RC MAHENGE ATAKA WANAFUNZI WOTE WALIOCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA KWANZA WARIPOTI SHULENI KAMA ILIVYOPANGWA
Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameziagiza Halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma kusimamia na kuhakikisha wanafunzi wote elfu 33,803 waliofaulu darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanaripoti shuleni na kuanza masomo ifikapo Januari 6 mwaka huu.Dkt. Mahenge ametoa kauli hiyo jana Januari 3 kwenye kikao kazi cha Watendaji na Wasimamizi wa elimu Mkoa wa Dodoma.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Maduka Kessy akizungumza kwenye kikao kazi cha Watendaji na Wasimamizi wa elimu wa Mkoa wa Dodoma.
Alisema elimu kwenye Mkoa wake ndio kipaumbele cha kwanza na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa namna inavyoendelea kuwekeza kwenye elimu kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia awali, msingi hadi sekondari kidato cha nne na ujenzi wa miundombinu ya kutolea elimu.Alisema nchi nyingi za Afrika bado ziko nyuma kimaendeleo kwa sababu bado zinakabiliwa na changamoto ya kuwa nyuma kwenye nyanja za elimu, sayansi na teknolojia.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma akifungua kikao kazi cha Watendaji na Wasimamizi wa Elimu ambao ni Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma, Idara ya Elimu, Mdhibiti Ubora wa Shule Kanda ya Kati, Maafisa Elimu, Taaluma Mkoa na Wilaya za Dodoma kwa upande wa msingi na sekondari, Makatibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu na Wadhibiti ubora wa elimu wa Wilaya zote Mkoani humo.
“Kupitia kikao hiki niwaagize kuhakikisha mnatoka na mikakati ya kuinua hali ya elimu kwenye Mkoa na kuinua kiwango cha ufaulu wa mitihani ya Taifa ya elimu ya msingi na sekondari (Darasa la saba na Kidato cha nne) kwa kuwa bado hali na kiwango cha sasa hakiridhishi,“Japokuwa Mkoa unapandisha ufaulu kila mwaka, lakini bado hairidhishi, kwa mfano, katika mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2018 Mkoa ulishika nafasi ya 21 Kitaifa na upande wa elimu ya Msingi ufaulu wa Mkoa kwa mwaka 2019 ulikuwa asilimia 74.69 na hivyo Mkoa kushika nafasi ya 23 ukiulinganisha na mikoa mingine” alibainisha Dkt. Mahenge.Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Maduka Kessy amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa atasimamia maelekezo yaliyotolewa na kamati ya ushauri ya Mkoa inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa iliyoagiza kuandaliwa na kufanyika vikao vya wadau wa elimu wa Wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma na Kikao cha Wadau wa Elimu wa Mkoa mzima ili kupata jukwaa la kujadili changamoto za kielimu na kuziwekea mkakati wa kuendelea kuzishughulikia.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge akifungua kikao kazi cha Watendaji na Wasimamizi wa elimu Mkoa wa Dodoma.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni mkoa uweze kuchukue hadhi inayostahili kwenye elimu ikiwa ni Makao Makuu ya Nchi.Kikao hicho kilichohusisha Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma idara ya elimu, Mdhibiti ubora wa shule Kanda ya Kati, Maafisa elimu, taaluma Mkoa na Wilaya za Dodoma kwa upande wa msingi na sekondari, Makatibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu na Wadhibiti ubora wa elimu wa Wilaya zote Mkoani Dodoma. Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.
Post a Comment