Ads

LUGHA ADHIMU YA KISWAHILI NDIO ITAKAYOIKOMBOA TANZANIA KIUCHUMI NA KITEKNOLOJIA!

Profesa Chacha Nyaigotti Chacha - wa Kiswahili


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizinduwa mfano wa kamusi Kuu ya Kiswahili hivi karibuni Bungeni Dodoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizinduwa mfano wa kamusi Kuu ya Kiswahili hivi karibuni Bungeni Dodoma.


Mhe Salama Kikwete akishiriki katika uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili..


Waziri wa Habari,  Utamaduni Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe akitangaza kuanza hafla ya uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili hivi karibuni.

Mbunge wa Viti Maalum Nd Salma Kikwete  Mdau mashuhuri wa kukikuza Kiswahili nchini na Kimataifa akihojiwa katika hafla ya uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili iliyofanyika Bungeni hivi karibuni.


Mafano wa jarida Kamusi Kuu ya Kiswahili.

SUNDAY, NOVEMBER 25, 2007


KISWAHILI NDIO KITAKACHOTAIFISHA ELIMU KWA MANUFAA YA JAMII YA WATANZANIA

  • Viongozi wa Kitaifa wanaowakilisha Nchi wajiamini wasioone haya kutumia Kiswahili!
  • Wataalamu waache ubinafsi kama kweli wana maarifa yawekwe katika Kiswahili!
  • Wanasiasa waongoze mapinduzi ya kukiamini Kiswahili sio tu katika kuombea kura bali katika kulifanya Taifa letu la watu walioelimika!
  • Mfumo wa sasa wa elimu ya juu kwa kiingereza ni Uabunuwasi!
  • Kuna Kiongozi mmoja wa Kitaifa tu anayenzi matumizi ya lugha adhimu ya Kiswahili wangeongezeka kuwa japo 20 ingekuwa jambo la maana sana!
  • Kigezo cha kiingereza ni mojawapo kilichotufanya tugwaye kukubali kujiunga haraka na Jumuiya ya Afrika Mashariki!

    Na Zerkala Pravdu
    Nakumbuka katika miaka ya mwanzo ya 1980/81 wakati nikiwa katika Chuo cha Uandishi wa Habari sasa IJMC nilihudhuria kongomano la Maendeleo ya Kiswahili lililofanyika Chuo Kikuu Mlimani, ambapo mojawapo ya mipango na matarajio yalikuwa yamebainishwa ni kuwa ifikapo 1991/92 lugha ya kufundishia sekondari na katika yyuo vya Elimu ya juu. Lakini kilichotokea kuanzia pale Uingereza ikamimina paundi milioni kadhaa na kwa vile awamu ya kwanza ilikuwa inaondoka ikaja awamu ya 2 ambayo kama mnavyojua ikawa ya rukhsa basi ikawa rukhsa kufanya mambo mepesi lakini mambo mazito hapana!

    Ndio kugeuza lugha ya kufundishia ni jambo kubwa. Hata hivyo kutumia lugha ya kigeni kwa kawaida ni endelevu lakini kwa kikundi fulani cha watu wenye vipaji na uwezo kujifunza haraka taaluma iliyomo katika lugha husika kwa lengo baadae kuineza kwa mapana na marefu katika jamii husika .

    Wakati watu wanasema afadhali tungeachia madini yawe ardhini hadi tutakapo pata maarifa ya kuyachimbua sisi wenyewe ili tupate faida labda asilimia 100 nafikiri ni mwaka 3000! Kwa upande wa elimu kwa maarifa tulioanza kuyapata kupitia , Kiingereza, Kirusi, Kichina, Kijerumani, Kijapani na Kireno kama tungekuwa na mkakati endelevu kuyaweka katika Kiswahili (Akademia ya Sayansi na Teknolojia) hivi leo tungekuwa labda tujadili ni taaluma gani imebakia kuwa haitolewi kwa lugha ya Kiswahili kikamilifu katika ngazi ya Chuo Kikuu.

