Mh. JAJI MARK BOMANI: MWANASHERIA MKUU WA KWANZA MZALENDO NCHINI AFARIKI DUNIA!
Mzee wa Atikali katika makala hii ya Wasifu wa Marehemu Jaji Mark Bomani ameanisha yafuatayo:
Usuli:
Mh.Jaji mstaafu MARK DANHI BOMANI, mmoja wa viongozi waliolifanyia Taifa letu mambo mengi na aliyekuwa akijua mambo lukuki ya nchi yetu ambayo Watanzania wengi hawayajui, ameaga dunia jana usiku tarehe 10.9.2020 akiwa na umri wa miaka 88 kutokana na maradhi.
Je, Mh. BOMANI, mmoja wa Watanzania waliokuwa wakiheshimika sana nchini, alitokea wapi na mchango wake kwa Taifa ni upi?
Mark Bomani azaliwa:
MARK DANHI BOMANI alizaliwa siku ya Jumamosi, tarehe 2.1.1932 huko Uchashi, Bunda, mkoani Mara. Bomani ni mmoja wa watoto wa Mzee Bomani ambapo wengine ni Daniel, Paul, Emma, Francis, Martha, Yona, Washington, Fibe & Neema.
Safari ya Elimu ya Bomani:
Bomani alisoma shule ya msingi Mwamanyili, Nassa ambapo baba yake mzazi ndiye alikuwa mwalimu wake.
Shule ya Kati:
Mwaka 1945, serikali ya kikoloni ilijenga shule ya wavulana ya Bwiru na kuwataka wanafunzi wakafanye mtihani. Mzee Bomani, baba yake Mark, alimuomba jirani yao, Mzee Shitebo, ampeleke Mark kwa baiskeli kwenda kufanya mtihani huo na Mark akafanya mtihani na kuwa mmoja wa wanafunzi wa mwanzo 30 waliochaguliwa kujiunga na "Bwiru Boys". Jina la Bomani ndilo lililokuwa la kwanza kwenye orodha ya waliochaguliwa ikimaanisha yeye ndiye aliyepata alama za juu kuliko wote. Akiwa shuleni hapo, talanta ya uongozi ambayo Bomani alijaliwa na Mola wake ilianza kujionesha kwani alikuwa mmoja wa Viranja -Prefects.
Mwaka 1950, BOMANI alifanya mtihani wa darasa la 10. Kwavile alikuwa kipanga aliweza kupasua pepa na kuwa mmoja wa wanafunzi wawili (2) tu kati ya wanafunzi 30 wa "Bwiru Boys" waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na Tabora School, shule iliyokuwa bora na maarufu kuliko zote Tanganyika enzi hizo.
Elimu ya Sekondari
Bomani alipojiunga na "Tabora School" kwaajili ya elimu ya sekondari, alikutana na vijana hodari na 'vipanga' kama yeye. Darasa lao ndilo linahesabika kuwa na 'vipanga' kuliko madarasa yote katika historia ya shule hiyo. Katika darasa hilo, Mh. Edwin Mtei, aliyekuwa mwanafunzi bora nchini mwaka wao 'Tanganyika One' ndiye aliyekuwa akiongoza darasani.
Bomani akiwa shuleni hapo alikuwa 'Kiranja Mwandamizi' wa bweni. Walipofanya mtihani wa mwisho wa kumaliza shule, 'vipanga' 7 wa darasa hilo walichaguliwa kwenda Chuo cha Makerere nchini Uganda ambao ni EDWIN MTEI, MARK BOMANI, GEOFREY MMARI, J.PENDAEL, ROWLAND MWANJISI, O. MWAMBUNGU na G. SIMITI.
