TANZANIA IMEPIGA HATUA KUBWA KATIKA KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO YA MWAKA 2025 - RAIS MAGUFULI
Rais Magufuli amesema miaka 4 ya tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020, mipango ya kimataifa na kikanda na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka 5 (2016/17 – 2020/21) iliyolenga kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Rais Dkt. John Magufuli amesema hayo tarehe 21 Januari, 2020 katika hafla ya kuukaribisha Mwaka Mpya aliyowaandalia Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa (Diplomatic Sherry Party) na kufanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Waakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party
Rais ametaja baada ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi, kuimarisha Muungano ambao Aprili 2020 utatimiza miaka 56, ukuaji mzuri wa uchumi wa wastani wa asilimia 7, kudhibiti mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 3.5 na kuongeza akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani Bilioni 4.123 hadi kufikia Dola za Marekani 5.579 zinazotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi 6.3.
Kiongozi wa Mabalozi (Dean of Diplomatic Corps) Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih akizungumza katika Diplomatic Sherry Party.
Mafanikio mengine ya kiuchumi ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi Bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi Trilioni 1.5 (ambapo Desemba 2019 ilifikia shilingi Trilioni 1.9), kuvutia uwekezaji wenye thamani ya shilingi Trilioni 30 uliozalisha ajira laki 1, kuogeza biashara ya nje kutoka shilingi Trilioni 11.5 hadi kufikia shilingi Trilioni 16.6, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara kutoka tani 796,512 hadi kufikia tani 1,141,774 (ongezeko la asilimia 43.3) na kujenga viwanda vipya 4,877.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Waakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party
Aidha, katika kipindi hicho mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.469 hadi kufikia Bilioni 1.743, mapato ya Serikali kutokana na madini yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 168 hadi kufikia shilingi Bilioni 346, idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii Milioni 1.1 hadi kufikia Milioni 1.5 na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.9 hadi kufikia Bilioni 2.488.
Rais Magufuli ameongeza kuwa katika kipindi hicho Serikali imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu zaidi ya shilingi Trilioni 7, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme utakaogharimu shilingi Trilioni 6.5, ujenzi wa kilometa 2,500 za barabara za lami na nyingine 2,400 zikiendelea kujengwa, kilometa 7,087 la barabara za lami zikiwa katika maandalizi ya kuanza kujenzi na kukamilisha ujenzi wa madaraja makubwa 8.
Miradi mingine ni kufufua reli ya Dar es Salaam – Tanga – Moshi iliyokuwa haitoi huduma tangu miaka zaidi ya 20 iliyopita, kupanua bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, kukarabati meli 7 katika maziwa makuu, kukamilisha ujenzi wa jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (Terminal III), kujenga viwanja vya ndege 11, kununua rada 4, na kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) baada ya kununua ndege mpya 11.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Waakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party)
Kwa upande wa huduma za kijamii amesema mbali na kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, Serikali imejenga njia ya umeme ya Iringa – Shinyanga, Makambako – Songea na Lindi – Mtwara, kupeleka umeme vijijini ambapo idadi ya vijiji vilivyofikiwa na umeme imeongezeka kutoka 2,018 hadi kufikia 8,587, kujenga vituo vya afya 352 na Hospitali za Wilaya 69, kuajiri watumishi wa afya 8,000 na kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270 kwa mwaka.
Amebainisha kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo imeshatumia shilingi Trilioni 1, mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 341 hadi kufikia shilingi Bilioni 450, imetekeleza miradi ya maji yenye thamani ya shilingi Trilioni 3 na hivyo kuongeza upatikanaji wa maji kutoka wastani wa asilimia 56 hadi kufikia asilimia 71, kuongeza mapambano dhidi ya rushwa na Serikali kuhamia Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kuongozwa na sera ya diplomasia ya uchumi, Tanzania imeendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na nchi mbalimbali duniani ambapo pamoja na kufanya ziara katika nchi mbalimbali, Balozi mpya 7 zimefunguliwa na kushiriki katika shughuli na mipango mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ulinzi wa amani ambapo kwa sasa askari 2,297 wa Tanzania wapo katika ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali.
Baadhi ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party)
Ameahidi kuwa katika mwaka 2020 Serikali imejipanga kuendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kudumisha amani na usalama, kukuza zaidi uchumi, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kukuza sekta kuu za uzalishaji yaani kilimo, viwanda, ujenzi, madini na utalii pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ambapo amewaomba Mabalozi hao kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi zao kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Pia, amewahakikishia kuwa katika mwaka 2020 ambapo Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu, Serikali imejipanga kuhakikisha unafanyika kwa misingi ya kidemokrasia na katika mazingira ya amani, uhuru na haki, na amezikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia jinsi Tanzania ilivyokomaa kidemokrasia pindi wakati ukifika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kabla ya chakula cha jioni alichowaandalia Mabalozi hao katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party) zilizofanyika katika Ukumbi wa Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party) zilizofanyika katika Ukumbi wa Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ameahidi kuwa Tanzania, itaendelea kukuza ujirani mwema, kushirikiana na nchi mbalimbali na kutekeleza majukumu ya kimataifa ikiwemo kuwahudumia wakimbizi na kuwarejesha makwao kwa hiari, lakini ameeleza kusikitishwa na hujuma na propaganda zinafanyika kwa lengo la kwamisha zoezi hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi hao, Kiongozi wa Mabalozi (Dean of Diplomatic Corps) Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri aliouonesha katika kipindi cha miaka minne ambapo miradi mikubwa ya maendeleo imetekelezwa, kukua kwa uchumi, ustawi wa watu na ameahidi kuwa Mabalozi wataendelea kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
(PICHA ZOTE NA IKULU)
Post a Comment