    Kuna watu ukisema Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia katika Vyuo Vikuu wanatuona machizi lakini ukiwauliza swali nchi gani duniani imepiga maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa lugha ya kuazima jibu hamna. Wakorea wameendelea kwa kutumia Kikorea( japo miaka ya 1960 kiwango chao cha maendeleo kiuchumi na kijamii hakikuwa juu sana kuliko sisi), hivyo hivyo Waswidish, Wadeni, Wanorwe, Wafini na Wabelgiji. Ingekuwa rahisi kutumia lugha ya kigeni kujiendeleza basi Waswidish ambao katika kila watu wawili wanajua kiingereza basi wangetumia lugha hiyo lakini kiutamaduni kielimu na urithi wao kwa ujumla umeifanya lugha ya Kiswidish ndio mujarab kuelimisha na kuleta maendeleo ya Wanaskandinavia hao. Ieleweke kule Wanajita Waskendinavia (nchi nyimgine ni Norwei, Finlandia lakini kila nchi ina lugha yake ya Taifa na ndio iliotumika kuwaelimisha kuanzia ngazi ya chekechekea hadi Chuo Kikuu.
    Hapa nchini lazima niseme tunakipenda kiingereza kama lugha wengine ni zaidi wangependa hata kwenda Uingereza ikiwezekana kila mwishoni mwa wiki na hii sio hapa nchini tu hata kwa waswahili wanaokuwepo hasa Ulaya ya Mashariki! Wakati fulani katika miaka ya 86 hadi 92 nikiwa Shirikisho la Usovieti na baadae Urusi foleni iliyokuwa ikisababisha vifo wakati wa kupanga foleni za viza likizo ya majira ya baridi (Januari hadi Machi) ni katika Ubalozi wa Uingereza jijini Moscow . Mimi rohoni nikawa najiuliza zaidi ya kupewa viza je hupewa nauli ya kwenda London pia! Lakini ni mapenzi tu inasemekana kuna baadhi ya Waafrika wakifika Ulaya hasa ya Mashariki bila ya kwenda London au Paris (kwa wale watokao nchi zilizokuwa makoloni ya Ufaransa) inakuwa kama vile ufike Saudia bila kufika Makka na Madina kwa Muislamu. Na vivyohivyo Mzazi anayehisi hakifahamu Kiingereza uzuri angependa mwanae amwage ung’eng’e ile mbaya! Ndio kipimo cha kwanza kwa waswahili kuwa umesoma ni kukimanya kiingereza barabara lakini hiyo inafifia kwa vile kuna sisi tunaojua Kirusi, wako wa Kichina , wako wa Kispanyola! Sasa labda niguse wale wajanja wajanja ambao hujidai kujua Kiingereza wakati kwa ukweli kimewakataa. Na humu wamo wote wapo Viongozi wa kitaaluma na wanasiasa. Bila ya kutaja majina, wadhifa kuna baadhi ya viongozi hawawezi kusoma uzuri kiingereza lakini kwa hofu ya kuambiwa hawakusoma wanajikalifisha na matokeo ni ajali tupu! Maana baada ya kumwita mtu ‘Principal’ unamwita ‘Headmaster’ hii ilitokea mwaka mwaka 1980 kwa vile tulikwenda mahali na Mkuu wa Chuo chetu cha Tanzania School of Journalism Mwenyeji wetu alitafsiri midhali Chuo chetu ni School basi na Mkuu lazima ni ‘Headmaster’ mimi nasema sawasawa ndio matatizo ya lugha hizi ukizingatia mwenyeji wetu alikuwa Mhitimu wa Mlimani wa mwaka 1975! Sio ajabu katika warsha ,semina, kongamano au mikutano yenye kuhutubiwa na wahutubiaji wenye matatizo na kiingereza (hasa matamshi mtiririko na ‘istilahi zake’) utaona watu wanainamia chini wengine kujibaraguza kuanzisha mada ndogo kabla ya Msemeji Mkuu hajamaliza hotuba yake.