Chuoni Makerere
Bomani alisomea Uchumi na Siasa. Alipokuwa Mwaka wa Kwanza Mwai Kibaki alikuwa mwaka wa tatu. Mwai Kibaki alipasua pepa na kubakishwa chuoni hapo kama Msaidizi Mafunzo - Tutorial Assistant hivyo akamfundisha Bomani. Akiwa Makerere, Bomani talanta yake ya uongozi ilizidi kujitanabaisha kwani alikuwa Rais wa Umoja wa Wanafunzi (Makerere Students Guild). Baada ya kuhitimu vizuri masomo yake Makerere, BOMANI alikwenda Uingereza kusomea Sheria.
Uingereza
Bomani alienda London, Uingereza kusomea Sheria kwenye Chuo cha "London University". Akiwa huko, akakutana na CHARLES NJONJO ( aliyekuja kuwa Mwanaheria Mkuu wa Kenya-1963) na alikutana tena na Mwai Kibaki (aliyekuja kuwa Rais wa Kenya) aliyekwenda kusomea Shahada ya Uzamili ya Uchumi katika Chuo cha: 'London School of Economics'.
Bomani Akutana na Kambona
Akiwa Uingereza, Bomani alikutana na Oscar Kambona aliyekwenda huko pia kusomea Sheria. Bomani awa Mpambe wa Harusi ya Kambona! Tarehe 19.11.1960, Bw. Oscar Kambona alifunga ndoa ya kukata na shoka na Bi. Flora Urio huko Uingereza. Bi Flora alikuwa ni binti mrembo aliyewahi kushinda taji la Msichana Mlimbwende wa Tanganyika . Bomani ndiye alikuwa mpambe wa Kambona . Mwalimu Nyerere, aliyekuwa Uingereza kuhimiza uhuru wa Tanganyika, ndiye aliyemtoa Bi. Flora siku ya harusi katika Kanisa la Mtakatifu Paulo( St. Paul's Cathedral). Harusi hiyo ilikuwa ya kipekee na iliandikwa sana kwenye magazeti ya Uingereza. Bomani arejea Nchini Bomani alihitimu vizuri masomo yake ya Sheria ikiwa ni pamoja na mafunzo Lincoln's Inn na kurejea nchini mwaka 1962. Bomani awa Mtanganyika wa 3 Kuwa Wakili Bomani aliporudi nchini aliapishwa kuwa Wakili tarehe 21.1.1962. Bomani akawa Mtanganyika wa tatu kuwa Wakili baada ya Humphrey Mkondya na Juma Mawalla. Bw. Bomani aanza Kazi ya Uwakili Mara tu baada ya kuapishwa, Bw. Bomani alifanya kazi ya uwakili wa kujitegemea mjini Mwanza lakini baadaye akaitwa kufanya kazi serikalini. Mh. Bomani ateuliwa Naibu Mwanasheria Mkuu Rais Nyerere alimteua Bomani kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika mwaka 1963, huku Mwanasheria Mkuu akiwa Mzungu, Rowland Brown. Familia ya Bomani yaweka rekodi ya kuwa na Viongozi wawili Wakubwa Mwaka huo wa 1963, Rais Nyerere alimteua Mh. Paul Bomani kuwa Waziri wa Fedha. Hivyo, kwa Mh. Mark kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu maana yake familia ya Bomani ilikuwa ndiyo yenye ndugu wenye nyadhifa za juu kabisa serikalini. Mh. Bomani ashiriki kutayarishaji nyaraka za Muungano Kazi kubwa kabisa ya mwanzo aliyoifanya Mh. Bomani akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu ilikuwa ni kusaidiana na Mwanasheria Mkuu Bw. Brown kutayarisha nyaraka zote za kisheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kazi aliyoitekeleza kwa weledi wa hali ya juu. Mh. Bomani ateuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Mwaka 1965, Mh. BOMANI aliteuliwa na Rais