KIWANDA CHA KUCHAKATA NYAMA CHA TANCHOICE KUAJIRI WAFANYAKAZI 500
Mratibu wa Mradi katika kiwanda cha nyama na machinjio cha Tan Choice Dkt. Juma Mtei akitoa maelezo kuhusu mashine za kuchinjia mifugo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea kuona namna kiwanda kilivyojipanga kuanza shughuli za uzalishaji wake katika Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
Kiwanda cha kuchakata nyama na machinjio ya mifugo cha Tan Choice kinatarajiwa kuzalisha ajira 500 za kudumu katika fani mbalimbali nchini mara baada ya kuanza kazi rasmi mapema Machi, 2020.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa kiwanda hicho Bw. Albert Kilalah wakati akiwasilisha taarifa ya kiwanda kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zilizowasilishwa za kiwanda hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akihutubia wakati wa mkutano wake na watendaji wa kiwanda cha kuchakata nyama cha Tan Choice (hawapo pichani) alipotembelea kiwandani hapo Januari 17, 2020 Wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani.
Waziri Kairuki alifanya ziara hiyo (Ijumaa tarehe 17 Januari, 2020) ambapo alipata fursa za kukagua maeneo ya kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchakata nyama bora (organic meet) na kusema amevutiwa na kupongeza jitihada za uwekezaji huo mkubwa.
“Nimefarijika kuwa hadi sasa mmeweza kutoa ajira zaidi ya 300 na ni matarajio yenu kutoa ajira 500 kiwanda kitakapoanza kazi mapema mwaka huu na tutaendelea kuwaunga mkono ili kuwafikia wananchi kwa utoaji wa bidhaa bora zenye uhakika,”alisema Waziri Kairuki.
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha Tan Choice, Rashid Abdul akisema neno la ufunguzi wa mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea kiwandnai hapo.
Waziri alieleza kuwa huo ni uwekezaji mkubwa wenye tija ambapo hadi sasa umegharimu zaidi ya Tshs bilioni 25, hivyo ni kiwanda cha mfano kwa nchi za Afrika ya Kati na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufikia malengo ya kiwanda hicho.
Aidha Msemaji wa Mradi huo alieleza uwepo wa kiwanda hicho ulizingatia mahitaji ya nyama bora na mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyopo nchini kwa kuzingatia umuhimu wa wawekezaji na wafanyabiashara.
Msemaji wa kiwanda cha kuchakata nyama cha Tan Choice Bw. Albert Kilalah akikabidhi taarifa ya kiwanda hicho kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki wakati wa ziara yake ya kikazi kiwandani hapo.
“Bodi ya Tan Choice ilivutiwa uwekezaji kwenye sekta ya nyama kutokana na uwepo wa mazingira rafiki ya uwekezaji nchini chini ya Serikali ya Awamu ya Tano na uwepo wa mifugo itayowezesha uendeshaji wa miradi huu na kukidhi soko la ndani na nje ya nchi,” alisema Bw. Albert Kilalah
Alieleza kiwanda hicho ni fursa kwa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo nchini ambapo zaidi ya watu 10000 watanufaika kiuchumi kwa kuzingatia uhakika wa soko la nyama na mazao yatokanayo na mifugo.
Sehemu ya washiriki wa mkutano wakimsikiliza hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (hayupopichani) wakati wa ziara yake katika kiwanda cha TAN CHOICE.
Alifafanua, Kiwanda hicho kitakuwa cha pili kwa ukumbwa kwa nchi za Africa Mashariki kikifuatiwa na kiwanda cha Ethiopia ambacho kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 3,000, kondoo na mbuzi 6,000 kuzalisha zaidi ya tani 300 kwa siku.
“Kiwanda kitakapokamilika kitakuwa kikubwa na bora cha aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 1,000 na mbuzi na kondoo 4,500 kwa siku nyama na mazao mengine yatakayozaliswa na kiwanda yatazingatia ubora na usalama,”alisema Kilalah.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Evarist Ndikilo akizungumza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipomtembelea ofisi kwake wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kutembelea maeneo ya uwekezaji ikiwemo viwanda vilivyopo katika mkoa huo.
Alisema kuwa, Tan Choice inatarajia kuuza nyama soko la nchi za Uarabuni Mashariki ya Kati ikiwemo Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia pamoja na masoko yatakayo jitokeza ikiwemo China, Malaysia, Vietnam na Indonesia pamoja kutumia fursa ya soko huru la kibiashara litakaloazishwa barani Afrika na kuuza nyama hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Serikalini pamoja na watendaji wa kiwanda cha kuchakata nyama na machinjio ya TAN CHOICE mara baada ya kumaliza ziara yake kiwandani hapo Januari 17, 2020.Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Asupter Mshama na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu kiwanda hicho Bw. Rashid Abdul.
Akihitimisha taarifa hiyo aliomba Serikali kuendelea kuboresha barabara kutoka eneo la kiwanda hadi Kongowe iboreshwe kwa viwango vya lami ili kurahisisha usafirishaji wa mifugo kiwandani na pamoja na nyama zitakazozalishwa kwenda uwanja wa ndege, bandarini na masoko ya ndani.
Aidha aliomba kuwe na uboreshwaji wa minada ili kuwe na uhakika wa upatikanaji wa wanyama wengi na wenye uhakika.
Mratibu wa Mradi katika kiwanda cha Tan Choice Dkt. Juma Mtei akitoa maelezo ya kiwanda cha kuchakata nyama cha Tan Choice kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki wakati wa ziara yake ya kikazi kiwandani hapo,Januari 17, 2020.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Asupter Mshama alishukuru wawekezaji katika Wilaya yake, na kuwatoa shaka juu ya utatuzi wa changamoto walizonazo na kuendelea kuunga mkono jitihada zao kwa kuhakikisha huduma muhimu ikiwemo, nishati ya umeme, maji, barabara na mawasilino vinazingatiwa ili kuwa na manufaa ya uzalishaji wa kiwanda.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
Post a Comment