Ads

RAIS MHE.DKT.MAGUFULI ATOA SIKU 60 KWA MASHIRIKA 187 YASIYOTOA GAWIO, WATENDAJI WAWEKWA KIKAANGONI


 

Rais Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli,akizungumza Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika Taasisi, Makampuni na Mashirika ya Umma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt.Philip Mpango,akizungumza wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika Taasisi, Makampuni na Mashirika ya Umma iliyofanyika Chamwino Ikulu jijini Dodoma.

Msajili wa hazina nchini Bw.Athuman Mbutuka,akifafanua jambo wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika Taasisi, Makampuni na Mashirika ya Umma iliyofanyika Chamwino Ikulu jijini Dodoma.

 

Baadhi ya Taasisi,Makampuni na Mashirika ya Umma yakimkabidhi Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli,gawio na michango katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo.

Sehemu ya washiriki katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika Taasisi, Makampuni na Mashirika ya Umma wakisikiliza hotuba ya Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo.

Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kupokea gawio na michango kutoka katika Taasisi, Makampuni na Mashirika ya Umma hafla hiyo imefanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo.

 

Na.Alex Sonna,Dodoma

Rais Mhe.Dkt.John Magufuli ametoa siku 60 kuanzia leo Taasisi na Mashirika ya Umma 187 yaliyoshindwa kukabidhi gawio na michango yao kuhakikisha wanakabidhi gawio hilo vinginevyo viongozi wake wajiondoe wenyewe.

Mhe.Magufuli ametoa agizo hilo leo Ikulu jijini Dodoma, wakati wa  hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma ambapo amepokea shilingi Trilioni 1.05 kutoka kwa taasisi na mashirika 79 kati ya 266.

Amesema kuwa Serikali imewekeza shilingi trilioni 59.6 kwa taasisi na mashirika 266 lakini kutokana na utendaji mbovu,ufuatiliaji dhaifu na vitendo vya wizi,rushwa na ubadhirifu kwenye mashirika ambayo serikali ina hisa mapato yaliyokusanywa kupitia uwekezaji huo yalikuwa madogo.

“Hatuwezi kuendelea kuwa na Mashirika au Taasisi za namna hii, pamoja na wenyeviti wa Bodi, tunazungumza kila mara hawataki kuelewa, licha ya Serikali kuweka fedha kiasi cha shilingi trilioni 59.6 ambazo ni fedha za watanzania kama mtaji katika Mashirika hayo, Waziri Mpango natoa siku 60 kuanzia leo ili Mashirika haya 187 yaweze kukabidhi kwako gawio” amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Fedha awaandikie barua wote ambao hawapo kwenye orodha hii, baada ya siku 60 ambaye hataleta gawio lolote ajihesabu hayupo, kila siku wanasema wanapata hasara, kila siku ni hasara tu, nchi za Scandinavia zinaendesha nchi zao kwa sababu ya gawio, wana watu waaminifu kama nyinyi mlioleta gawio hapa leo.

Rais Magufuli amewapongeza waliochangia gawio na kusema kuwa waendelee kufanya hivo kwani nchi haiwezi kuwa na maendeleo kwa kujenga miradi kama vile reli ya kisasa, kujenga hospitali na shule au mradi wa Bwawa la Nyerere bila kuwa na fedha ambazo zinakusanywa kupitia vyanzo vya kodi pamoja na gawio au michango.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesena kuwa anawakumbusha watanzania kuwa uchumi wa Tanzania utajengwa na watanzania wenyewe  na hakuna mtu atakayekuja kulijenga taifa hili.

 Waziri  Mpango amesema kuwa katika Serikali ya Awamu ya Tano ukusanyaji wa mapato umeongezeka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka iliyopita.

“Mapato yaliyotokana na gawio na michango ya Kampuni, Taasisi na Mashirika yameongezeka ambapo mwaka 2014/2015 ilikuwa shilingi bilioni 161.04 tu, na  mwaka 2017/2018 yalikuwa shilingi bilioni 842.13, na kama hiyo haitoshi mwaka 2018/2019 mapato yamefikia shilingi trilioni 1.05, hili ni ongezeko kubwa sana na linastahili pongezi kwa Serikali yako Mheshimiwa Rais” Mhe. Mpango.

Awali,Msajili wa Hazina, Bw.Athumani Mbutuka amesema kuwa Serikali imefanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kudhibiti   matumizi katika Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma, ambapo Juni mwaka 2019 Mashirika ya Umma 15 yalipunguzwa hadi kufikia 8 na kupunguza gharama za uendashaji.

Pia ameongeza kuwa  katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka huu, Ofisi ya Msajili wa Hazina imevirudisha viwanda 31 vilivyokuwa havifanyi kazi, pamoja na kurudisha Serikali viwanja, mashamba na nyumba.

No comments