"Nitaendelea Kuhitaji Msaada Wenu" Hapa Mzee Mkapa Ulimaanisha Nini na Itakuwa Lini Tena?
HAYATI MZEE BENJAMIN WILLIAM MKAPA RAIS MSTAAFU WA AWAMU YA TATU
Na Dkt. Hassan Abbasi
Mwaka 2018 tarehe ambayo kwa bahati mbaya sikuitunza kichwani nilipokea simu yenye sauti nzito kutoka kwa mzungumzaji aliyekuwa upande wa pili: "Mkurugenzi hujambo?" "Mimi ni Mzee Mkapa'" alijitambulisha kwangu Mzee Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu na kiongozi wetu mpendwa wa Awamu ya Tatu tuliyemzika kijijini Lupaso, Masasi, Mtwara, Jumatano ya Julai 29, 2020, na kuhitimisha rasmi mwendo wa miaka 82 alioutembea katika dunia hii. Licha ya kujitambulisha nilikuwa bado siamini kupokea simu ya Mzee Mkapa na akajitambulisha kwa unyenyekevu vile kwa mtu mdogo kwake kiumri na kiuongozi kama mimi. Si kwamba katika maisha yangu ya kikazi kwa sasa sipati nafasi ya kuzungumza na viongozi wakuu au mashuhuri wa aina yake, la hasha! Au kwamba katika maisha yangu pia huko nyuma kama mwanahabari sijapata kufanya mahojiano na viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi yetu, la hasha! Nikiwa mmoja wa wahariri vijana barobaro na mwanahabari za maisha ya viongozi mashuhuri wakati huo, nimepata kukutana na kuwahoji viongozi wakubwa katika mihimili yote ya dola na pia katika mawanda ya diplomasia. Nimepata kumhoji Rais Mstaafu Mzee Kikwete siku Taifa Stars ilipoifunga Burkinafaso nyumbani kwao, nimepata kumhoji aliyekuwa Spika wa Bunge Mzee Samuel Sitta wakati wa sakata la Richmond, nimepata kumhoji Jaji Mkuu Barnabas Samatta siku alipostaafu rasmi na hata kumhoji Jaji Mkuu Augustino Ramadhani siku alipoanza majukumu yake rasmi au Mama Fatma Karume kujua kwa undani historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na kifo cha Mzee Karume na mengineyo lakini pia kuhoji Wanadiplomasia wengi akiwemo aliyepata kuwa Balozi wa Marekani nchini, Balozi Mark Green, alipokuwa akihitimisha safari yake ya kikazi Tanzania. Simu ya Mzee Mkapa siku ile itabaki kuwa maalum na wosia muhimu kwangu na wale nitakaowataja katika yulojia hii. Mosi, siku hiyo nilipokea simu na kuzungumza kwa mara ya kwanza na ya mwisho katika maisha yangu na mtu wa aina ya Mzee Mkapa, galacha sana katika fasihi, nguli katika fonetiki, manju wa sintaksi na hata simantiksi za lugha ya kiingereza tuliyekuwa tunamuona kama rejea tukiwa shuleni. Wakati akiwa tayari kiongozi katika ngazi mbalimbali kama Uwaziri na baadaye Urais, sisi wanafunzi wa fasihi na simantiksi kila tulipokuwa tukimsikiliza tulimtumia kama rejea kwa kufuatilia sana hotuba zake ndani na nje ya nchi hasa anapochapa kimombo lakini pia hata Kiswahili. Alikuwa kamusi yetu ya misamiati mipya na rejea yetu katika matamshi. Kwa wanaotaka kuamini hili soma pia "My Life, My Purpose" uvune hazina ya misamiati. Kwa hivyo siku ile nilipokea simu ya "role model" wangu katika mawanda ya fasihi katika lugha ya kiingereza, moja ya masomo niliyochukua katika elimu ya juu