Ads

TAARIFA YA TEF KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU CORONA





Deodatus Balile Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeshitushwa na habari za kuwapo kwa ugonjwa
wa Virusi vya Corona (COVID-19) nchini. Habari hizi ni mbaya kwa kuwa mataifa
yaliyoathiriwa na virusi hivyo kumetokea vifo vingi, mateso makubwa kwa watu na
kuharibu uchumi kwa kiwango kikubwa.
Tanzania, kama yalivyo mataifa mengi duniani, maambukizi ya COVID-19 yamewapata
baadhi ya watu. Ingawa maambukizi yapo kiwango cha chini nchini ikilinganishwa na
nchi nyingine, bado tunahitaji kuchukua hatua madhubuti kuzuia maambukizi mapya
nchini kwetu. Kwa kutambua hali hii, Jukwaa la Wahariri Tanzania tunapenda kueleza
yafuatayo:-

(1) Pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vya habari hadi sasa hapa nchini,
tunawasihi Wahariri wote kuendelea kutoa habari za ugonjwa wa COVID-19, hasa njia
za kuzuia maambukizi na kukabiliana na ugonjwa huu. Hii iwe ajenda ya kudumu kwenye
vyombo vya habari hadi utakapotokomezwa.

(2) Tunatoa rai kwa waandishi wa habari wote nchini na watu wanaomiliki mitandao
ya kijamii zikiwamo blogs, twitter accounts, WhatsApp, Instagram na mitandao mingine
ya kijamii kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi bila kuziongezea chumvi.

(3) Tunatoa rai kwa viongozi wa dini na wa kisiasa kuchukua hatua muhimu za
kuelimisha waumini na wafuasi wao juu ya janga la Corona. Pia tunawahimiza viongozi
kuwakumbusha waamini wao kanuni za kukabiliana na maambukizi ya Corona.

(4) Kuna maeneo yanayoweza kuwa hatarishi kama hatua za haraka za kujikinga na
virusi hivi hazitachukuliwa. Baadhi ya maeneo hayo ni vituo vya daladala, mwendokasi,
pantoni na kwenye masoko hakuna maji ya kunawa mikono kama ambavyo Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilivyoagiza. Tunaomba serikali
ihakikishe maeneo haya yenye msongamano mkubwa yanawekewa vifaa vya kusafisha
mikono kuepusha maambukizi ya Corona

(5) Tunajua na kutambua kwamba hadi sasa serikali haijasema lolote juu ya
mikusanyiko katika nyumba za ibada kama misikitini na makanisani. Katika maeneo haya
kuna msongamano wa watu. Kuna nchi tunaambiwa maambukizi makubwa yalitokea
kwenye nyumba za ibada. Pamoja na viongozi wa kidini kutoa miongozo ya ibada,
tunaiomba serikali itoe maelekezo mahususi kwa viongozi hao ili wachukue hatua
madhubuti za kukinga waumini dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

(6) Tunatoa mwito kwa kila mwananchi kutambua kuwa usalama wa afya yake uko
mikononi mwake, kwa maana hiyo kila mmoja kuanzia ngazi ya familia ana wajibu wa
kuzingatia masharti ya kukabiliana na Corona.

(7) Tunapongeza na kuunga mkono hatua ambazo zimekuchukuliwa na Serikali
kupambana na maambukizi ya virusi hivi. Hatua hizi ni pamoja na kupima wasafiri
wanaotoka ng’ambo katika viwanja vya ndege; kufunga shule na vyuo vyote nchini na
kutoa maelekezo muhimu kwa wananchi juu ya njia za kujikinga dhidi ya maambukizi ya
virusi vya Corona.

(8) Tunavipongeza vyombo vya habari kwa kutoa kipaumbele kwa habari zinazohusu
ugonjwa huu. Wahariri na waandishi wamekuwa mstari wa mbele katika kudadisi habari
za Corona na kuziweka wazi kuwajengea wananchi uelewa wa virusi vya Corona na
kuwaondolea hofu. Dhima ya vyombo vya habari sasa iendelee kuwa ni kuhabarisha
umma namna ya kukabiliana na maambukizi mapya, badala ya kutoa habari zenye
kuwajaza hofu wananchi. Tukizingatia haya tutaushinda ndani ya muda mfupi ugonjwa
huu ambao umeleta athari kubwa za kijamii na kiuchumi. Mungu ibariki Tanzania.

Imetolewa na:
Deodatus Balile
Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania
Dar es Salaam, Machi 19, 2020


No comments