NYERERE kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiwa na miaka 33 tu na bado akiwa bado mseja. Hivyo, Mh. Bomani akawa Mzalendo wa kwanza nchini kushika cheo hicho. Rais NYERERE amwagiza Mwanasheria Mkuu Bomani akatafute Jaji Mkuu Nje Baada ya nchi yetu kupata uhuru ilikuwa ni dhahiri kwamba hatukuwa na Wanasheria wa kutosha. Hii ni kwasababu Chuo pekee Afrika Mashariki enzi hizo kilikuwa cha Makerere ambacho kilifahamika kuwa Havard ya Afrika kilikuwa hakifundishi fani hiyo. Waliotaka kusomea Sheria ilibidi kwenda India au Uingereza. Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndio kwanza kilikuwa kimeanzishwa (25.10.1961). Hivyo, Mwalimu akamtuma Mwanasheria Mkuu Bomani aende nje ya nchi kutafuta Jaji Mkuu, baadhi ya Majaji na Mahakimu, kama Mh. Bomani alivyowahi kuelezea--: Mpaka wakati huo, Jaji Mkuu alikuwa Mzungu (Sir Ralph Windham). Aidha, Majaji wote walikuwa Wazungu na Mahakimu wengi walikuwa wazungu na Wahindi wachache. Mwalimu akanipa kazi ya kwenda nje kuwatafuta. Nilikwenda Nigeria, Sierra Leone na West Indies Mwanasheria Mkuu Bomani afanikiwa kumuibua Jaji Mkuu Ziara hiyo ya Mwanasheria Mkuu Bomani ilikuwa ni ya mafanikio makubwa kwani alifanikiwa kumpata mtu aliyekuwa na sifa za Jaji Mkuu, kama Mh. Bomani alivyoeleza-: Nilifanikiwa kumpata Bw. Telford Georges toka Trinidad & Tobago aliyekuwa na vigezo vyote vya Jaji Mkuu.
Mwanasheria Mkuu Bomani Afanikiwa Kumpata Jaji Mmoja na Mahakimu 20
Mwanasheria Mkuu Bomani alifanikiwa pia kumpata Jaji Gabriel Onyiuke wa Mahakama Kuu ya Nigeria na Mahakimu 20 toka Nigeria. Jaji Mkuu, Jaji Onyiuke na Mahakimu hao 20 walitusaidia sana kama Mh. Bomani alivyodadavua-: Jaji Mkuu Georges alifanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuweka msingi imara wa Idara ya Mahakama na Mahakimu hao 20 pia walitusaidia sana kupunguza wingi wa kesi.
Mwanasheria Mkuu BOMANI Afunga "Ndoa ya Mwaka" na Bi Rahma Mwapachu
Mwaka 1967, Mwanasheria Mkuu Bomani alifunga pingu za maisha na Bi. Rahma Mwapachu (dada wa Mh. Harrith Bakari na Balozi Juma Mwapachu). Harusi hii huenda ilikuwa ndio bora zaidi kuliko zote zilizofungwa miaka ya 60. Harusi hii ilikuwa na Wapambe wawili badala ya mmoja ambao walikuwa ni Mh. Charles Njonjo, Mwanasheria Mkuu wa Kenya, na Wakili Juma Mawalla, Mtanganyika wa kwanza kuwa 'Barrister', nchini Uingereza mwaka 1960.
Kuvunjwa Vyama Vya Ushirika Kulimkera Mno Mh. Paul Bomani
Mwaka 1968, serikali ilikuja na uamuzi wa kuvivunja vyama vya ushirika. Kitendo hiki kilimkera mno Mh. Paul Bomani aliyekuwa Waziri wa Ushirika na Muasisi wa Ushirika nchini hadi akaribie kuutema uwaziri, kama Mh. Bomani anavyoelezea- 'Uamuzi huo ulimsononesha sana kaka yangu Paul. Yeye akiwa Waziri mhusika na mimi nikiwa Mwanasheria Mkuu tulifanya mazungumzo magumu sana ikiwa ni pamoja na uwezekano wa yeye kujiuzulu. Lakini tukaona kujiuzulu kungeweza kuchafua hali ya hewa nchini hivyo tukakubaliana asijiuzulu".