    Wakati umefika Wasomi , wataalamu na viongozi wasijing’ate mdomo bure kama kiingereza kinawafanya wawe na kigugumizi watumie lugha yetu adhimu. Sasa natoa changamoto kwa mtu hapa nchini anayejiita msomi, mtaalamu kuanzia wenye shahada za uzamili na hasa wale wenye za uzamivu wengine wanakuwa nazo hadi 7! Kama kweli wao ni wataalamu sio waakisi wa utaalamu basi waufungue huo kwa kuuweka katika lugha ya kiswahili. Sio jambo la kujivunia au kujinadi kuwa sisi ni wataalamu wakati miaka zaidi ya 40 imepita jamii haina maarifa ya sayansi na teknolojia halisi iliyojikita ndani yake ambayo ni ya lazima ili kila mmoja mwenye utashi aweze kujifunza na hatimaye kutoa mchango wake kwa jamii. Korea watu wanasema katika miaka ya 60 kimaendeleo ilikuwa kama sisi lakini kwa mikakati mizuri ya kielimu na kiuchumi na kwa kutumia lugha yao sisi sasa ni wateja wao wa magari yao ya Hyundai. Sisi kwa vile hata zile baiskeli zetu za Swala pale kiwandani Mwenge zilikuwa zinatengenezwa kwa teknolojia ya kuakisi sio ajabu pale penye kiwanda sasa wanauza mitumba. Tungepaswa nasisi tunawauzie kile ambacho wao hawana lakini sio korosho! Mfumo wa elimu ya juu kuendelea kufungiwa katika kijaluba cha kiingereza ambacho mtu ambaye ni mahiri wa lugha hiyo ndio anaweza kujaribu kuipata umetukwamisha umetuhukumu kuwa tegemezi kimaendeleo hadi sasa! Wenzetu wa Kuba wamebahatika lugha ya kispanyola ndani yake ina msingi wa sayansi ya teknolojia ndio maana kuchakarika kwao na Komredi Castro kumewafikisha mahala pazuri kielimu na kiafya licha ya kuwa chini ya vikwazo dhalili vya Wamarekani tokea 1959!
    Na kama mfumo huu wa kulazimisha kiingereza kuwa lugha ya kupatia taaluma katika elimu ya juu kama ulivyo sasa daima dumu hatutaweza kupiga maendeleo endelevu. Maana hii elimu itakuwa sawa na ahadi au utani uliomo katika Hekaya za Abunuwasi ambapo kuna visa vitatu kimoja ni kile kwa uchungu mzazi masikini alimmulika mtoto wake katika hodhi la maji ya barafu kuhakikisha ni mzima ili asubuhi apate mikwanja ya kujikwamua na umasikini. Tajiri husika alikataa. Kumlipa yule kijna asubuhi kwa vile aliota moto! Kesi mwishoe ikafika kwa Abunuwasi ambaye naye aliwaalika Sultan na yule Tajiri asubuhi asubuhi lakini wakakuta kila kitu kiko mbali na moto iwe nyama, mchele na kadhalika. Yule tajiri akamchongea kwa Sultan Abunuwasi kuwa anawashindisha na njaa tu hakuna kitu kitaiva. Abunuwasi akatoa hoja ikiwa yule mtoto masikini kule hodhini alipata joto basi na vile vyakula vitaiva ama sivyo basi Tajiri awajibike ampe yule kijana bingo yake. Mwafaka ukafikiwa tajiri akatoa bingo na Abunawasi akaweka vyakula motoni karamu ikaiva. Sasa elimu hii kwa miaka 40 imekuwa haileti matunda yanayokusudiwa kwanza Tanzania haina rasilimali ya kukifanya kiingereza kuwa lugha ya Taifa ili watu wawe na uwezo wa kufurahi na kucheka kwa lugha hiyo, wafikiri na kutafakari kwa kiingereza ili kuweza kutatua mahitaji mbali mbali ya kitaaluma na ya kijamii. Hadi leo hakuna Akademia yetu wenyewe ya Sayansi na Teknolojia zilizopo ni zile za kuakisi. Nina hisi wako wataalamu hapa nchini ambao wanafahamu kwa mfumo wetu wa elimu ya kuakisi hatutafika mbali lakini hofu yao kubwa kazi watakayoianza hawataimaliza itabidi iendelezwe na vizazi vijavyo. Lakini wako ambao ninawaita bila ya kimeme kuwa ni wasaliti wao wanajali nafasi zao katika jamii wanafurahia maisha na kwamba siku zao za kuishi duniani si nyingi maana katika msahafu wanasema uhai wa binadamu umekadiriwa kuwa ni makumi matatu mawili na kumi moja! (miaka 70). Kufahamu jambo la msingi ambalo litastawisha jamii yako na kuleta mapinduzi makubwa yatakayoleta maendeleo ya kijami na uchumi lakini kwa ubinafsi tu hufanyi hivyo huu ni usaliti. Sawa na hekaya ya Abunuwasi ambapo mtu alifika kwake kuazima punda Abunuwasi akasema punda hayupo mara punda akalia yule mtu akamwambia punda si huyo, Abunuwasi akajibu umekuja kuazima punda au mlio kama mlio basi Abunuwasi akalia ‘Hoo..hoo.. !’ Akamwambia yule mtu apande aende! Sasa wataalamu kuendelea kuwalazimisha Watanzania kujifunza Kingereza ili waelimike wakati rasilimali za kufanya hivyo hazipo kwani kama ingekuwa rahisi basi Sweden ingefanya hivyo kwa vile nusu ya raia wake wanaporomosha kimombo ile mbaya! Huu mlio wa punda wa Abunuwasi hautotufikisha popote.