ya sekondari. Naamini unanielewa aina ya furaha mtu unayoweza kuwa nayo! Pili, ukiacha shida aliyokuwa nayo ya kuhitaji picha za kumbukumbu kutoka kwenye maktaba ya Idara ya Habari-MAELEZO niliyokuwa naiongoza wakati huo, simu ile itabaki kuwa chachu ya kuendelea kumuenzi Mzee Mkapa! Ni katika simu ile unapata nguvu kupongezwa na mtu wa aina ya Mzee Mkapa. Nakumbuka alisema: "MAELEZO naijua sana, mmepabadilisha mno kwa sasa, endeleeni kufanya mageuzi." Kabla sijaendelea, niliitoa na sasa naitoa tena hii kama "dedication" kwa TeamMAELEZO wooote popote mlipo. Tatu, labda hili la tatu ndilo linalonifikirisha sana, kunitafakarisha sana na kunifanya nipekeche macho yangu kuzuia machozi kumkumbuka Mzee Mkapa ambaye tayari tumemlaza kwenye nyumba yake ya milele pale kijijini Lupaso. Ni hivi: Baada ya kuwa ameniomba nimtafutie kwenye maktaba yetu picha za rafikiye, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uswidi, Olof Palme, aliyepata kuja nchini miaka ya 1970 (na kwa bahati nzuri picha zikawepo za kutosha), Mzee Mkapa akaniambia mambo mengine mawili muhimu katika tanzia yangu hii. Kwanza, ni katika mazungumzo haya ndipo aliponidokeza kuwa yu mbioni kukamilisha kitabu cha maisha yake. Akasema nitawategemea sana hapo MAELEZO kwa picha zaidi za kumbukumbu muhimu za maisha yangu hasa zile za kikazi! Na hakika TeamMAELEZO hatukumwangusha. Nilifarijika mwaka jana aliponiletea mwaliko wa uzinduzi na baadaye nakala ya bure ya kitabu chake "My Life, My Purpose; A Tanzanian President Remembers." Picha kutoka maktaba ya Idara ya Habari-MAELEZO ni miongoni mwa zilizosawiri kitabu chake hicho na kila alipozitumia alinakilisha hati miliki ya picha hizo kuwa ni za MAELEZO au Tanzania Information Services. Mzee Mkapa aliijua vyema Idara ya Habari-MAELEZO, kwani SHIHATA aliyopata kuianzisha ilizaliwa katika ubavu wa MAELEZO na hata miaka mingi baadaye ilipohitimisha kazi zake; majukumu, mali na wafanyakazi walirejea MAELEZO na hata baadhi ya wasaidizi wake waandamizi wa habari akiwemo dada Maura Mwingira walipita/ kutoka MAELEZO. La Pili, tukiendelea na simu yake ya mwaka 2018: wakati tunaendelea kumshukuru kwa kitabu chake na uungwana wake wa kunakilisha hatimiliki ya picha kadhaa alizotumia kwa MAELEZO, fauka ya hayo, kama kuna kitu kinaniliza leo na nilikuwa na wakati mgumu pale kijijini Lupaso na kumkumbuka sana Mzee Mkapa basi ni kile cha mwisho alichoomba katika simu ile na bahati mbaya sikupata kuzungumza naye tena: "Nitawategemea sana MAELEZO katika machapisho yangu mengi, mna hazina kubwa hapo ya picha. Nitaendelea kuhitaji msaada wenu." Leo Mzee Mkapa hatunaye tena, ametangulia mbele za haki, ametenda wema amekwenda zake, kwa Mola wake, hakutazama nyuma, kuna ya kutafakari katika kauli yake hii. Mengi yameandikwa, yamesemwa sana lakini leo nikiwa nimerejea jijini Dar es Salaam jioni hii na viongozi wengine wa nchi najiona nimebaki mpweke na nimejiuliza sana niandike? Na kama ndiyo