Mwanasheria Mkuu Bomani aendesha Kesi ya Uhaini 1970
Mwanasheria Mkuu Bomani ndiye aliyeendesha kwa weledi mkubwa kesi ya kwanza ya Uhaini nchini iliyoanza kurindima Mahakama Kuu Jumatano, tarehe 24.6.1970 dhidi ya washtakiwa 7, akiwemo Oscar Kambona (Bomani alikuwa Mpambe wa Kambona) waliotaka kupindua serikali ya Rais Nyerere kati ya tarehe 4.3.1968 na 12.10.1969. Washtakiwa 4, akiwemo Bibi Titi Mohamed, walihukumiwa kifungo cha maisha, wawili miaka 10 na mmoja aliachiwa huru.
Sheria ya Ndoa 1971 Ilimuhenyesha Sana Mwanasheria Mkuu Bomani
Akiwa Mwanasheria Mkuu Mh. Bomani alishiriki kupitisha sheria mbalimbali. Moja ya sheria zilizomsumbua na kumkosesha usingizi ni Sheria ya Ndoa ya 1971 . Sheria hii ilikuja na vipengele vipya vilivyoonekana kukwaza watu mfano kuwatambua watoto wote, wa ndani na wa nje ya ndoa, kuwa wana haki sawa na pia haki sawa kwa mali ambazo mke na mume wamechuma pamoja. Mwishowe, sheria hiyo ikapitishwa na bunge.
Mwanasheria Mkuu Bomani ang'atuka Baada ya kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu kwa zaidi ya muongo mmoja
Mwanasheria Mkuu Bomani aliamua kung'atuka mwaka 1976 na Rais Nyerere akamkubalia-: Baada ya kuwa Mwanasheria Mkuu kwa zaidi ya miaka 10 niliona nitafute kitu kingine cha kufanya. Mwalimu akaniruhusu.
Mh. Bomani ajiunga na Umoja wa Mataifa -UN
UN iliunda Kitengo maalum cha kuwaandaa Wanamibia kuendesha nchi yao ikipata uhuru kwa kutoa mafunzo. Mh. Bomani akajiunga na kitengo hicho ambacho kilifundisha waliokuja kuwa Makatibu Wakuu wote na baadhi ya Mawaziri wa Namibia. Mh. Bomani awa Mshauri Mkuu wa Serikali ya Namibia Mh. Bomani alipata heshima ya kuteuliwa kuwa Mshauri Mkuu wa serikali ya Namibia kwa miaka 2 kabla ya kurejea nchini mwaka 1992.
Mh. Bomani ateuliwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam 10
Baada tu ya kurejea, Rais Ali Hassan Mwinyi alimteua Mh. Bomani kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba ya Wataalam 10 (Bara 5, ZNZ 5). Kamati hii ilileta mapendekezo mengi mujarab mfano: Rais aweze kushtakiwa iwapo ametumia vibaya madaraka yake (Impeachment) na Rais wa ZNZ asiwe Makamu wa Rais nk.
Mh. Bomani ateuliwa Mwenyekiti Kamati ya Kupitia sekta ya Sheria Mwaka 1993
Rais Mwinyi alimteua Mh. Bomani kuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya kupitia sekta yote ya Sheria. Kamati hii ilifanya kazi nzuri na kutoa mapendekezo yaliyokubaliwa mfano: uanzishwaji wa 'Shule ya Sheria-Law school'. Kutokana na ubora wa kazi hiyo, mwaka 1997 WB iliitisha mkutano Washington, Marekani wa nchi zilizoendelea ili kujifunza toka kwa Tanzania. Hii ilikuwa ni heshima kubwa kwa Mh. Bomani.
Rais Mwinyi amteua Mh. Bomani Mwenyekiti Tume ya Utangazaji Mwaka 1993
Rais Mwinyi alimteua Mh. Bomani kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji, ambako alihudumu hadi 2002.