    Wa kwanza kurusha jiwe ni Wanasiasa hivi sasa kuachia Rais Jakaya Kikwete kuhutubia kule Addis mwaka jana wakati wa Mkutano wa AU kwa Kiswahili hakuna kiongozi wa kitaifa aliyethubutu kuhutubia hadhara yoyote ya kimataifa iwe nyumbani au nje katika Serikali, hata hivyo tumebahatika kuwa na kiongozi mmoja wa pekee mwenye hadhi ya Kitaifa anayefanya hivyo Mama Salma Kikwete kuanzia mwaka jana. Sehemu mojawapo alikofanya jambo hilo jema la kutukuka ni Amerika ya Kusini Mexico, na mwaka huu kule Bamako Mali na katika hadhara nyingine kadhaa hapa nchini halikadhalika hivi karibuni wakati wa ziara ya Marekani . Kiongozi wetu kama kawaida yake amefanya vitu vyake kwa Kiswahili. Tungepata viongozi wengine 20 kama huyu mambo yangekuwa mutrib sana kwa hadhi ya Kiswahili. Mimi kwa ufahamu wangu hotuba zote za viongozi wa kitaifa kuanzia Makatibu Wakuu, Mawaziri hadi viongozi juu kabisa wa Kitaifa wanapokuwa na ziara rasmi au kuhudhuria mikutano hotuba zao hutayarishwa kwa kiingereza. Sasa ikiwa ndio hivyo je kwanini wanashindwa kuwa na nakala ya Kiswahili ambayo ataisoma kwa heshima ya lugha yetu mwanana na Taifa letu. Wajumbe wengine katika mikutano hiyo wataifuatilia kwa lugha zao kama kawaida. Hivi tunataka mpaka siku moja Rais wa Nigeria au wa Chad afanye hivyo na sisi ndio tuige hii hali ya kutojiamini itaendelea mpaka lini Watanzania wenzangu? Hivi sasa licha ya kuwepo Shule nyingi zinazotumia kiingereza kama lugha ya kufundishia kiwango cha ufahamu wa kingereza unazidi kushuka kiasilimia kwa kasi sana.
    Katika miaka ya 70 wakati Kiingereza kilipoanza kushuka Watanzania walikuwa hawazidi milioni 16 sasa ambapo tunakaribia milioni 40 hali iko pale pale ndio kila mtu hapa Tanzania anaweza kusema Yes au No! Lakini kiwastani wasiokimanya kimombo ni wengi zaidi hivi sasa kuliko 1970! Tofauti sasa ni kwamba kuna vyombo vya habari vingi kuanzia magazeti zaidi ya 40, televisheni na radio zaidi ya 20. Kuonyesha Watanzania walivyopagawa na kiingereza haihitaji kufanya utafiti mkubwa ni kwamba ukifanya mapitio ya magazeti ya mitaani yenye kuchanganya lugha ndio maarufu! Utakuta Kichwa cha Habari ya makala au riwaya yenye maneno ya kingereza sio sentenso ya kiingereza! Lakini Habari au Riwaya ni ya Kiswahili! Sijaona jambo hili duniani kokote lakini hapa Tanzania inaelekeka limekubalika kwa vile hatujui athari yake ina uzito gani! Nafikiria siku moja mwenye kukimanya Kirusi au Kichina aandike kichwa cha habari kwa Kirusi au Kichina taarifa iandikwe kwa Kiswahili itawezekana kweli?. Jambo hili lazima niliseme bila ya kupepesa macho kuwa ubunifu wa aina hii unashusha hadhi ya Kiswahili. Hali hii ni sawa na ile kampeni ya kuwataka kina dada zetu waache kupaka mikorogo! Je kama unafikiri mkorogo wa kujichubua uonekane mweupe ni mbaya je mkorogo huu wa kichwa cha habari lugha nyingine na maelezo yote kwa kiswahili ni mzuri? Aidha katika hali ya kudhalilisha hata baadhi ya vituo vya televisheni vinaonyesha kubeza Kiswahili , mathalan katika taarifa ya habari wanamweka muhusika wa habari katika picha na sauti kwa lugha ya kiingereza bila ya kuweka maelezo ya sauti ya kiswahili kama ilivyo desturi ya kutumia habari za aina hiyo. Kwa sasa ni kituo cha TVT peke yake kinajiepusha na kuchanganya lugha hasa ikizingatiwa taarifa ya habari ya Kiswahili hapana budi kila kitu kieleweke kwa lugha hiyo si vinginevyo. Mimi siwezi kusema uvivu wa kutayarisha maelezo ndio sababu nafikiri ni dharau tu kwa lugha ya kiswahili iliyojikita miongoni mwa wanataaluma ikiwa pia na Waandishi wa Habari jambo linalopaswa kuanza kupigwa vita kila siku kama kweli tunataka kuienzi lugha yetu ya Kiswahili..