ni kuhusu nini kumhusu Mzee Mkapa? Lakini roho imeniambia lazima nimuage Mzee Mkapa kwa kuandika kitu. Sasa naandika nini? Ningeweza kueleza aliyoyafanya katika sekta mbalimbali za umma ikiwemo habari na michezo nchini; ningeweza kuzungumzia mageuzi aliyosimamia kwa kuunda taasisi za huduma kama NHIF, za mapato kama TRA na za udhibiti kama PCCB! na mengine mengi. Haya yameandikwa na kusemwa vya kutosha. Nikiri imenichukua zaidi ya siku 6 za kuamua niandike nini! Maana lazima niandike kumuaga mwandishi mahiri kwa andiko stahiki! Nikiwa mtu mwenye mapenzi na fasihi, nimeandika tanzia nyingi kuhusu siku na maisha ya viongozi wengi duniani lakini pia nimesoma tawasifu za viongozi wengi duniani ikiwemo ya Mzee Mkapa mwenyewe; nikiri kuandika maneno machache kumhusu Ben Mkapa ilikuwa ngumu sana. Sikubahatika kufanya kazi kwa karibu na Mzee Mkapa akiwa kiongozi madarakani, sikubahatika kufanya naye kazi kwa karibu sana akiwa mstaafu, lakini lililodhahiri unapomfanyia Dhukuru mtu wa aina ya Ben Mkapa unabaini, kwa minajili ya athari chanya zinazotokana na maono yake na kazi zake, amekuwa mtu adhimu na adimu, na zaidi johari yenye thamani zaidi kuliko tu kuwa naye karibu. Linaloniuma sana ni ahadi yake hasa siku ile aliponipigia simu aliposema: "Nitaendelea kuhitaji msaada wenu!" Inafikirisha! Nimeeleza hapo juu, tulishamsaidia kupitia wasaidizi wake, kumpatia baadhi ya picha kwa ajili ya chapisho la rafiki yake Olof Palme na nyingine akaja kuzitumia katika "My Life, My Purpose" lakini alimaanisha nini kusema "nitaendelea kuhitaji msaada wenu? Hili linabaki kuwa fumbo kuu! Januari 31 mwaka huu, Mhe Rais Magufuli aliniteuwa kuwa Katibu Mkuu na hivyo kuniondoa MAELEZO kama ofisi yangu ya kila siku na sasa kiofisi nimehamia na "nashinda" zaidi Wizarani. Ingawa siku tatu baadaye, yaani Februari 3, Mhe Rais alinirejeshea jukumu la kuendelea kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, kimsingi, na kimajukumu ya kila siku "nashinda" sana Wizarani na si tena MAELEZO! Alichokisema Mzee Mkapa katika "nitaendelea kuhitaji msaada wenu" ni fumbo kuu. Sasa najaribu kuendelea kulielewa. Na kama ilivyoandikwa katika Biblia kuwa ni wale tu wenye uelewa ndio wataelewa maana ya unabii na kama inavyoelezwa katika Quran Tukufu kuwa "Fadhakir Inafaat Dhikira" (Kumbusha Iwapo ni Muhimu Kufanya Hivyo), basi kauli hii ya Mzee Mkapa inabaki na maana kubwa kwangu na kwa wanatasnia wenzangu. Na ninawakumbusha. Leo Mzee Mkapa hayupo nasi lakini nataka kuamini tunapaswa kuendelea kuwa naye. Wenzangu pale MAELEZO na tamathali ya jumla ya Idara ya MAELEZO ikiakisi vitengo vyote vya habari Serikalini alivyovianzisha mwaka 2003 na hata tasnia ya habari kwa ujumla iliyomjenga sana, nataka kusema nanyi hapa katika tanbihi ya dhukuru hii. Katika tamathali ya "nitaendelea kuhitaji msaada wenu" Mzee Mkapa anafumbo kubwa alilotuachia; naamini anataka si MAELEZO tu, bali sote wanatasnia, tuendelee kumuenzi tena akiwa