SERIKALI IMEJIPANGA KUHAKIKISHA NISHATI YA MAFUTA INAPATIKANA MUDA WOTE NCHINI
Na Hafsa Omar-Dar es Salaam
Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani, amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa mafuta nchini kujadili hatua ambazo nchi itazichukua endapo uhaba wa mafuta utajitokeza katika kipindi hiki cha Mripuko wa maradhi ya Virusi vya Corona. Tukio hilo lilifanyika Machi 17 2020 jijini Dar es Salaam, katika Ofisi za Wakala wa Uagizaji Mafuta Kwa Pamoja ( PBPA) na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, Kamishina wa Petroli na Gesi Adam Zuber na viongozi mbalimbali wa Taaasi za Wizara ya Nishati na wadau mbalimbali wa mafuta.
Aidha amesema kuwa Serikali imepanga kukutana na wadau hao ili kuona namna bora ya kuhakikisha mafuta yatapatikana muda wote kulingana na mahitaji ya nchi, endapo itatokea dharura yoyote kwenye nchi ambazo wafanyabiashara na wanaponunulia mafuta na kuhakikisha kuwa shughuli zote zinaendelea nchini .
“ Sisi kama Serikali pamoja na wadau ni jukumu letu kuhakikisha kwamba mafuta yanapatikana muda wote tena ya kutosha kuendesha shughuli zenu wafanyabiashara lakini na kuendesha shughuli za Serikali pamoja na shughuli za kijamii zote ziendelee kama kawaida”.Alisisitiza.
Aidha alifafanua kuwa nchi inajenga miradi mingi mikubwa ya kimaendeleo na kiasi kikubwa miradi hiyo inategemea sana mafuta katika kuendesha shughuli za uendeshaji. Aliongeza kuwa nchi ambazo Tanzania inanunua mafuta mpaka sasa bado wanaendelea na uzalishaji wa mafuta na bado hawajafunga mipaka yao. Hata hivyo kwa upande wa Serikali lazima ichukue hatua Madhubuti kwa kushirikiana wadau wake ili kuweza kujiwekea akiba ya mafuta ya kutosha nchini. Wakati huo huo Dkt Kalemani amewatoa wasiwasi Watanzania kwamba mafuta yapo ya kutosha kwa muda wa miezi miwili ijayo yakiwemo mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ndege. Aidha Serikali inajipanga kuongeza akiba yake ya mafuta ili yatosheleze siku nyingi zaidi.
Alifafanua kuwa hata kama nchi ina mafuta ya kutosha kwa kipindi hiki lakini Serikali haitakaa kimya na kuona nchi inakosa mafuta ya kutosha kama Serikali lazima itafute kinga badala ya kusubiri kuhangaika na tiba.
Waziri Kalemani aliwashukuru wadau hao wa mafuta kwa michango yao mizuri yenye uwazi na inayoangalia hali halisi ya upatikanaji wa mafuta inavyoendelea nchini na kuwapongeza kwa kutoa michango yenye tija ya kulisaidia Taifa endapo kama itatokea dharura yoyote katika kipindi hiki cha maradhi Corona.
Nao wadau wa mafuta nchini, wameipongeza Serikali kwa kitendo cha kuwaita ili kuzungumzia suala hilo ambalo limejikita katika kuchukua tahadhari ambazo zinajitokeza katika kipindi ambacho dharura itayojitokeza na kuahidi kuwa wapo tayari kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mafuta nchini yanapatikana muda wote.
Aidha walitoa ushauri wa njia mbalimbali ambazo wanaziona zikichukuliwa zitasaidia katika kukabiliana na uhaba wa mafuta kama hilo tatizo la uhaba litajitokeza siku za mbeleni.
Njia hizo ni pamoja na kutafuta wazalishaji wa mafuta wa nchi nyengine endapo wale wazalishaji wa awali watafunga mipaka ya nchi zao katika kipindi hiko cha mpito.
Post a Comment