    Siku hizi kuna tabia ya kujifanya kwa makusudi kuzungumza Kiswahili bila kufuata taratibu kanuni na sheria ya lugha! Kuna mtu unamsikia matamshi ‘Mtu nane’, Watu mbili! Kuna tabia ya kuvumilia Kiswahili kibovu ilianzia kwa Wazungu, Wahindi, Waarabu sasa hata Waswahili wanavumiliwa. Hatujali wala hatuheshimu kurekebisha maneno ya maandishi mahala pa karamu panawekwa kalamu ! Karibu inakuwa ‘kalibu’ kimatamshi! Yaani ni ukweli kwamba Watanzania huwa ati wanaumia zaidi mtu akiboronga Kiingereza lakini Kiswahili wanasema inaruhusiwa wanaita ‘free style’! (nafikiri tafsiri sisisi ni ‘mtiririko huria’) Kama tutafanya Kiswahili ‘ mtiririko huria’ ina maana kila kitu chetu kuanzia, tabia, utamaduni, siasa, uongozi ni ‘ mtiririko huria’ pata mpatae ukikosa ujinga wako! Hii sio sawa tukubali kuna mambo mazito yachukuliwe leo na sio kesho ile mipango ya muda mfupi na mrefu ya kuendeleza kiswahili ,irudishwe miradi ya majaribio iliyopaswa kufanywa miaka ya 90 ifanyiwe utekelezaji ! Kukubaliwa Kiswahili kuwa lugha ya kimataifa kuende sambamba na kuwepo mkakati wa kitaifa wa kukipa hadhi ya lugha Kiswahili kuwa lugha ya taaluma katika vyuo vya juu vya elimu ya Taifa kampeni ianze kwa Taifa kuona umuhimu wa kiswahili. Nasikia Mzee Ibrahim Kaduma aliposema kuwa Chuo Kikuu cha Mzumbe wanakusudia kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia rasmi taaluma hapo baadhi ya Watanzania wakatishia kuwaondoa vijana wao. Napenda kuwauliza hawa wazazi wasiokubali ukweli kuwa Kiswahili kinatumika katika Sekondari hadi Chuo Kikuu kama lugha isio rasmi ya kupata taaluma. Mhadhiri ambaye hajimudu kitaaluma anashindwa kueleza dhana kwa Kiswahili husababisha wanafunzi wake kulichukia somo lake na kuwa na wasiwasi na uwezo kwa somo husika. Na yeye akiwa kweli ufahamu wake ni finyu hujificha kitaaluma kwa kuwaporomoshea mibambo ambayo haikidhi haja ya kutoa taaluma.

