Ads

SERIKALI YAINGIA MIKATABA 9 NA BARRICK: UGUMU WA MAJADILIANO NUSRA PROFESA KABUDI AJIUZULU !



Na  Mwandishi Maalum, Ikulu Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi

Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuna wakati aliandika barua ya kujiuzulu lakini alinyang’anywa na ikachanwa.

Profesa Kabudi  ameeleza hayo leo Ijumaa Januari 24, 2020 Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Kamati ya Madini ya Barrick.

Waziri Kabudi amesema alichukua uamuzi wa kuandika barua hiyo baada ya mchakato wa majadiliano na wajumbe wa Barrick kuwa magumu na kwamba aliona aibu kushindwa kazi aliyotumwa.

Amemtaja aliyemnyang’anya barua hiyo ambayo haikuifafanua kwa kina ni Kasmir Simbakuki.

“Nilifikia hatua nikafanya dhambi ya kukata tamaa nikasema jambo hili haliwezekani, niliona ni bora aibu na fedheha hiyo niibebe lakini barua niliyoandika sikufanikiwa kuileta.”

“Nilisema sijawahi kutumwa kazi na mkuu wangu wa nchi ikanishinda,” alisema Profesa Kabudi.

UTIAJI SAINI WA MAKUBALIANO KATI YA SERIKALI YA TANZANIA NA KAMPUNI YA MADINI YA BARRICK KATIKA PICHA:






Alisema wakati huo alikuwa katika wakati mgumu kwani Rais wa Tanzania, John Magufuli alikuwa akiuliza mambo yanayoendelea na huku Bungeni Wabunge wakihoji majadiliano ambayo wakati huo hayakuwa yakienda vizuri.

“Kuna wakati walikuja Wachina tofauti wa kuwekeza tukaongea nao ila wakaingia mitini, huku Bungeni unapigwa mijeledi, huku Wachina wale wameingia mitini, huku Rais anasubiri umalize, huku unajiuliza utatoka kwa aibu ila Mungu akasimama na sisi,” alisisitiza Waziri Kabudi.

Waziri huyo aliomba radhi kwa lolote litakalopungua, akibainisha kuwa utakuwa upungufu wa kibinadamu, “ila tulifanya kazi kwa moyo wote na akili zote.”

Alisema katika hafla hiyo itasainiwa mikataba tisa.

Rais Magufuli wakati akianza kuzungumza baada ya kukamilika kwa utiaji saini huo aligusia suala la Profesa Kabudi, “ni kweli mengine Kabudi hajayasema, nilikuwa nampigia simu usiku na simu zake zote alikuwa akipokea ni matusi lakini nashukuru amekuwa mvumilivu, hongera sana Kabudi. Watanzania wavumilivu wapo.”

   

 

 


No comments