TAASISI ZA ELIMU NCHINI ZIMETAKIWA KUWAPA WASOMI MAARIFA YA KUTUMIA RASILIMALI KULETA TIJA ENDELEVU!
TAASISI za elimu nchini zimetakiwa kuwaandaa wasomi kwa kuwapa maarifa yatakayowezesha kutumia rasilimali zilizopo hapa nchini vizuri ili kuleta maendeleo endelevu kwa ajili ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya kivukoni jijini Dar es Salaam, Profesa Richard Kangalawe wakati wa kusanyiko la wasomi wahitimu wa chuo hicho.
Profesa Kangalawe amesema nchi ya Tanzania si maskini bali wasomi wana kazi kubwa ya kufikiria kwa umakini kwa kutumia rasilimali zilizopo zilete maendeleo endelevu kwa taifa.
“Tanzania si maskini kazi kubwa ni wasomi kukuna vichwa vyetu ili kutumia rasilimali zilizoko kuleta maendeleo,” alisisitiza Prof. Kangalawe.
Alisisitiza kuwa duniani kote wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu wamekuwa ni chachu ya maendeleo katika taasisi husika wanazozihudumia kwa kuwa wamekuwa ndio wafadhili wakubwa wa program mbalimbali za masomo vyuoni.
Prof. Kangalawe amesema wasomi wanahitajika kwa ajili ya kusimamia uchumi wa viwanda kwani maendeleo endelevu ni suala la ulimwengu mzima ndio sababu umoja wa mataifa ulianzisha malengo ya maendeleo endelevu ambayo yanataka dunia kuyasimamia.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya kusanyiko hilo, Jumanne Muluga alisema changamoto kubwa kwa wahitimu ipo kwa kuwa bado hawajarudisha kile walichokipata kwa jamii.
Kwa upande wake Dkt. Ahmed Sovu ambaye ni mhadhiri chuoni hapo alisema wasomi wamekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia na kuhamasisha masuala mbalimbali kwa kutambua mazingira na kutoa masuluhisho yanayozunguka jamii.
Imetolewa na:
Kitengo Cha Habari na Mawasiliano
Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Post a Comment