    Sasa ombi langu kwa Wanasiasa ambao mara nyingi kwa siku hizi ni wasomi wa ngazi za juu kabisa kuwataka kutafakari hivi wana lengo gani na Taifa hili kielimu itaendelea kuwa katika mfumo huu tegemezi sana sana inaakisi tu maendeleo lakini sio maendeleo halisi na endelevu. Hii hali ya kutojiamani itaendelea mpaka lini takriban wote wale ambao tumebahatika kusomea katika nchi ambazo hawatumii Kiingereza bado utando machoni haujatutoka kumaizi kuwa lugha yeyote ikipewa jukumu nayo inakua . Na kwamba ni uamuzi wa kisera na pia kimkakati kuona katika muda sio mrefu elimu yetu inakua kwa manufaa na sio iendelee kuwepo maabara. Hali ya sasa ikiwepo ikiachiwa kuendelea hapo 2025 tutakuwa kama hivi kwa wale watakaojaaliwa kuwa hai wakati huo. Hapo awali nilizungumzia usaliti ujanja katika mfumo wa kutoa elimu ambayo imefutikwa katika kiingereza. Msomi aliandika kwa ukali ambapo alisema elimu ya juu Kiswahili hapana na moja ya hoja yake ni kwa nini Viongozi wa juu nchini wanahangaika kuwapeleka watoto wao nje ambako wanakwenda kupata elimu ya juu nzuri! Lazima nimueleze ukweli wa mambo sio kila mtoto wa mkubwa au Mtanzania mwenye uwezo anayempeleka mtoto wake Ulaya kusoma ananufaika na elimu ya huko. Kama ilivyo kawaida ni wale wenye uwezo kikweli kikweli kiakili ndio wananufaika kama inavyotarajiwa. Msiogope wengi hao wanaopelekwa kwa jeuri ya fedha nawahakikishieni bure ghali. Kuna rafiki yangu mmoja amenidokeza kwa jina kuwa kuna afisa mmoja mwandamizi wa idara nyeti ya Umma kwa jinsi mtoto wake alivyo goigoi kimasomo basi ofisi ya kigogo huyo imekuwa kama ile taasisi ya kupata Elimu kwa mtandao TGDLC ! Amenieleza rafiki yangu huyo kuwa ili kuweza kumsaidia huyo bazazi mchanga inabidi atume kwa mtandao maswali au mazoezi ya masomo ama kwa simu au mtandao au nukshi na baadae mzazi wake au kupitia wataalamu huyafanyia kazi na kumrejeshea. Vema mtoto huyu hatimaye atapata Shahada yake lakini huyu hana tofauti na tukio la juzi juzi la yule kijana aliyekamatwa akimfanyia mtihani wa Taifa wa Kidato cha 4 swahiba wake ! Hivi sasa kwenda Ulaya kusoma hakutegemei kama kijana amefaulu vyema katika mitihani ya Taifa ya kidato cha 6 kama zamani bali sifa na nguvu kubwa inatokana na ukwasi wa Wazazi wake. Ulaya na Marekani kuna vyuo vya kitapeli vingi tu kuhudumia hawa ‘mamilionea’ na watoto wao. Watanzania wasihofu hata kidogo juu ya vijana wachovu wa siku hizi wanaorejea majuu na shahada za kuotesha maua au kuchonga vijiti! Sisemi wote ni wachovu wengine wanakuja wameiva na kwa kweli wanarejea nchini kwa vile wana uchungu na nchi yao tu kwani kule Ulaya wanakuwa wamepata kazi nzuri tu mifano ipo! Ila wengi wengineo wanarejea kuatamiwa na Wazazi wao na pili kuwa tayari kuandaa mapambano ya kugombea urithi wa mali! Sasa ukweli elimu, taaluma na stadi zitazoikomboa na kuijenga na kuiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii endelevu nchi yetu itatokana na msingi wa maendeleo ya sayansi na teknolojia iliyojikita ndani ya jamii yetu ya Tanzania. Mimi ni mmojawapo siogopi Shirikisho la Afrika Mshariki lakini kama kuna sababu kubwa mojawapo ya hofu ya kujiunga nayo kwa kufikiria kuwa tujiunge na wenzetu mara kiwango cha elimu lkitapokuwa kikubwa! Hii maana yake moja tu ni kuwa tutaona inafaa pale ambapo uwezo wa kukimanya kiingereza tumewafikia Wakenya na Waganda. Kwanza lazima niseme wazi tufute hiyo ndoto hakuna wakati ambapo tutawafikia hao jamaa kama vile wao hawataweza kukiporomosha Kiswahili murua hata wadhikiri ashakum bila nguo kama sisi Watanzania! Sasa wasiwasi wetu Watanzania ni unatokea wapi? Inasemekana