Matangazo ya mitandao ni fursa ya kukuza biashara yako!
Na Peter Mmbaga
Mitandao ya kijamii ni njia ya biashara inayokuwa kwa kasi tofauti na kipindi inaanza mnamo mwaka 2004 Facebook alipotangulia, hapa nyumbani pia biashara zimerahisishwa zaidi kupitia majukwaa mbalimbali.
Si ajabu ukakutana na kijana hana duka la nguo, simu au bidhaa yoyote lakini jukwaa la Instagram au Facebook ndio duka lake. Unashangaa? Kinachompa biashara ni watu waliomfuata (followers) wakiwa 5,000 tu ni mtaji tosha, haimaanishi atauzia wote 5,000; anaweza kuuzia watu 100 tu, hao wengine atawapata kwa kushea (share) na kwa kutangaza ukurasa wake au ‘post’ yake.
Njia ya haraka na itakayomwezesha ni kupitia matangazo ya kulipia (paid advertising) na kupata wateja wapya kwa bajeti ndogo. Kama una Tsh 10,000/ utapata tangazo la thamani yako, vilevile kwa mwenye Tsh 50,000/ na zaidi. Na ukiangalia soko letu, Facebook na Instagram ndizo zenye watumiaji wengi, unaweza tumia bajeti hiyo hiyo kwenye mitandao yote miwili ikiwa akaunti zitakuwa zimeunganishwa (linked).
Katika ulimwengu huu wa teknolojia yawezekana mwenye jukwaa la Instagram akapata faida zaidi ya mwenye bidhaa/ huduma, hii ni kwasababu tangazo litapata nafasi ya kuonwa na watu wengi zaidi katika maeneo mengi zaidi ya duka la bidhaa lilipo.
Ni kwasababu, una uhakika wa kujua tabia za watumiaji mitandao, muda gani wanakuwa mtandaoni,mtandao upi wanapenda, wanakaa wapi, wana umri na jinsia gani. Mfano mtandao wa Instagram wenye watumiaji hai zaidi ya bilioni 1 kwa mwezi unakuonyesha twakimu hizo katika mchakato wa kulipia tangazo lako. Kimjini mjini tunasema ni namna ya ‘kuji-position’ tu!
Mitandao ya kijamii ina data za kutosha kuhusu watumiaji wake, dunia haina siri kabisa. Hivyo kupitia matangazo ya kulipia ambayo hupelekea kuwafikia watumiaji wapya ambao hujawajakufuata, ni rahisi ukishalipia tangazo lako ambalo umetengeza kwa bajeti yako kwa kuangalia taarifa muhimu kama vile umri, aina ya bidhaa wapendayo, eneo, jinsia (gender) n.k
Kama bidhaa yako ni ya hereni wateja wa kipaumbele watakuwa wanawake hivyo kwenye suala la jinsia itakuwa ni rahisi kuwafikia.
Biashara inafanyika kiurahisi kwakuwa haihitaji kwenda shule, mtandao umerahisisha kila kitu, kwa mfano mtandao wa Instagram unakupa chaguo la kutoka kwenye akaunti binafsi (personal account) na kwenda kwenye akaunti ya biashara (business account) yenye twakimu zote.
Twakimu hizo ni za ufahamu (insight) kuhusu kile kifanyikacho kwenye akaunti yako, taarifa za msingi za watu wapya wanaofuata akaunti yako (profile visit) au kama una website itaonyesha (website visit), wangapi wamefikiwa (reach), muda gani, mkoa au nchi gani, bidhaa (product) ipi inapendelewa na wanaokupigia simu (calls), wanaoku-DM au baruapepe watakazokutumia n.k. Waingereza wanasema , ‘numbers do not lie’.
Usiumize kichwa, kupitia darasa la bure la Google na Facebook analytics unajua ni namna gani hayo hufanyika, kama vile unawezaje kulipia tangazo kwa bei ya kitanzania na upate faida.
