Ads

TAARIFA KWA UMMA MKAKATI WA KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA KORONA KWA TRENI, MAGARI YA ABIRIA NA MIZIGO




Katika kutekeleza Agizo la Mhe. Eng. Isack Aloyce
Kamwelwe, (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, alilotoa tarehe 18 Machi, 2020 juu ya kujikinga
na maambukizi ya virusi vya Korona kwenye vyombo vya
usafiri na usafirishaji Nchini, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri
Ardhini, imekutana na Wadau wa Usafiri na Usafirishaji
Nchini, kutafakari na kuweka mikakati ya kukabiliana na
janga hili.

Wamiliki wote wa vyombo vya usafiri na usafirishaji, mashirika
ya reli Nchini na wafanyakazi wao wanaagizwa kuzingatia na
kutekeleza yafuatayo:

1. Wamiliki wa mabasi wanyunyizie dawa za kuua virusi
katika mabasi yao kila mwisho wa safari.

2. Shirika la Reli Tanzania – TRC na Mamlaka ya Reli ya
Tanzania na Zambia – TAZARA wahakikishe kuwa treni
zinapuliziwa dawa za kuua virusi kila mwisho wa safari

3. Watu wote wanaoingia na wanaotoka vituo vikuu vya
mabasi na treni wanawe mikono kwa maji yanayotiririka
na sabuni;

4. Kila basi liwe na dawa ya kuua virusi mikononi (hand
sanitizer), kabla ya abiria kuingia ndani ya basi, asafishe
mikono kwa dawa ya kuua virusi mikononi;

5. Waendesha taxi, pikipiki za magurudumu mawili na
matatu, wahakikishe kuwa abiria wanapaka dawa ya
kuua virusi mikononi (hand sanitizer) kabla ya kupanda
kwenye chombo husika;

6. Magari ya mizigo hayaruhusiwi kubeba abiria yeyote;

7. Idadi ya abiria wanaoruhusiwa kwa mabasi yanayosafiri
kutoka mkoa kwenda mkoa mwingine ni kulingana na
idadi ya viti vilivyopo kwenye basi tu.

8. Idadi ya abiria wanaosafiri kutoka mijini kuelekea
sehemu za vijijini ni kulingana na idadi ya viti vilivyopo
kwenye basi tu;

9. Mabasi yaendayo Haraka (BRT) yabebe idadi ya abiria
kulingana na idadi iliyoainishwa kwenye leseni zake;

10.Mabasi yote ya mijini (daladala) yabebe abiria kulingana
na idadi ya viti katika basi (level seat);

11.Elimu juu ya kujikinga na virusi vya Korona itolewe ndani
ya vyombo vya usafiri kwa kutumia Redio na Runinga
zilizopo kwenye vyombo hivyo.

12.Abiria wasiingie na wasindikizaji ndani ya vituo vikuu vya
mabasi na treni;

Mamlaka inashirikiana na Mamlaka ya Usambazaji wa
Madawa Nchini - MSD kuhakikisha dawa ya kuua virusi
mikononi (hand sanitizer) inapatikana kwenye maduka ya
madawa yaliyopo karibu na vituo vikuu vyote vya mabasi Nchini
ili wamiliki wa vyombo vya usafiri waweze kununua na
kuvitumia kwa urahisi.

Kamati ya pamoja iliyoundwa kwa kushirikiana na wadau
wengine itaendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo haya na
kufanya kaguzi mbalimbali ili kuhakikisha utekelezaji sahihi
kwa wakati.

Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
LATRA
19 Machi, 2020


No comments