Mungu hana huruma lakini ana rehema amewapa mazingira mazuri ya kujifunza kingereza sisi tuna tunu ya mazingira mazuri ya Kiswahili. Sasa hivi Kiswahili ndio lugha kuu hapa Afrika Mashariki tatizo kubwa ni moja tu kutojiamini basi! Tukubali jambo moja sisi lazima tujitambue ni tai tuliolelewa na vifaranga vya kuku lakini hivi sasa Kiswahili kinatuambia kuwa sisi ni tai tupange siku tena isiwe mbali tukunjue mabawa yetu na kuruka juu juu kama yule tai wa hadithini ambaye baada ya kutanabaishwa hakurejea chini kuchakurachakura kama kuku! Nawashauri Watanzania wenzangu waache kupoteza rasilimali binafsi na za nchi kwa kuwapeleka watoto wao kwenda kujifunza kiingereza tu! Ikiwezekana kabla ya kutumia rasilimali zao hizo adimu wajiridhishe kuwa hao watoto wao wana uwezo wa kwenda kujifunza huko majuu kupata taaluma yenye faida kwao wao binafsi na nchi yao? Taarifa ambazo zimezagaa mara nyingi kama ilivyo mchagua jembe si mkulima vijana hawa miaka mingi wanapoteza wakibadilishwa kutoka chuo kimoja kwenda kingine bila matokeo kuwa ya kuridhisha. Hatimaye kwa kukata tamaa vijana wetu hugeuka kuwa mateja sawa na wa hapa nyumbani isipokuwa huyu atakuwa ameupata majuu kwa vile alipanda ndege au pipa wanavyoita la masafa marefu. Binafsi naamini asilimia kubwa ya vijana ambao wanaonekana wachovu iwe wa vigogo au Watanzania wa kawaida huenda wangeweza kupata taaluma au stadi wanazozihitaji kuendeshea maisha yao kwa misingi ya kujitegemea kama elimu ingetolewa kwa kiswahili. Kwa kutumia Kiswahili tutapata faida nyingi sana zisizo na idadi mojawapo ikiwa kuwanusuru hawa vijana wetu na hii kadhia ya kuwapeleka ukimbizini Ulaya ambako wanakosa chakula cha roho wanakuja watupu na kwamba mbegu tunayoimpanda itasababisha ombwe la kila kitu kuanzia maadili hadi utaifa kuangamia muda sio mrefu sisi kutokweka. Tukubali kupunguza tujitolee muhanga tukubali ,kulaumiwa ili tuwekeze kwa ajili ya maendeleo ya kweli ya Taifa letu. Kuendelea kuzunguka Mbuyu hakuna hatima njema kwa mustakabali wa Taifa letu! Lugha ni muhimu sawa kama chombo cha kujipatia elimu, maarifa, stadi na utalamu, ustaarabu nikimaanisha mila na desturi. Ni kweli mtu mwenye kufahamu lugha nyingi ni kigezo tosha kuwa ni mstaarabu zaidi kwa vile anazijua tamaduni za binadamu wenzake wengi. Lakini inabakia jambo moja la msingi katika kujifunza lugha yeyote lazima kuwepo na mbinu na mkakati na kujituma kwa muhusika isiwe mtu anataka kujifunza kiingereza halafu hafanyi jitihada zozote yaani anakuwa kazi yake kwenda shule za gharama kubwa lakini ni mvivu kusoma hasomi fasihi wala riwaya za lugha anayojifunza, huyu ni sawa tu na mtu anayesoma vichwa vya habari za magazeti bila ya kwenda katika kina cha habari yenyewe. Vijana wengi japokuwa wanasoma katika shule zinatumia kingereza kufundishia hawafanikiwi kuimanya lugha hiyo kwa vile utaratibu unaotumiwa sio wa kisayansi. Vitabu vya riwaya hawasomi, nyumbani huwa ni vioja vitupu siku hizi kuchezea vikatuni vya kompyuta au kuangalia vipindi mfululizo vya maizgio na nyimbo tu. Kusomea lugha kama taaluma nyingine inafanyika kisayansi na sharti mtu ajenge tabia na utamaduni wa kujisomea mfululizo. Na ikiwezekana uwe unazungumza lugha hata kama watu watakuita punguani lakini ajabu Watanzania hao hao wanolilia kingereza wanaona haya kuzungumza kiingereza ili ijulikane wapi wanakosea ili wasahihishwe. Kwa kumalizia napenda kusisitiza kuwa Kiswahili kama yalivyo madini kama tutakusanya nguvu tukajipanga kimkakati na pia kukubali kuwekeza na kuwa wavumilivu na kuwacha tamaa na ubinafsi ndani ya Kiswahili kuna kula kitu. Ukombozi