Ads

UTEKELEZAJI UMEME VIJIJINI TABORA HAURIDHISHI - BODI

Na Veronica Simba – Tabora

Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imesema hali ya utekelezaji mradi wa umeme vijijini mkoani Tabora hairidhishi.

Akitoa tathmini ya ziara waliyoifanya leo Oktoba 2, 2019 kukagua utekelezaji wa Mradi huo Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza mkoani humo; Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi husika, Mhandisi Styden Rwebangira amesema, kufuatia hali hiyo isiyoridhisha, wamelazimika kuchukua hatua ikiwemo kuzungumza kwa simu na msambazaji wa nguzo ili kazi ifanyike kwa ufanisi.

Akifafanua, amesema moja ya changamoto walizogundua ni ukosefu wa nguzo na nyaya hali inayosababisha mkandarasi kutekeleza kazi kwa kusuasua na baada ya kuzungumza na msambazaji wa nguzo ambaye ni kampuni ya Qwihaya General Enerprises, amekubali kuendelea na huduma hiyo mara moja.

“Ameahidi kuleta malori 40 ya nguzo ambayo ni sawa na takribani nguzo 4,000. Kwahiyo ni matumaini yetu kuwa kwa hapa Tabora, suala la nguzo kwa mwezi huu, tutakuwa tumetatua,” amesema Mhandisi Rwebangira.

Kuhusu suala la nyaya, amesema Bodi imemwagiza mkandarasi ahakikishe anatafuta msambazaji mwingine badala ya kumtegemea mmoja anayewahudumia kwa sasa ambaye anashindwa kutosheleza mahitaji.

“Pia, tumemwagiza Mkurugenzi wa Ufundi wa REA, Mhandisi Jones Olotu, amfuatilie msambazaji huyo ili kujua tatizo ni nini na atupatie taarifa kufikia kesho.”

Awali, Mhandisi Rwebangira alieleza sababu ya msambazaji wa nguzo kusitisha huduma husika ni kucheleweshewa malipo yake ambapo amesema tayari suala hilo lilikwishafanyiwa kazi na serikali, malipo yanatolewa kwa wakati na kwamba wamemhakikishia hilo msambazaji husika ndiyo maana naye kwa upande wake akaridhia kuendelea na kazi.

Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Bodi hiyo imegundua kuwa kumekuwa na matatizo katika kampuni za ukandarasi zinazoungana kutoa huduma ya pamoja kwa kushirikiana hususan katika masuala ya uendeshaji.

Kwa sababu hiyo, amesema kuwa wamewaagiza wakandarasi husika kujitathmini na kuhakikisha wanakuwa na lengo moja na kuwataka wasigawane kazi bali wafanye kwa pamoja kama walivyojipambanua wakati wakiomba zabuni husika.

“Tumewaonya kwamba wanapojitenga na kugawana kazi, ile nguvu na sifa iliyosababisha wakapewa zabuni husika inapotea. Wametuahidi watalifanyia kazi mara moja na kutupatia mrejesho kabla ya kukamilika kwa ziara yetu katika mikoa mingine.”

Kwa upande wake, mkandarasi husika amekiri kusuasua katika kutekeleza kazi hiyo lakini ameahidi kukamilisha kazi kwa wakati na viwango kama serikali ilivyoagiza kwani sasa wana uhakika wa kupata vifaa husika.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Rwebangira amefuatana na mjumbe mwingine wa Bodi husika, Luis Accarro, ambao kwa pamoja wanaiwakilisha Bodi nzima na wanatarajiwa kuwasilisha ripoti ya ziara hiyo baada ya kutembelea maeneo yote yaliyopangwa ikiwemo Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro.

No comments