Pia, kuhusu muda ni jinsi ‘unavyo-jiposition’ kwa wateja, muda wowote baada ya kuwasoma wadau unaweza ukaposti, ukiamua mara 3 kwa siku kila baada ya masaa manne ni sawa, haina masharti ni maamuzi yako. Vyovyote vile, kifupi haubanwi na mambo yako mengine, ukitofautisha na njia nyingine za kutangaza. Na mara nyingi simu yako uko nayo. Umeibeba dunia ya mtandaoni mkononi mwako!
Kwa mujibu wa mtandao wa Statica, katika robo ya tatu ya mwaka 2019 Facebook walikuwa na watumiaji hai kila mwezi wapatao bilioni 2.45. Facebook inaongoza kwenye mitandao ya kijamii tangu ilipoanzishwa, ilikuwa ya kwanza kufikisha watumiaji hai bilioni moja kwenye robo ya tatu ya mwaka 2012. Na kupitia taarifa ya kampuni hiyo iliyoeleza kuwa watumiaji hai billioni 2.8 ndio hutumia japo bidhaa zingine za kampuni hiyo (Facebook, WhatsApp, Instagram, au Messenger) kila mwezi, inaonyesha biashara kupitia mtandao inaahidi (promising) kutokana na watumiaji kuongezeka kila wakati, hivyo uhakika wa soko upo.
Kwa mujibu wa tafiti Napolean cat ya Desemba 2019 watumiaji wa Facebook hapa nchini wanafikia milioni 4.59, hata kwa idadi hii ukiwekeza, faida utaiona!
Hii inaonyesha biashara inalipa kwa uwekezaji (return on investment) unaofanya kupita matangazo ikiwa tu utaamua kuwekeza katika kuandaa maudhui yanayoendana na wakati, mahitaji na aina ya wateja ili kutengeza maingiliano baina yenu, kwa taarifa zinazohusu bidhaa, au lolote linaloingiliana na bidhaa. Mfano kinywaji baridi ukikifungamanisha na chakula na joto la Dar au pengine utani kidogo (funny stories), lazima utapata wateja, usiwe ‘kiprofeshino’ muda wote!
Kingine, hufikia watu sahihi (targeted audience), mara nyingi wanaokufata sio lazima wawe wateja. Unaweza kuwa na nusu wateja sahihi na nusu sio lakini tangazo la kulipia linatoa uchaguzi wa nani apate maudhui yako na kwasababu gani; jinsia, umri n.k hivi vitasaidia kuwapata walengwa, itakuwa rahisi kufanya biashara.
Watu au kampuni nyingi haziamini kwenye kulipia matangazo wakijiamini kuwa bidhaa/ huduma zao hujulikana hivyo hutegemea ‘organic followers’ ambao wapo au watakaokufuata kwa matumizi ya maneno muhimu, ‘hashtags’ kwa matokeo ya injini za utafutaji (search engine optimization) ili kufikia kundi fulani, hivyo hufikia watu wachache.
Pengine, hata kama chapa (brand) ni kubwa, wekeza; si kuwapata wateja wapya bali hata maongezi mtandaoni (conversation) husaidia kuiweka chapa yako hai, hivyo kuishi muda mrefu vichwani. Kwa kufanya kwangu ushauri (consultation) kupitia mitandao ya kijamii kwenye makampuni na matukio kadhaa asilimia kubwa wengi hawaamini kwenye matangazo ya kulipia, wanahisi ni upotezaji wa fedha lakini baadae hugundua faida yake wakiwa wamechelewa.
Matangazo ya kulipia yana faida ila muda mwingine hukera au huchosha kutokana na fursa ya mitandao kuwa eneo la kibiashara kuwa kubwa, kila dakika ukiwa mtandaoni kuna tangazo linaloruka au kurushwa (pop ups ads). Lipia kwa kipimo!
(Mwandishi ni mshauri (consultant) wa maudhui, mahusiano ya umma (PR) na mitandao ya kijamii, anapatikana kupitia nambari +255 656 859 045 au barua pepe: petermmbaga29@gmail.com)
Post a Comment