kitaaluma na uhakikisho kuwa hii sayansi na teknolojia isioyoepukika kama tunataka kupiga maendeleo ya haraka kijamii na kichumi basi tutaitia mkononi kwa muda sio mrefu sana. Tujipe lengo sambamba na visheni ya kidunia 2025 hili liwemo la lugha ya kufundishia elimu ya juu kama tutaendelelea kukaidi. Namaliza kwa swali pale Ghuba wana uwezo wa kuajiri walimu wa kiingereza wote wazuri wa dunia na kuhakikisha Waarabu wote wanazungumza kiingereza lakini kiarabu kinapewa kipaumbele sasa ninyi na hizi hela zetu za madafu zisitosha tunadiriki kujidanganya kuwa Taifa letu litaelemika kwa kuking’ang’ania kiingereza kisichotutaka? Tayari kuna istilahi 20,000 za taaluma mbali mbali na nyingine ziko jikoni kwa mujibu wa BAKITA kinachosubiriwa ni uamuzi wa Serikali kutangaza kuwa Kiswahili ndio lugha rasmi ya kufundishia katika vyuo vya elimu ya juu. Baada ya hapo kila kitu kitajipanga kwa umuhimu wake. Narudia uamuzi wa kubadili lugha ya kufundishia sio jambo dogo lakini ili Taifa lipate maendeleo ya haraka lazima kuwepo maamuzi makubwa na ya msingi kama huu wa lugha ya kufundishia elimu ya juu. Hatuwezi kuitaifisha elimu ya juu kwa lugha ya kuazima ambayo haina asili wala utamaduni wa karibu na sisi (Mifano awali nimeitoa Waswidi na hata Wajerumani walio karibu hawaitumii sembesu sisi Wamatumbi wa Afrika ! Makubwa haya!). Miaka zaidi ya 45 imepita woga wote wa nini si ni kweli Baba wa Taifa ametufundisha kupanga ni kuchagua. Sasa tuchague kupata maendeleo ya kweli ya elimu na jamii yetu ya Kitanzania au tuendelee kuakisi maendeleo ya wengine . Kama mambo yetu yangekuwa mazuri kweli hatuhitaji viongozi wetu kwenda kufia Ulaya wakitafuta matibabu. Lakini tukiendelea hivi zaidi yakuoneana wivu nani wanawapeleka watoto wao majuu kujifunza ‘elimu kiingereza’ (mimi naibatiza hivyo ‘elimu kiingereza’) kwa wingi tutaanza kuoneana wivu nani wanaokwenda mara nyingi kutibiwa ulaya na labda kufia hukohuko! Mwenyezi Mungu apishie mbali! Kiswahili pekee ndio kitalifanya taifa lake kuendelea katika misingi ya sayanasi na teknolojia na kwamba ndoto yetu kuwa sisi ni tai itatimia kwa hili uthubutu wa kisiasa unahitajika fikiria wewe uliye na miaka 40, 50 na 60 na uko katika uongozi kitaifa na unashikilia elimu yetu iwe ya kuakisi kwa vile umezoea kiingereza hivyo ni kweli Wajerumani wasemeje, Wawidish nao je?. Tujivue hili gamba la kutojiamini la miaka 40 na ushei tumetanga na njia tuamue tuende kwenye ile nchi tulioahidiwa wakati tunadai Uhuru wa kisiasa. Inasemekana ni rahisi kudai Uhuru wa kisiasa lakini kama hukuwa makini huo uhuru utafanana na ule wa mazingaombwe au ndoto ukiamka hamna kitu. Elimu hii iliyofunikwa katika kijaluba cha kiingereza sio mujarab na wala haitotufikisha katika nchi ya ahadi! Changamoto kwa wale wote katika nafasi za uongozi katika Taifa letu iwe serikalini,taasisi na asasi nyinginezo na hasa zisizo za kiserikali na vyama vya siasa wakati wa maamuzi magumu umefika. Kiswahili chenyewe kimeonyesha njia kwa sasa kinakubalika kimataifa lakini wenye ‘madini’ hawana habari tunatarajia nini? Hatimaye tuamue kwa pamoja tukipe dhima Kiswahili ili Watanzania waanze kupaa kwa vile sisi ni TAI hatupaswi kuwepo chini na kuendelea kuchakurachakura kama kuku na vifaranga vyake.
    Mungu Kibariki Kiswahili, Mungu Wabariki Viongozi wetu, Wajaalie ufunuo kama ulivyowajaalia Wakorea, Wajapan, Wataiwan, Warusi,Waswidi, Wanorwei, Wafini na Wapenda Maendeleo wote Duniani!

    (Mwandishi wa makala hii ni mwandishi habari mwandamizi  ni Meneja Uhusiano Mstaafu wa Kampuni ya Reli Tanzania –TRL)
    maezhabari@gmail.com

No comments