NI WAZO TU: LILA NA FILA HAZITANGAMANI
Na Dr Yahya Msangi
Jana tumefanya kumbukizi ya Baba wa Taifa.
Nimependa sana kuambatanisha kumbukizi hii na mbio za mwenge. Lila na Fila hazitangamani! Aliyebuni hili aliona vizuri.
Sasa ningependa aone mbali zaidi.
Je inaswihi kumkumbuka Mwalimu bila kuwakumbuka Kawawa na Karume kwa wakati mmoja? Kumbuka:
LILA NA FILA HAVITANGAMANI.
Kama Mwalimu alikuwa LILA basi KAWAWA NA KARUME walikuwa FILA! Walau Karume ana KARUME DAY! Masikini MFAUME! Simba wa vita! Kama tunamsahau vile?
Kuna taarifa potofu sana kuhusu mtu huyu toka zamani. Ukimuuliza mtu yeyote haraka utasikia "hakusoma"! Kwa taarifa ya wenye upotofu huu: Kawawa alisoma Makerere university wakati ikiwa "citadel" ya academic institutions dunia nzima! Kweli hakusomea digrii lakini si haba! Makerere ile haikuwa inapokea vilaza! Kawawa alichaguliwa na maprofesa wake aendelee na digrii pale Makerere! Sasa sikia hii: Kawawa alikuwa mtoto wa 8 kipindi hicho katika familia yao. Baba yao kazi yake ilikuwa uwindaji. Kawawa alipenda ndugu zake nao walau wapate elimu ya msingi na sekondari. Akamwambia Baba yake ada ambayo angemlipia Makerere aitimie kuwasomesha nduguze! Aka sacrifice elimu yake ili nduguze wasome. Wangapi leo tunaweza?
Kinyume na wasomi wetu wanaomponda Kawawa alitunga kitabu! Kikiitwa: IJUE TANU. Maprofesa wetu leo hata kutunga kitabu akiite KIJUE KIJIJI NILICHOZALIWA hawawezi! Kawawa alikuwa film director na script writer! Ndiye mwazilishi wa FILM INDUSTRY nchini wakati akiwa SOCIAL WORKER kipindi cha ukoloni!
Kawawa ndiye muasisi wa trade unionism nchini! Alianzisha chama cha social workers na hatimaye TFL (Tanganyika Federation of Labour). TFL ikashikamana na TAA kudai Uhuru WA Tanganyika! Kawawa akiitumia TFL kudhoofisha uchumi wa mkoloni kupitia migomo.
Kama ambavyo Mwalimu aliacha kazi ili ajikite kwenye harakati ndivyo na Kawawa alivyofanya. Aliacha ukarani Serikali ya kikoloni ili aijenge TFL na TAA. Karani wa Serikali enzi zile alikuwa na maslahi kuliko mwalimu wa shule! Tunalisahau hili!
Mwalimu alipoacha uwaziri mkuu nchi iliangukia mikononi mwa Kawawa! Angekuwa mroho wa madaraka na Ikulu kama jamaa zetu kingenuka! Asingekubali kumrudishia Mwalimu kiti! Angekatalia kitini kama fulani! Ukumbuke enzi zile yeye ndio alikuwa "mtoto wa mjini" kuliko Mwalimu! Angeweza kumzidi kete! Lakini Kawawa hakufanya hivyo na nchi ikasalimika na mgogoro! Mkoloni alikuwa anapiga debe agomee kitini ili ionekane waafrika hatufai! Kawawa aliweka maslahi mapana ya nchi mbele!
Sasa jana tumemkumbuka swahiba wake! Jambo jema! Lakini kwa nini tunamsahau SIMBA WA VITA kwa kiwango cha kutisha?
Hebu tuangalieni utaratibu wa kuwaenzi hawa watatu. Kama mwalimu alikuwa BABA basi BABA WADOGO ni KARUME na KAWAWA. Haifai kumkumbuka BABA na BABA MDOGO mmoja na kumsahau KAWAWA! Hili Taifa lisingekamilika lilivyo kama sio pamoja na mchango wa RADHID MFAUME KAWAWA!
Nadhani huko waliko wote watatu wananisikia!
LALENI SALAMA WAZEE WETU WAASISI WA TAIFA LETU. HOLY TRINITY!
Post a Comment