilizialika nchi 47 kutoka Afrika kushiriki katika mkutano wa pamoja wa
ushirikiano uiofanyika mjini Peking. Mkutano ule ulipelekea kuundwa kwa mara ya kwanza kwa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika,
(China Africa Cooperation Forum).
Mkutano ule wa Peking uliandaa mbali ya mambo mengine mikakati ya pamoja na ya muda mrefu kati ya Afrika na China. Iliamuliwa kuwepo kwa mkutano wa ngazi ya mawaziri kila baada ya miaka
mitatu ili kuimarisha na kuingia kwa undani zaidi katika ushirikiano
huo. Mikutano ilifanyika kama ilivyopangwa, kulikuwa na mkutano Addis
Ababa Ethiopia mwaka 2003 na mwishoni mwa mwaka jana mjini Peiking
China.
Matokeo mazuri ya ushirikiano huu ni pamoja na Afrika na China kuwa na sauti moja yenye nguvu katika majadiliano kwenye Jumuiya ya
Biashara Duniani , WTO. Mfumo wa kibiashara katika Afrika nao pia umebadilika. China inanunua malighafi nyingi zaidi kutoka Afrika na inauza zaidi bidhaa zake katika Afrika kulinganisha na Marekani na
Ulaya.
Kikubwa na cha maslahi ya muda mrefu kwa Afrika na hata kwa nchi yetu, ni endapo, katika ushirikiano huo, China iwe tayari kuzisaidia nchi za Afrika katika kujenga uwezo wa kuwa na viwanda vya
kuzalisha bidhaa badala ya kuishia kuuza malighafi tu.
Maggid Mjengwa.
Post a Comment