Rais Magufuli aongeza siku 20 usajili laini za simu, atoa agizo kwa TCRA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiweka alama ya kidole gumba alipokwenda kusajili Laini yake ya simu kwa njia ya alama ya Vidole katika kampuni ya simu ya Airtel Mjini Chato Mkoani Geita. Desemba 27, 2019.Kushoto ni Msajili wa laini za Simu wa Airtel tawi la Chato Michael Martin.
Kwa ufupi
Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Desemba 27, 2019 amefanya usajili wa laini yake ya simu kwa kutumia alama za vidole na kuwasisitiza Watanzania wote wahakikishe laini zao za simu zinasajiliwa kwa alamu za vidole kama ilivyoelekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameongeza siku 20 kwa Watanzania watakaoshindwa kusajili laini zao za siku kwa alama za vidole ifikapo Desemba 31, 2019 huku akifanya usajili wa laini yake ya simu kwa kutumia alama za vidole mjini Chato Mkoa wa Geita.
Rais Magufuli amefanya usajili huo leo Ijumaa Desemba 27, 2019 akiwa mapumzikoni nyumbani kwake Chato na kuwasisitiza Watanzania wote wahakikishe laini zao za simu zinasajiliwa kwa alamu za vidole kama ilivyoelekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania, imeeleza Rais Magufuli ameongeza siku 20 kuanzia Januari Mosi hadi 20, 2020 kwa wote ambao watashindwa kusajili laini zao katika kipindi cha kuishia Desemba 31, 2019 kama ilivyotangazwa na TCRA kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo kuugua na kukamilisha upatikanaji wa namba ama Vitambulisho vya Taifa.
“Rais Magufuli amesisitiza baada ya muda huo hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika na ameagiza TCRA kuhakikisha laini ambazo hazijasajiliwa zinazimwa,” imeeleza taarifa hiyo.
Amefafanua usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni muhimu kwa usalama wa nchi ikiwamo kuepusha vitendo vya utapeli na ujambazi vinavyofanywa na wahalifu, ambao licha ya wengi wao kukamatwa na vyombo vya dola wameendelea kusababisha usumbufu na upotevu mali za wananchi hususani fedha.
Pamoja na kuwasalimu wananchi wa Chato Mjini waliojitokeza kushuhudia wakati akisajili laini yake kwa alama za vidole, Rais Magufuli amewasalimu na kusikiliza maoni yao kuhusu shughuli hiyo na pia mwananchi Steven Joseph Wandwi anayefanya biashara ya kuuza chipsi na mishikaki akawaongoza wenzake kumuombea.
Wandwi pia amemshukuru kwa utumishi wake mzuri ulioongeza kasi ya maendeleo kwa Taifa hasa vijana ambao sasa wanachapa kazi bila bughudha.
Kabla ya kwenda kusajili laini yake ya simu, Rais Magufuli ametembelea Mtaa wa Chato Kati na ametoa pole kwa familia ya Marehemu Atanasi Masansa Mnaku aliyefariki dunia juzi Jumatano Desemba 25, 2019 na mazishi yake yamepangwa kufanyika kesho.
Post a Comment