Ads

Wapenzi wa mpira wajipanga kurasimisha ‘Jukwaa la Kandanda’



Na Jacquiline  Mrisho
 mwambawahabari

Wapenzi wa mpira wa miguu wamejipanga kurasimisha jukwaa la kandanda kuwa jukwaa rasmi litakalozungumzia changamoto zinazohusu mpira wa miguu na jinsi ya kuzitatua ili kuongeza kasi ya maendeleo ya mpira nchini.

Mipango hiyo imejitokeza baada ya wapenzi wa mpira huo kuona kuwa kuna haja ya kuandaa kongamano litakalowaunganisha ili kuzungumzia masuala hayo kuliko kuendelea kuongelea suala hilo katika grupu waliloliunda katika mtandao wa kijamii wa ‘WhatsApp’.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti  wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hilo, Henry Tandau alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu lengo la Kongamano hilo litakalofanyika  kwa siku mbili kuanzia Septemba 3 mwaka huu katika uwanja wa Taifa.


“Sisi wapenzi wa mpira wa miguu tumeamua kuandaa kongamano la kubadilishana mawazo na kutoa maoni kuhusu mpira huu ambapo lengo kubwa ni kupanga namna ya kurasimisha jukwaa hili kuwa chombo rasmi kitakachozungumzia masuala ya maendeleo ya mpira huu”, alisema Tandau.

Tandau ameongeza kuwa malengo mengine ya kongamano hilo ni kuongelea changamoto zinazokabili uendeshaji wa mpira wa miguu nchini, kuangalia jinsi ya kuubadilisha mpira wa miguu wa Tanzania kuwa wa kitaalam zaidi pamoja na kuchangia mawazo juu ya matatizo yanayozikwamisha klabu za Tanzania kushindwa kukidhii vigezo vya kushiriki mipira ya nje ya nchi.

Ametaja baadhi ya washiriki watakaoshiriki katika kongamano hilo kuwa ni wanachama wa jukwaa hilo, wawakilishi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),  Bodi ya Ligi, Viongozi wa Klabu mbalimbali za mpira wa miguu, Baraza la Michezo Tanzania (BMT) pamoja na  Waandishi wa habari.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa anategemea Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye kuwa mgeni rasmi atakayelifungua kongamano hilo kwa kuwa ndiye waziri mwenye dhamana katika masuala ya michezo pia ni mmoja wa wadau wakubwa wa Jukwaa hilo.

No comments