Mh. Bomani na Kinyang'anyiro cha Urais 1995
Mwaka 1995, baadhi ya wananchi na marafiki wa Mh. Bomani walimuomba agombee Urais wa Tanzania lakini alisita kwani alikuwa ameishi sana nje (miaka 16). Shinikizo lilipokuwa kubwa, akachukua fomu. Mh. Bomani aweka rekodi ya Wadhamini Mh. Bomani alipata wadhamini 1,050 akifuatiwa na Mh. John Malecela(925), licha ya kwamba ni wadhamini 250 tu waliohitajika. Hii iliakisi kukubalika kwake nchini.
Kamati Kuu yafyeka majina 10
Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM walipitia majina ya wagombea 16 waliorudisha fomu za Urais na kupendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa - NEC majina 6 (J. Kikwete, B.Mkapa, C. Msuya, Pius Msekwa, J. Warioba na M. Bomani) na kuyafyeka majina 10.
Mh. Bomani awa wanne !
Katika upigaji kura kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa - NEC , Mh. Bomani alikuwa wa 4 baada ya Mh. J. Kikwete, B. Mkapa na C. Msuya.
Halmashauri Kuu ya Taifa - NEC ya mchinjia baharini Mh. Bomani
Kanuni ya Chama ilieleza kuwa "NEC ya CCM itapitisha majina yasiozidi 5 na kuyapeleka Mkutano Mkuu". Kwa vile Mh. Bomani alikuwa wa 4 basi aliamini jina lake nalo lingepelekwa Mkutano Mkuu. Aliumia sana-: 'Ghafla NEC ilibadili Kanuni na kuamua itafikisha Mkutano Mkuu majina 3 tu. Hivyo kalamu ya NEC ikapita juu ya jina langu. Niliumia sana'.
Wapambe Wamtaka Mh. Bomani ajitoe CCM!
Mh. Bomani alidadavua- 'Suala hilo lilileta utata mkubwa kwani baadhi ya mashabiki wangu na viongozi wa UVCCM walinitaka nijitoe CCM niunde chama kipya. Nilikataa'.
Baba wa Taifa amfariji Mh. Bomani
Baada ya Baba wa Taifa kuona wapambe wa Mh. Bomani wamefura kwa hasira na kuleta mtafaruki mkubwa viunga mbalimbali vya Idodomia, alimwita Mh. Bomani nyumbani:- "Hali hiyo ilimfanya Mwalimu aniite nyumbani kwake na kunisihi nisiuchukulie vibaya uamuzi huo wa NEC. Nilimwelewa".
Vyama vya Upinzani vya mnyemelea Mh. Bomani
Baada ya songombingo hiyo, vyama vya upinzani _havikulaza damu:- "Baadhi ya vyama vya upinzani vilinifuata na kuniomba niwe mgombea wao. Nilivikatalia kwavile nilikuwa na "principles" zangu".
Hatimaye, Mh. BOMANI alifanikiwa kuwatuliza wapambe wake waliokuwa na munkari na hivyo suala hilo likaisha.
Baba wa Taifa amwomba Mh. Bomani kuwa Msaidizi Wake
Mwishoni mwa 1995, UN & OAU vilimteua Mwalimu JK Nyerere kuwa Mpatanishi wa mgogoro wa Burundi. Mwalimu akamuomba Mh. Bomanu kuwa Msaidizi wake (Facilitator's Representative). Akakubali. Hivyo akaanza kutekeleza jukumu hilo na Mwalimu Mei 1996 Mwanza. Miundombinu hafifu ikafanya upatanishi uhamie Arusha. Hadi Mwalimu anafariki 14.10.1999, hakuna maafikiano yoyote yaliyofikiwa. Oktoba 1999, OAU ikamteua Mh. Nelson Mandela kuwa Mpatanishi mpya huku Mh. Bomani akimsaidia. Agosti 2000, pande husika walifikia makubaliano na kusaini mkataba.
