YALIYOJIRI WAKATI WA UZINDUZI WA KITUO CHA FORODHA CHA PAMOJA KATIKA MPAKA WA TANZANIA NA ZAMBIA, MKOANI TUNDUMA, OKTOBA 05, 2019
Alionena Rais John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa hafla hiyo:
Sherehe hizi za ufunguzi wa Kituo cha Forodha cha pamoja hapa Tunduma,kwa upande wa Tanzania na Nakonde,upande wa Zambia,ni muhimu sana na naipongeza na kuishukuru wizara ya Fedha kwa uamuzi wa kujenga kituo hiki,wizara imenigusa na nasema inafanya kazi nzuri ikiwamo kutoa fedha za miradi mikubwa ya maendeleo huku ikishuhudiwa hata mishahara ikitoka mapema.
Baada ya kufungua kituo hiki Tunduma,kwa upande wa Tanzania,pamoja na mwenzangu wa Zambia, Rais Edgar Lungu, nitakwenda pia Nakonde,upande wa Zambia,pamoja na mwenzangu wa Zambia,ambako pia kumeandaliwa sherehe kama hizi.
Miaka 3/4 iliyopita,nilipita hapa kushughulikia barabara ya Tunduma Sumbawanga, baadae nikarudi kuwaomba kura nikiwa mgombea Urais kwa kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi,ninashukuru kura zenu zimeniwezesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Karibu sana Rais Edgar Lungu,wa Zambia,karibu nyumbani mheshimiwa,sisi ni ndugu,mazingira,utamaduni na watu ni walewale na kikubwa zaidi sisi sote ni wanachama wa SADC.
Tanzania na Zambia tuna historia toka wakati wa harakati za ukombozi kusini mwa Afrika chini ya waasisi wa Mataifa haya mawili,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kenneth Kaunda, na badae tumeendelea kuwa washirika wa Uchumi.
Bomba la Mafuta la TAZAMA linafanya kazi vizuri lakini Reli ya TAZARA,iko mahututi licha ya jitihada na maelekezo ya kuiweka hai Mamlaka hiyo kutozaa matunda,baada ya hotuba zetu,nitazungumza na mwenzangu wa Zambia,na kuona nani anakwamisha maendeleo ya TAZARA na ikibidi yeye atumbue upande wa Zambia na mimi nitumbue upande wa Tanzania.
Uwekezaji wa Zambia nchini Tanzania umekua kutoka shilingi milioni 89.2 mwaka 2010 na kufikia shilingi bilioni 265.6 mwaka 2018,Kufikia Septemba 2016,jumla ya makampuni 8 ya Zambia yamesajiliwa nchini katika uwekezaji uliogharimu mamilioni ya shilingi na kuzalisha ajira 312,aidha nakushukuru Mheshimiwa Lungu,kwa nchi yako kuendelea kupitisha mizigo ya nchi yako nchini,mwaka 2017 asilimia 38 ya mizigo yote ya iliyohudumiwa na mamlaka ya bandarinTanzania (TPA) ilielekea Zambia.
Kituo hiki cha Forodha cha Pamoja,kitakua na manufaa na kutazidi kurahisisha shughuli za biashara lakini weledi wa maafisa husika utakua ni nyenzo kuu ya kuleta tija ama vinginevyo.
Napenda kuwashukuru wadau wa maendeleo kama hawa wa TRADE MARK EAST AFRICA (TMEA),ambao wamefadhili ujenzi wa kituo hiki hawa ndiyo wafadhili wa kweli wanaothamini na kutambua vipaumbele vyetu. TMEA wamefadhili ujenzi wa vituo vya mipakani kama hivi vikiwemo Holili,Taveta,Namanga,Rusumo na kwingineko.
Hii mipaka iliyowekwa na watu fulani kutoka sehemu fulani kwa madhumuni ya kututawanya ili watutawale kiurahisi isiwe kikwazo kwa wananchi kutembea pamoja na isitucheleweshe na lazima vikwazo vya kimipaka viondoke.
Kwa wananchi na watumiaji wa kituo hiki,itunzeni miundombinu ya kituo hiki na kuwafichua watu watakaokua na nia ovu ya kutaka ama kuhujumu miundombinu ya kituo hiki.
Naye Rais Edgar Lungu,wa Zambia alikuwa na haya ya kusema:
Kituo hiki cha Nakonde - Tunduma kina shughuli nyingi katika ushoroba wa kanda hii ya Kusini mwa Afrika,ambapo kwa wastani inakua na magari ya mizigo zaidi ya 600 kwa siku na kituo hiki kinarahisisha biashara kwenye huu ushoroba wa Dar es salaam na kuna biashara ya mamilioni ya dola za Kimarekani.
Baada ya uboreshaji wa miundombinu ya kituo hiki,upitishaji wa mizigo utakua wa haraka kabisa na kuongeza kiasi cha mizigo,kwa hiyo kuja kwetu hapa leo kunahamasisha kutekeleza ikiwemo ushindani wa ushoroba huu na kuongeza kiasi cha mizigo kwa nchi zetu hizi mbili.
Kituo hiki kitasaidia sana kupunguza muda ambao watu walikua wanakaa mpakani kutoka siku 4 awali kufikia siku moja.
kufanyakazi kwa kituo hiki cha Forodha cha pamoja mpakani kutasaidia sana na kurahisisha utendaji kazi.
Nashukuru serikali zote mbili kwamba hazikuchukua tu hatua za kuwasaidia wafanyabiashara wakubwa peke yao lakini pia wafanyabiashara wadogo wanavuka mpaka kupitia mkataba uliosainiwa na mamlaka husika kufuatia watu wetu wengi wanaishi kwa biashara ndogo.
( Taarifa hii Imeandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO)
Post a Comment