ameshatuachia namna ya kufanya hivyo kupitia falsafa yake ya "Ora Et Labora" (Sala na Kazi). Nayaandika haya kuwakumbusha tu wenzangu kuwa Mzee Mkapa hajakamilisha mahitaji yake kwetu na kwamba, ninavyoendelea kuuelewa unabii katika tamko lake, ni kwamba kimwili alihitaji tumsaidie tu kwa picha, bado kiroho anatuhitaji sana na ataendelea kutuhitaji. Juzi saa sita usiku nilipigiwa simu ikihitajika picha ya Mzee Mkapa kwa ajili ya sehemu ya maziko yake. Nilifikiria sana. Usiku wa siku moja kabla ya maziko yake, nilipata ujumbe saa 11 alfajiri kuhusu mashada ya maua kwenye kaburi lake. Kumbe, wenye kuelewa maana sasa tunapaswa kuzidi kuelewa. Mzee Mkapa ameendelea "kuhitaji msaada wenu" hata akiwa amelala kwenye jeneza lile. Hata sasa akiwa amelala katika nyumba yake ya milele Mzee Mkapa anaendelea kuhitaji msaada wetu. Tuendelee kusali kumwombea na kuwaombea marehemu wengine wote kila tupatapo nafasi. Lakini sala haitoshi, ametuonesha shauku yake kwetu kuwa ni pamoja na kuchapa kazi! Nazungumza tena na watu wangu wa MAELEZO kama namna nyingine ya kuupambanua ufunuo wa Mzee Mkapa kwangu, kuwa si MAELEZO tu atakaowahitaji. Hapana. Katika "Ora Et Labora" niwaombe Watanzania tumuenzi Mzee Mkapa kwa yote na tumsamehe alipotukosea, iwapo lipo alilotukosea au kutukwaza na pia wanatasnia ya habari kwa upana wake tumuenzi Mzee wetu kwa sala na maombi. Katika "Ora Et Labora" Mzee Mkapa anatuhimiza kuchapa kazi. Niwakumbushe Watanzania, WanaMAELEZO, tasnia ya habari kwa ujumla na maafisa wa habari wenzangu Serikalini, Mzee Mkapa anaposema atatutegemea si kwa sala tu bali KAZI. Tuchape kazi hasa, tutimize wajibu wetu katika taaluma hasa na tusitetereke katika kulinda amani, utulivu na mshikamano na kuenzi misingi ya fani zetu. Fumbo la "nitaendelea kuhitaji msaada wenu" ni dhahiri lilikuwa la kinabii na linalohusu maisha ya dunia na akhera pia. Huenda katika dunia Mzee Mkapa alihitaji picha na tulishampa katika "My Life, My Purpose" lakini katika maisha ya akhera kauli ile, siku ile, kutoka kwa Mzee Mkapa, lilikuwa fumbo kuu, tuendelee kulifumbua. Leo ametangulia mbele ya haki Mzee Mkapa hahitaji picha tena, mabango tena wala mashada pekee, anahitaji sana shada za sala na maombi yetu. Anahitaji tuyaenzi aliyoyaamini kwa kazi kweli kweli! Hakika ametuachia mtihani mzito ndio maana nabaki naelewa lakini bado pia nabaki najiuliza kila mara: Mzee Mkapa kwa hii kauli ya "nitahitaji msaada wenu" na haya yaliyokufika siku ile ya Julai 23, 2020 Ulimaanisha Nini? Itakuwa Lini tena? Na wapi tutakuona tukupe kile ulichotamani na kuomba tuendelee tukusaidie? Hakika umetuachia fumbo kuu, tutaendelea kulifumbua kupitia Ora et Labora🙏🏼🙏🏼🙏🏼🙏🏼 Mola akupe pumziko la amani na la milele Mzee wetu galacha wa simantiksi, sintaksi na fonetiki uliyeacha alama za kukumbukwa milele katika nchi yetu na dunia!
Dk Hassan Abbasi - Mwandishi wa tanzia hii ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Post a Comment