Rais JK amteua Mh. Bomani Mwenyekiti Kamati ya Madini
Mwaka 2007, Rais Jakaya KIKWETE alimteua Mh. Bomani kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya watu 12 kupitia upya sera ya madini. Kamati ilifanya kazi yake nzuri na kutoa ripoti.
Mh. BOMANI taka Muundo wa Serikali 3!
Tarehe 13.6.2013, Mh. Bomani aliongea na waandishi wa habari na kuipongeza Tume ya Warioba kwa kupendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu- : "Huo ndio muundo unaofaa na hilo ndilo limekuwa pendekezo la Tume zote zilizowahi kuundwa kuhusu Muungano; yaani Tume ya Jaji Mkuu Nyalali 1991 na Kamati ya Jaji Robert Kisanga 1998".
Mh. Bomani alikuwa- 'The Most Senior Living Advocate in Tanzania'
Moja ya kazi ambazo alikuwa akizifanya Mh. Bomani ni ya uwakili kupitia Kampuni yake ya Uwakili 'Bomani & Company Advocates'. Mh. Bomani alikuwa ndiye _"The Most Senior Living Advocate " kwani aliapishwa tarehe 21.1.1962.
Mh. Bomani awa Mjumbe wa Bodi ya Udhamini CCM
Mwezi Julai 2018, licha ya umri mkubwa, Mh. BOMANI aliteuliwa kuwa mmoja wa Wajumbe watano wa Bodi ya Kwanza ya Udhamini ya CCM. Hii ilikuwa ni heshima kubwa sana kwake.
Familia ya Mh. Bomani
Mh. Bomani ameacha mke, Bi. Rahma Mwapachu Bomani na watoto watatu wa kiume ambao ni Heri (Mchumi aliyesomea Wales na aliwahi kuwa Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa KCB), Clement na Andrew . Tarehe 18.6.2016, Andrew aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mikakati na Mambo ya Nje wa chama cha upinzani cha UDP cha Mh. J. Cheyo, "Mzee wa Mapesa".
Bw. na Bi Bomani Washeherekea Miaka 50 ya Ndoa -GOLDEN Wedding Anniversary !
Mwezi Agosti 2017, Mh. Bomani na mkewe Bi Rahma walisheherekea miaka 50 ya ndoa yao nyumbani kwao Mikocheni.
Sherehe hiyo iliyofana ilihudhuriwa na viongozi wengi akiwemo Rais Mstaafu Mh. Ali Hassan Mwinyi na Mkewe Mama Siti Mwinyi.
Afya ya Mh. Bomani Yatetereka
Afya ya Mh. Bomani ilitetereka kutokana na umri na magonjwa na kupelekea kulazwa hospitali ya TMJ, Mikocheni. Naibu PM wa Namibia Amtembelea Mh Bomani Hospitalini Tarehe 3.12.2019, Bi Netumbo Nandi-Ndaitwah, Naibu Waziri Mkuu wa Namibia, alimtembelea Mh. Bomani hospitalini TMJ. Hii ilikuwa kuonesha uungwana kwani Mh. Bomani alilifanyia mambo makubwa Taifa la Namibia. Mh. Bomani Afariki Baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, Mh. Bomani alifariki dunia usiku wa tarehe 10.9.2020.
Hili ndio hitimisho la shujaa wetu aliyetangulia mbele ya haki.
Huyu ndie Mh. MARK DANHI BOMANI, mmoja wa wasomi wa kwanza kabisa nchini aliyeheshimika vilivyo kutokana na kutoa mchango mkubwa, ndani na nje ya nchi. Baba wa Taifa alimuamini sana na kumpa majukumu mazito huku akiwa kijana mdogo na pia Marais wengine walimteua kuwa Mwenyekiti kwenye Kamati mbalimbali ikionesha walivyomuamini na akahudumu kwa weledi wa hali ya juu!
Mh. MARK DANHI BOMANI:- UMEVIPIGA VITA VILIVYO VIZURI, MWENDO UMEUMALIZA PUMZIKA KWA AMANI!
Post a Comment