Ads

Mané awasili nchini Misri kuhudhuria sherehe ya utoaji tuzo za CAF bila kuambatana na Mo Salah!

Sadio Mane' wa Liverpool

Na Mwandishi Maalum, Cairo

Sherehe za utoaji tuzo za CAF zinatarajiwa kuhudhuriwa na magwiji mbalimbali wa mchezo wa kandanda duniani kama vile Drogba, Eto'o, Cafu, Arsene Wenger na Pierluigi Collina.

Sadio Mané raia wa Senegali aliwasili katika uwanja wa ndege Hurghada  jana Jumatatu akiwa tayari kuhudhuria Sherehe za Utoaji Tuzo kwa Wachezaji Bora za CAF kwa mwaka 2019 ambazo zitafanyika leo katika Hoteli ya  kifahari ya Sahl Hashish .

Winga huyu hatari wa Liverpool aliwasili kwa ndege maalum ambayo ilitarajiwa kumchukua pia mchezaji mwenzake Mohamed Salah ambaye pia kama Mane amependekezwa kuwania tuzo ya mchezaji bora kwa  mwaka uliopita wa 2019. Kutokana na kutowasili jana inahofiwa Nyota huyo wa Misri huyo atazikosa sherehe hizo za utoaji tuzo za mwaka huu.
Taarifa zisizothibitishwa inasemekana Salah hakutoa uthibitisho wowote kama atahudhuria sherehe hizo.

Aidha imefahamika muwaniaji nambari tatu wa tuzo hiyo Mualgeria na winga machachari wa timu ya Manchester City Riyad Mahrez  hatoweza kuhudhuria sherehe hizo za CAF kwa vile atakuwa anashiriki na timu yake katika mtanange wa nusu fainali ya Kombe la Ligi utakaopigwa leo Jumanne  baina ya Man City na Manchester United.

Mané  anatajwa kuwa na nafasi kubwa  kunyakuwa tuzo  ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa mwaka 2019, kutokana na uchezaji wake wa hali ya juu katika msimu wa 2018-2019 wa Ligi Kuu ya Uingereza ambako alitunukiwa tuzo ya kiatu cha dhahabu kwa kufanikiwa kufunga mabao 22 na pia alifunga mabao 10 katika mechi 11 katika michuano
ya Ligi ya Mabingwa ya UEFA ambapo timu yake ya Liverpool iliibuka kidedea baada ya kuukosa ubingwa huo kwa miaka 14.

Diamond Platnumz akiwasili nchini Misri na Wapambe wake
Wakati huohuo Mwanamuziki nguli wa Tanzania na Kimataifa Naseeb Abdul Al'maarufu Diamond Platnumz amewasili nchini Misri tayari kutumbuiza leo katika Sherehe hizo za Utoaji Tuzo za CAF kwa Wachezaji Bora kwa mwaka 2019 ambazo zitafanyika leo katika Hoteli ya  kifahari ya Sahl Hashish .

Diamond akiwa amebarizi katika Hotel Sahl Hashish

Akiwa katika hoteli hiyo ya Sahl Hashish alionekana mwenye bashasha na kuchangamka. Diamond kama kawaida yake ameahidi  kutoa tumbuizo la hadhi ya kimataifa. Msanii huyu sio mgeni kualikwa katika sherehe na matamasha ya kimataifa. Tayari Diamond aliwahi kualikwa na kushiriki katika tamasha la ufunguzi wa michuano ya AFCON iliofanyika mwaka 2017 nchini Gabon.


No comments